• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Biashara ya kuvuka mipaka katika mtandao wa internet yahimizwa nchini China

    (GMT+08:00) 2016-01-20 10:27:46


    Wakati biashara ya China na nje inakabiliwa na changamoto kubwa, biashara ya kuvuka mipaka katika mtandao wa internet imekuwa ajenda muhimu katika mkutano wa kwanza wa baraza la serikali la China mwaka huu. 

    Waziri mkuu wa China Li Keqiang Jumatano iliyopita aliitisha mkutano wa baraza la serikali la China ili kuchagua miji yenye mazingira mazuri ya kimsingi, inayofanya vizuri katika uagizaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi, na biashara kupitia mtandao wa internet. Hatua hiyo ina lengo la kuanzisha maeneo ya majaribio ya biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet, kuiga na kueneza sera na kanuni za usimamizi zinazofuatwa katika eneo la majaribio la biashara ya aina hiyo la Hangzhou, mji uliopo mashariki mwa China.

    Katika mkutano huo Bw. Li Keqiang alitangaza hatua za kuunga mkono biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet ikiwa ni pamoja na kuanzisha maeneo mapya ya majaribio, zinazoonesha ishara wazi ya kutumia mtindo mpya kuhimiza ongezeko la biashara ya China na nchi za nje, kuyasaidia makampuni madogo na yenye ukubwa wa kati kupunguza gharama na pia kuhimiza ujasiriamali na uvumbuzi. Hii ni mara ya nne kwa waziri mkuu wa China kuhimiza biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet katika mkutano wa baraza la serikali la China tangu mwaka 2015.

    Mwaka jana, serikali ya China ilitoa nyaraka tatu ndani ya mwezi mmoja kupanga kazi za kukuza biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet. Kazi hizo ni pamoja na kuongeza ufanisi wa kupita forodhani, kuhamasisha miamala ya fedha kupitia mitandao ya simu kwa kuvuka mipaka ya nchi, kuziunga mkono benki za China kupanua biashara zao nje ya nchi, na kusaidia makampuni ya kuendesha biashara kwenye mtandao wa internet kupata masoko yao nje ya nchi.

    Lakini ni kwa nini China imeanza kutilia mkazo biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet? Sababu ni kwamba hivi sasa biashara ya China na nchi za nje inakabiliwa na changamoto kubwa.

    Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa kwenye forodha, katika miezi kumi ya kwanza ya mwaka jana, biashara ya China na nje ilipungua kwa asilimia 8.8, ambapo uuzaji wa bidhaa nje ulipungua kwa asilimia 3 huku uagizaji bidhaa kutoka nje ukipungua kwa asilimia 15.1. Ni hakika kuwa kwa mwaka mzima uagizaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi vyote vilipungua.

    Kutokana na uchumi wa dunia kufufuka taratibu, kutokea tena kwa hali ya kujilinda kibiashara na mahitaji ya ndani kupungua, biashara ya China na nchi za nje itakabiliwa na changamoto zaidi mwaka 2016. Wakati huohuo, oda mpya kutoka nje zimekuwa chache kwa miezi 15 mfululizo hadi mwezi Disemba mwaka jana, na uuzaji bidhaa nje ya nchi utaendelea kukumbwa na shinikizo kubwa mwanzoni mwa mwaka huu.

    Kinachostahili kufuatiliwa ni kwamba, wakati biashara ya jadi ya China na nchi za nje inapungua, biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet inaongezeka nchini China. Takwimu rasmi zinaonesha kuwa kiwango cha ongezeko la biashara kuu za kuvuka mipaka katika mtandao wa internet ni asilimia 40 hivi kwa wastani kila mwaka, ambapo kiwango cha ongezeko la mauzo ya rejereja ya kuvuka mipaka ni asilimia 40 hadi 50 hivi. Mwaka jana, kampuni kubwa ya biashara kwenye mtandao wa internet nchini China Alibaba ilivunja rekodi yake yenyewe tena kwa mauzo katika Siku ya Makapera ya China, tukio kubwa zaidi la manunuzi kwenye mtandao wa internet duniani.

    Katika mazingira hayo, mkutano wa baraza la serikali la China uliainisha kuanzisha maeneo mapya ya majaribio ya biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet, kusaidia kufanya biashara ya aina hiyo kuwa sekta mpya inayokuza biashara ya kigeni, na kufanya biashara ya China na nje ikabiliane vizuri na changamoto mbalimbali.

    Aidha, kutokana na makampuni mengi madogo na yenye ukubwa wa kati kuendesha biashara zao kupitia mtandao wa internet, kuhimiza biashara ya kuvuka mipaka katika mtandao wa internet kunaweza kusaidia makampuni hayo kupunguza gharama zao na kuongeza ufanisi. Kazi hiyo pia ni moja kati ya kazi tano muhimu za uchumi nchini China kwa mwaka 2016.

    Lakini ili kufanya biashara ya kuvuka mipaka katika mtandao wa internet inufaike na sera hizo, serikali ya China pia inatakiwa kufanya mageuzi zaidi. Mkutano huo umetaka kujenga utaratibu wa aina sita, ikiwemo kubadilishana taarifa kati ya makampuni, mashirika ya fedha na idara za usimamizi, kazi ambayo inazitaka vyombo mbalimbali vya serikali kuvunja mtindo wa jadi wa "kumiliki taarifa kwa ubinafsi" na kutumia mtandao wa internet kuongeza uwezo na kiwango cha huduma za umma.

    Waziri mkuu Li Keqiang amewahi kutoa wito wa kutumia "Internet Plus" kuboresha huduma za umma. Inatarajiwa kuwa baada ya mtandao wa internet kutumiwa zaidi katika kazi za serikali, biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet itapata maendeleo makubwa, na kufaidisha biashara ya China na nje na makampuni madogo na yenye ukubwa wa kati.

    Naam, msikilizaji, na kufikia hapo ndipo tunapokamilisha kipindi cha uchumi na maendeleo kwa leo hii. Kumbuka tu kipindi hiki kinakujia kila Jumatano muda kama huu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Katika kipindi cha leo, tumezungumzia kuhusu jinsi China inavyohimiza biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao wa internet ili kushughulikia changamoto kubwa zinazoikabili biashara ya China na nje. Aliyekuletea kipindi hiki, ni Zhou You, asante na kwa heri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako