• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Xidi na Hongcun, "vijii vya kale vilivyo kwenye michoro"

    (GMT+08:00) 2016-01-18 21:10:34

    Katika kipindi cha leo, tutatembelea kwa pamoja vijiji vya kale Xidi na Hongcun, vilivyoko wilaya ya Yi, mashariki mwa mkoa wa Anhui, ambavyo vinasifiwa kuwa ni "vijiji vilivyoko kwenye michoro".

    Makazi ya kale katika vijiji hivyo yalichukuliwa kuwa ni mali ya urithi wa utamaduni duniani, ambayo ni mara ya kwanza kwa makazi ya watu kupewa sifa hiyo duniani. Xidi na Hongcun ni vijiji vyenye umaalumu na uwakilishi zaidi wa mtindo wa makazi ya Anhui, na vinajulikana duniani kutokana na mandhari nzuri ya kimaumbile, hali yake ya kiasili iliyohifadhiwa vizuri kama ilivyokuwa wakati wa kale, na makazi yenye mapambo mbalimbali yaliyochongwa kwa mbao na undani wake maalumu wa kihistoria na kiutamaduni.

    Wimbo wa kienyeji ulikuwa unasikika mara baada ya kuingia kijiji cha Hongcun, kwenye barabara ya mawe anaonekana mzee mmoja aliyevaa nguo nyeusi na kofia ya kijani. Mzee huyu mwenye umri wa miaka 75 anaitwa Lu Rulin, ameuza mikate kwa miaka mingi kijijini humo. Tulimwona akiingia kijijini huko akiimba wimbo aliotunga mwenyewe, ambao umetukumbusha mara moja picha ya vijiji vya kale vilivyooneshwa katika mashairi ya kale ya China.

    Mzee Lu mwenyewe ni kama historia ya kijiji hicho, ametuelezea kuhusu urembo wa vijiji vya Xidi na Hongcun unaobeba utamaduni wa kale wa Huizhou.

    "mshairi mashuhuri wa kale Libai aliandika shairi moja kuhusu wilaya yetu ya Yi akisema: Wilaya ya Yi ni bustani ya peponi, miale ya jua yang'aa mbali, mimea mbalimbali bora inakua, watu hupendelea mavazi ya kale."

    Mshairi wa enzi ya Tang, Libai, alisifu sana mandhari nzuri iliyo kama peponi ya wilaya hiyo, ambayo pia inadhihirisha historia ndefu ya sehemu hiyo. Kijiji cha Hongcun cha wilaya hiyo ni kijiji cha ajabu ambacho mifereji ya maji inayozunguka kijiji hicho ina umbo la ng'ombe. Kijiji hicho kina eneo la hekta kama 30 hivi. Katika enzi ya Song ya kusini, wanakijiji wa Hongcun walijenga mfumo huo wa mifereji ambao ni wa pekee nchini China. Mwongoza watalii msichana Yuhuan alifafanua umbo hilo akisema:

    "umbo la kijiji kizima linaonekana kama ng'ombe, ambao milima ni kichwa chake, miti ni pembe zake, majengo ni mwili wake na madaraja ni miguu yake."

    Ukiangalia kijiji cha Hongcun kutoka angani, kinaonakana kama ng'ombe aliyelala kando ya mlima na mto.

    Ukiingia kijijini hapo, mitaa ya kale yenye barabara ya mawe, pamoja na nyumba zenye ukuta mweupe na vigae vyeusi ni kama michoro unayoiona taratibu mbele yako, na kukufanya ufikiri zama zilizopita wakati wa enzi ya Ming na Qing ya miaka mia kadhaa iliyopita. Mzee Wang Senqiang mwenye umri wa miaka 66 ameishi kijijini humo tangu kuzaliwa, na vizazi kadhaa vya familia yake vyote viliishi katika nyumba moja ya kale yenye mapambo mbalimbali yaliyochongwa, anasema:

    "nyumba yetu ya kale inaitwa "Shu Ren Tang", ilijengwa na babu yangu baada ya kuteuliwa kuwa ofisa wa serikali ya enzi ya Qing, umaalumu dhahiri wa nyumba za hapa Huizhou ni kwamba, kila nyumba ina sehemu iliyo wazi ya juu ili kuingiza mwangaza, lakini ina madirisha machache tu, kitu kingine ni kwamba, kila nyumba ina ukuta unaoitwa Ma Tou Qiang, ambao unasaidia kuzuia moto."

    Katika kijiji vya Hongcun, kuna nyumba zaidi ya 140 za enzi ya Ming na Qing kama Shu Ren Tang ambazo zimehifadhiwa vizuri, maziwa na milima vinatazamana na nyumba hizo za kale, mandhari za kimaumbile zinachanganyika na utamaduni wa kale. Milima, mifereji, makazi na binadamu wanaishi kwa masikilizano na kuchanganyika kuwa kitu kimoja, hali ambayo imekuwa moja ya miujizi katika mali za uridhi wa utamduni duniani.

    Mbali na majengo ya kale, wakazi wa huko pia wanafuata maadili ya kale. Msimamizi wa eneo la utalii la Hongcun Bw. Wang Guoping alisema,

    "kwa upande wa maadili, tulikuja hapa mwaka 1991, wakazi wa hapa wanatutendea sisi wote kwa ukarimu, bila kujali ni wasimamizi wa eneo hilo au watalii. Tunaweza kusema ukitembea na bakuli tu, utapewa chakula katika kila nyumba, kila familia kama ikiandaa vitoweo fulani, hakika itawaita majirani kula pamoja."

    Kama tukisema mfumo wa mifereji ni alama maalumu ya Hongcun, basi alama ya Xidi ni mnara wake wa kumbukumbu uliyoko mlangoni mwa kijiji hicho. Maafa ya kimaumbile yaliyotokea miaka mia kadhaa iliyopita hayajaangusha mnara huo, ila tu imeupatia sura ya kihistoria. Mwenyeji wa kijiji cha Xidi Liu Qiaofeng alisema:

    "mnara huo ni alama ya kijiji cha Xidi, mwenye mnara huo anaitwa Hu Wenguang, uchongaji wa mnara huo una undani wake, kwenye sehemu ya paa, kulichongwa kobe sita ambao wana kichwa cha dragon, na mkia wa samaki, nywele zake zilizotengenezwa kwa chuma zinaweza kuepusha radi. Maana ya kobe hao ni kuvitaka vizazi vijavyo vipate mafanikio makubwa katika masomo au kazi zao, kwa upande wa kushoto na kulia, kulichongwa picha za watu wenye busara na mashujaa wa vita, maana yake ni kuitakia nchi utulivu na amani."

    Kwa kupitia majengo hayo ya kale ya Xidi, si kama tu tunaweza kufahamu matumaini mema yaliyobeba, bali pia tunaweza kuelewa uundani wa utamaduni wa China. Kijijini Xidi tuligundua nyumba moja ambayo jiko lake lilijengwa nyuma kidogo ili kuacha nafasi kwa ajili ya barabara. Hali hiyo imeonesha maadili ya masikilizano ya wachina. Bi. Liu Qiaofeng alisema:

    "jiko hilo halikujengwa sambamba na nyumba, liko nyuma kidogo. Mwenye nyumba hiyo ana moyo mkubwa, mtizamo wa jamii yenye masikilizano, mbinu za kutafuta njia ya kati, na fikra za Confucious zote zimeonyeshwa kwenye jengo hilo."

    Majengo hayo ya kale ya kijiji cha Xidi yametuonesha ustadi wa juu wa ujenzi, jinsi wakazi wa kale walivyoishi, utamaduni wa kienyeji na matumaini ya wakazi kwa maisha bara, na pia yameonesha busara na maadili ya wakazi wa kale. Mwishoni utaweza kuhisi roho ya majengo hayo ya kale, yaani "masikilizano kati ya binadamu na maumbile".

    Bw. Yu Yahui ambaye kwa miaka mingi amefanya juhudi za kukarabati na kuhifadhi majengo ya kale katika wilaya ya Yi anaona kuwa:

    "wazo la kiini lililooneshwa katika majengo hayo ya hale ni masikilizano kati ya binadamu na maumbile, yaani uhusiano wa kusikilizana kati ya milima, mito na makazi ya binadamu, hali hiyo haipatikani katika sehemu nyingine."

    Mbali na majengo yanayoonekana, Xidi na Hongcun pia kuna kivutio kisichoonekana, yaani mila za kienyeji zilizoenziwa kwa karne kadhaa. Kijiji hicho cha kale kilipojulikana duniani, hakikuoneshi furaha ya kupewa sifa hiyo. Wakazi wa huko bado wanaendelea kudumisha amani na utulivu, wakifuata maadili ya kale na kuishi maisha yao kama kawaida.

    Wakati usiku unapoingia, kwenye vijiji hivyo utaweza kusikia sauti ya kuashiria wakati ambayo ni mila ya kijadi iliyoenziwa kwa karne kadhaa, utahisi kwamba kila kitu kiko mbali sana katika historia, lakini ulivyoona na ulivyosikia vyote ni vya kweli na halisi. Wanavijiji wanaamini kuwa, utamaduni wao utaenziwa kizazi baada ya kizazi kwa kupitia sauti hiyo nzito ya kuashiria wakati.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako