• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maisha yetu ya "mikononi"

    (GMT+08:00) 2016-02-04 09:57:13

    Ni muda mfupi umepita tangu watu washerehekee sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya. Wachina wanaopenda kusherehekea sikukuu hizo, mbali na kununua vitu wanavyopenda na kula chakula kitamu, pia wana njia mpya ya kusherehekea sikukuu, yaani wanawatumia marafiki, jamaa au wapendanao bahasha nyekundu iliyowekwa pesa, lakini si ya karatasi kama zamani, bali ni ya kitarakimu kwa njia ya simu za mkononi kupitia APP ya mawasiliano Wechat.

    Bila kujali ni kiasi gani kimewekwa ndani ya bahasha nyekundu, watu wanafurahia njia hiyo tu. Kama una namba ya Wechat ya rafiki yako, basi kwa kutumia kidole chako unaweza kubonyeza na kutuma bahasha nyekundu, ni rahisi lakini inaweza kuwaletea furaha kubwa watu wa pande mbili. Dada Wang Jiao ni mfanyakazi wa ofisini aliyezaliwa baada ya mwaka 1985, alivyosherehekea sikukuu ya Krismasi iliyopita ndivyo kushindania bahati nasibu kupokea bahasha nyekundu iliyotolewa kwenye Wechat Group ambayo inatoa pesa kiasi tofauti kwa marafiki walioibonyeza, na pia kutuma bahasha nyekundu kwa marafiki. Kwa kweli, watu wanaosherehekea sikukuu kama dada Wang si wachache. Dada Wang anasema,

    "Ndiyo, katika sikukuu ya Krismasi nilipokea bahasha nyekundu, ambazo nyingi zilitumwa na viongozi wetu, mimi na wanafunzi wenzangu pia tulitumiana bahasha nyekundu, kwa ujumla nilipata Yuan 200 au 300 hivi. Pia nilituma bahasha nyekundu, kwa wanafunzi wenzangu, wazazi wangu na marafiki. Hali hii inanivutia, kinachokuvutia labda sio kiasi cha pesa unachopata, cha muhimu ni furaha unayopata wakati unapobonyeza na kufungua bahasha nyekundu uliyopokea."

    Bahasha nyekundu ya Wechat ni njia ya kulipia iliyotolewa na Wechat mwaka 2014. Takwimu zilizotolewa rasmi na kampuni ya Tencent inayotoa huduma ya Wechat zimeonesha kuwa, katika siku ile ya mkesha wa mwaka mpya wa jadi wa mwaka 2015, idadi ya utoaji na upokeaji wa bahasha nyekundu ya Wechat ilifikia mara bilioni 1.01, ambayo inamaanisha kuwa, kwa wastani karibu asilimia 70 ya Wachina walitumia njia hiyo ya bahasha nyekundu ya Wechat waliposherehekea mwaka mpya wa jadi. Lakini rekodi hii ilivunjwa haraka katika sikukuu nyingine. Tarehe 20 Agosti mwaka 2015, yaani siku ya Qixi ambayo ni sikukuu ya mapenzi ya jadi ya kichina, idadi ya utoaji na upokeaji wa bahasha nyekundu kwenye Wechat ilifikia mara bilioni 1.427.

    Wechat imeingia na kubadili maisha ya watu, na mabadiliko yametokea chini ya miaka mitano tu. Wechat ni APP ya bure inayotoa huduma za mawasiliano ya haraka, ambayo ilitolewa na kampuni ya Tencent mwezi Januari mwaka 2011. Katika miaka mitano iliyopita, Wechat imekuwa software ya mawasiliano ya haraka inayotumiwa na watu wengi zaidi wa sehemu ya Asia. Hadi kufikia robo ya kwanza ya mwaka jana, Wechat ilikuwa inatumika kwenye zaidi ya asilimia 90 za smartphone, na idadi ya watumiaji wake kwa mwezi imefikia milioni 549.

    Sababu ya Wechat kupendwa na watu ni matumizi yake rahisi na kuweza kutumika kwa mambo mengi. Mwanzoni ilikuwa kifaa cha mawasiliano tu, lakini kutokana na kuenea na kuboreshwa kwa mtandao wa simu za mkononi, Wechat inayotegemea mtandao wa internet si tatizo tena, ikaanza kutumiwa badala ya ujumbe mfupi, na kuwa moja ya njia za mawasiliano zinazotumiwa na Wachina mara kwa mara. Urahisi na bei nafuu ndiyo sababu muhimu ya watu kutumia Wechat.

    Bibi Liu Bing ni mwongozaji filamu, na kila siku anahitaji kuwasiliana na watu wengi. Anasema Wechat ikiwa kifaa cha mawasiliano, imeleta urahisi kwa kazi yake. Bibi Liu Bing anasema,  

    "ni rahisi sana kutumia Wechat kwa mawasiliano, tena inabana matumizi. Hasa sasa kuna mtandao wa 4G, hatuna wasiwasi kuhusu kasi ya mtandao, ama kutotuma au kutopokea ujumbe."

    Hivi leo nchini China, bila kujali kama ni wazee au vijana, watu wanaotumia smartphone karibu wote wanaweza kutumia Wechat. Kwa kuwa huduma zinazotolewa na Wechat zinakidhi mahitaji yao mbalimbali. Hasa Wechat inaweza kuandika ujumbe kwa kusikiliza sauti yako moja kwa moja bila haja ya kutumia keyboard, uwezo ambao ni rahisi kwa wazee kutumia hata kama hawajui kutumia keyboard.

    Shangazi Zhu ni profesa wa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing. Binti yake alihamia Canada katika miaka iliyopita, na kufunga ndoa na kuzaa watoto huko. Kwa hiyo Wechat imekuwa moja ya njia muhimu ya kuwasiliana nao. Hivi sasa shangazi Zhu hana haja kusubiri likizo kwenda Canada, bali akiwa hapa Beijing anaweza kuwasiliana na binti yake na kuwaona wajukuu wake wakati wowote. Kama kuna matatizo ya kuwasiliana kupitia video, pia anaweza kujua hali ya hivi karibuni ya familia ya binti yake kwa kupitia picha na maelezo anayoweka binti yake kwenye Wechat. Wakati huohuo, Wechat pia imekuwa chombo muhimu cha mawasiliano katika shughuli zake. Shangazi Zhu anasema,

    "Polepole ninatumia kwa mara nyingi huduma ya Walkie-Talkie ya Wechat, naona kwa wazee ni rahisi kutumia. Marafiki kwenye Wechat yangu karibu wote ni wenzangu na marafiki ambao vitu wanavyopenda vinafanana na ninavyopenda mimi. Pia kuna maprofesa wa vyuo vikuu vingine, tunaweka baadhi ya vitu vya kitaaluma katika Group yetu kwenye Wechat. Vilevile wanafunzi wangu pia wananitumia baadhi ya ujumbe na vitu vingine kupitia Wechat."

    Hata hivyo kama ilivyo kwa wazee wengine, Shangazi Zhu anatumia huduma ya kimsingi ya mawasiliano tu, hatumii huduma ya kulipia ya Wechat, kwa sababu bado anaona ni jambo la utatanishi tena ni la hatari kuweka fedha katika simu ya mkononi. Shangazi Zhu anasema,

    "Sijawahi kutumia, na sithubutu kutumia, tena sifahamu. Kwa sababu si rahisi kutumia, naogopa utatanishi, tena si salama."

    Kwa vijana wa kawaida, Wechat ina ushawishi mkubwa zaidi kwa maisha yao. Huduma ya kulipia ya Wechat inawawezesha wasafiri, kufanya manunuzi na kula chakula bila ya kuwa na fedha taslimu. Hivi sasa hata wanaweza kutumia Wechat kulipa huduma mbalimbali, kuuliza habari kuhusu bima za jamii, usafiri wa barabarani n.k. Tunaweza kusema software ndogo imesaidia kuboresha maisha yetu kwa pande zote, na kuleta urahisi kwa maisha yetu. Lakini pia ina matatizo yake. Ingawa huduma ya kuwasiliana na marafiki ya Wechat inaweza kuwafanya marafiki wa zamani wawasiliane tena, na gharama hiyo ndogo inatoa urahisi kwa watu wa sasa ambao hawana muda mwingi kufanya mawasiliano ya kijamii, lakini pia inaleta matatizo kadhaa madogo: inachukua muda wa watu wa kusoma vitabu na magazeti, na kuangalia picha na matukio ya marafiki yanayowekwa kwenye Wechat kumekuwa njia ya kwanza ya kupata habari. Kutoa maoni na kubonyeza "like" kumekuwa njia ya kudumisha uhusiano, jambo ambalo pia linawafanya baadhi ya watu wasumbuliwe. Bibi Liu Bing pia anatumia Wechat kuwasiliana na marafiki zake, lakini anazuia huduma ya kuonesha matukio ya marafiki kwenye Wechat. Anasema,

    "Mimi situmii huduma ya matukio ya marafiki kwenye Wechat, mwanzoni nilitumia huduma hiyo, lakini nilizima baada ya kuitumia kwa miezi miwili mitatu. Sababu ni kwamba nagundua muda wangu 'unatekwa nyara' na huduma hiyo. Kila asubuhi nilikuwa naangalia matukio ya marafiki, naangalia watu wangapi wanabonyeza like, na nitabonyeza like kwa watu wangapi. Polepole naona inapoteza wakati. Kama nataka kumfahamu mtu mmoja, napenda zaidi kuongea naye ana kwa ana."

    Sayansi na teknolojia zinapotuletea urahisi, pia zinabadili maisha yetu, njia zetu za matumizi na mawasiliano ya kijamii. Katika siku za usoni, ushawishi wake utazidi kuwa dhahiri. Maisha yetu yataathiriwa na simu za mkononi na mtandao wa internet, na huu ni mwelekeo ambao hauwezi kubadilika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako