• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ndoto ya waridi ya kijiji cha kabila la Wali mkoani Hainan

    (GMT+08:00) 2016-01-21 10:28:17

    "Naona hapa pananivutia, mandhari ni nzuri sana."

    "Bustani kubwa ya maua ya waridi, harufu nzuri kweli, na hali ya hewa ni safi sana. Kweli ni nzuri sana. Hata bustani kubwa ya maua ya waridi haina maua mengi kama hapa, kweli inapendeza sana hata sitaki kuondoka."

    Sehemu hii inayopendeza na kuwavutia watalii wengi ni bustani ya kimataifa ya maua ya waridi iliyoko katika ghuba ya Yalong mjini Sanya mkoani Hainan. Watu wanapozungumzia ghuba ya Yalong mjini Sanya, kwanza huwa wanakumbuka hoteli mbalimbali za nyota tano, na vivutio maarufu vya utalii vyenye bahari ya buluu na anga ya buluu. Lakini hata mwaka 2009 kijiji cha Bohou cha sehemu ya Jiyang mjini Sanya, ambacho hakiko mbali na ghuba ya Yalong, kilikuwa ni kijiji cha kabila la Wali kilicho nyuma kimaendeleo. Kutokana na tatizo la maji ya baharini kujaa hadi kwenye maeneo ya nchi kavu, mashamba ya eneo hilo karibu yote yameathiriwa na chumvi na magadi na hayafai kulimwa. Kwa hiyo, vijana wa kijiji hicho wote walihama na kwenda kufanya vibarua nje eneo hilo, na wazee waliobaki kijijini wengi hawajui kuongea Kichina sanifu, wala hajui ufundi, hivyo mapato yao yanayotokana na kilimo cha mpunga hata yalikuwa chini ya Yuan elfu 16.6 tu kila hekta kwa mwaka. Lakini hali hiyo ilianza kubadilika kuanzia mwaka 2009, ua dogo la waridi lilibadili kabisa sura ya kijiji cha Bohou, na kubadili maisha ya watu wa huko.

    Waridi ni maua yanayoota katika ukanda wenye halijoto ya wastani, kwa hiyo ni adimu kuonekana katika mkoa wa Hainan wenye halijoto ya tropiki. Baada ya kufanya majaribio ya miaka mingi, hatimaye mwaka wa 2008, wataalam wa kilimo walifanikiwa kupanda ua la kwanza la waridi mjini Sanya, na kumaliza historia ya mkoa wa Hainan kutokuwa na maua ya waridi. Baada ya majaribio hayo kupata mafanikio, kwa upande mmoja walitaka kutafuta maeneo makubwa kwa ajili ya kupanda maua ya waridi, kwa upande mwingine, mashamba ya kijiji cha Bohou yalikuwa hayalimwi kutokana na kuwa na chumvi na magadi, kwa hiyo serikali ikaunganisha matakwa ya pande hizo mbili, na kuvipelekea viwanda katika kijiji cha Bohou, na kuanzisha bustani ya kimataifa ya maua ya waridi ya ghuba ya Yalong mwaka 2009. Kuanzia wakati ule, mashamba yenye chumvi na magadi yanapata uhai tena kutokana na upandaji wa maua ya waridi, na maisha ya wanakijiji wa kijiji cha Bohou pia yamebadilika kuwa ya kufurahia kutokana na maua ya waridi.

    Hekta 183.67 za mashamba yaliyoathiriwa na chumvi na magadi katika kijiji hicho zilikodiwa na kampuni kutoka kwa wanakijiji, na bei ya kodi ya kila hekta ni Yuan elfu 55. Wakati huohuo kampuni hiyo pia iliwaajiri wanakijiji kushughulikia upandaji wa maua ya waridi, usimamizi wa mashamba na kazi ya kuchuma maua. Kwa kufanya hivyo, wanakijiji sio tu waliweza kupata kodi ya mashamba, bali pia wanaweza kupata mshahara kutoka kwa kampuni. Wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 50 kijijini, hata kama hawajui kuongea Kichina sanifu, pia wanaweza kushughulikia kazi hizo. Bibi Su Pinglan ni mwanakijiji wa kijiji cha Bohou, na alianza kufanya kazi katika bustani ya maua ya waridi kuanzia mwaka 2010. Hivi sasa anafanya kazi vizuri siku hadi siku, na mshahara wake pia unapanda siku hadi siku. Alipozungumzia kazi hiyo alisema kwa furaha,

    "Umeona, nimefanya kazi hapa kwa muda mrefu, sasa kazi ni rahisi sana. Zamani nilikuwa nalima mpunga, kazi ilikuwa ni ngumu, sasa tunapanda maua. Tunachuma pesa nyingi, na mshahara pia unaweza kupanda, nafurahi kufanya kazi hapa."

    Kama alivyosema Bibi Su, mapato yao kutokana na kilimo cha maua ya waridi yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa, mapato ya wastani ya wanavijiji yamefikia Yuan elfu 70 kwa mwaka, ambayo ni ya kiwango cha juu katika vijiji vya kabila la Wali mjini Sanya.

    Mwaka 2012, baada ya kupanda maua ya waridi, bustani ya kimataifa ya maua ya waridi pia ilianzisha miradi mbalimbali ya kitalii kama vile utalii wa kutembelea bustani ya maua ya waridi, kuandaa harusi n.k. Wanavijiji wananunua hisa kwa dhamana ya ardhi zao, kwa hiyo kila mwaka wanapata faida nyingine ya Yuan zaidi ya elfu 13 kwa kila hekta kutokana na miradi hiyo ya kitalii. Wakati huohuo, kampuni pia inawasaidia wanavijiji kuendeleza hoteli za wanavijiji, mikahawa na maduka, ili wanavijiji waendeleze kwa pamoja uchumi wa utalii wa kilimo. Kijiji ambacho zamani kilikuwa nyuma kimaendeleo, sasa kimekuwa bustani kubwa ya waridi yenye milima ya kupendeza, maji ya kupendeza na maua yanayochanua kila mahali. Wanavijiji sio tu wanapata mapato mengi zaidi, bali mazingira yao ya kuishi pia yamebadilika kabisa. Mkurugenzi wa ofisi ya kampuni ya maendeleo ya bustani ya kimataifa ya maua ya waridi ya Lande ya Sanya Su Wenmao amesema,

    "Tumeingia katika kijiji cha Bohou kwa miaka 6, katika miaka hiyo 6, tumeona mabadiliko ya maisha ya wanakijiji. Tumeona mabadiliko makubwa katika barabara, mazingira ya kuishi, na hali yao ya ajira, na wamekuwa wachangamfu zaidi."

    Kijiji cha Bohou kinachobadilika kuwa kizuri si kama tu kinawavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali, bali pia vijana walioondoka kutoka kijiji hicho wanarudi. Kutokana na maendeleo ya shughuli za utalii, vijana hao wamepata nafasi nzuri za ajira. Bibi Liao Hongxia ni mwanakijiji wa kijiji hicho, pia ni mfanyakazi wa bustani ya maua ya waridi. Alijiuzulu kazi yake ya zamani katika kampuni moja, na kurudi maskani yake. Hivi sasa wanafamilia wake watatu wote wanafanya kazi katika bustani hiyo. Anaona kuwa wanaweza kuona kwa macho na kujisikia moyoni mabadiliko ya maisha yao. Anasema,

    "Maisha yetu yamebadilika sana, zamani familia yetu ilikuwa maskini, hivi sasa maisha yetu yanabadilika na kuwa nzuri zaidi."

    Mkurugenzi wa ofisi ya kampuni ya maendeleo ya bustani ya kimataifa ya maua ya waridi ya Lande ya Sanya Su Wenmao amesema, katika siku za usoni, kwenye msingi wa sasa wa bustani ya maua ya waridi, wanapanga kukifanya kijiji cha Bohou kiendelezwe kuwa mji mdogo wenye umaalum wa mtindo wa mapambo ya waridi, kikiwa sehemu ya mpango wa 13 wa maendeleo ya miaka mitano, mpango huo utazisaidia familia 765 zenye wanakijiji 2,544 wa kabila la Wali kuwa wakazi wa mijini bila ya kuhama. Bw. Su Wenmao anasema,

    "Katika siku zijazo, pia tunataka kukijenga kijiji hicho kiwe kijiji chenye shughuli maalum, na kukirekebisha kwa kuunganisha shughuli zetu za maua ya waridi. Tunataka kuwafanya watu wote waajiriwe na kila familia iwe na shughuli zake, huu ni mpango wetu katika siku za usoni."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako