• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bibi Zhang Rong na kahawa anayopenda

    (GMT+08:00) 2016-03-31 09:57:57

    Miaka 10 iliyopita, Bibi Zhang Rong, msichana aliyezaliwa baada ya mwaka 1980 alikuwa chuoni akisomea kozi ya biashara ya kimataifa. Wakati huo alianza kuipenda kahawa. Kwa sasa anatembelea tovuti mbalimbali za kahawa za nchini na za nchi za nje, na kubadilishana maoni kuhusu kahawa na washabiki wa kahawa kwenye mtandao wa Internet. Baada ya kuhitimu chuo kikuu, bibi Zhang Rong kwa nyakati tofauti alikwenda Shanghai na Beijing kujihusisha na kazi za kutengeneza kahawa na kutoa mafunzo kuhusu kahawa, na tabia yake ya kupenda kukaanga mbegu za kahawa mwenyewe nyumbani ikakuwa kazi yake rasmi, yaani mtengenezaji wa kahawa. Bibi Zhang Rong ana maoni yafuatayo kuhusu kazi zake,

    "Kwenye sekta ya kahawa, naona nafasi muhimu zaidi ni mtengenezaji wa mbegu za kahawa. Kwa kuwa napenda kazi hii, napenda watu wengine pia waielewe. Nakwenda kutafuta mbegu za kahawa kwenye sehemu mbalimbali kwa sababu napenda kukaanga kahawa, kwa hiyo nafanya kazi hii kuwa ni chaguo la lazima kwangu."

    Hatua ya kukaangwa kwa kahawa ndio unaamua uzuri wa kahawa yenyewe, na hii ni kazi yenye changamoto kubwa. Lakini kwa bibi Zhang Rong, hii ndio kazi anayoipenda zaidi, yaani kukidhi mahitaji wateja mbalimbali kupitia njia mbalimbali za kukaanga kahawa. Bibi Zhang anasema,

    "Utagundua kuwa kazi ya kukaanga kahawa ina utatanishi zaidi kuliko kazi ya kutengeneza kahawa yenyewe, kwa hiyo kazi hiyo inavutia zaidi, na ina changamoto zake. Kama utengenezaji kahawa ni kuonesha matunda yaliyopatikana, basi kukaanga kahawa ni uvumbuzi wa kahawa yenyewe. Kama ukikaanga kahawa kwa kiasi kidogo, basi itakuwa na ladha ya matunda, ukikaanga kwa kiasi cha kati basi zitakuwa na ladha ya karanga, kwa kiasi kikubwa basi zitakuwa na umaalumu wa chocolate. Katika mchakato huo, unahitaji kuchagua au kuvumbua ni ladha gani unayoitaka."

    Uzoefu wa miaka mingi wa kushughulikia kazi zinazohusiana na kahawa umemfanya bibi Zhang Rong atambuliwe katika sekta hiyo, na mawasiliano ya mara kwa mara na makampuni maarufu ya kahawa ya nchi za nje na wataalam wa kahawa wakati alipofanya kazi mjini Beijing, pia yamempa habari nyingi za kisasa. Mwaka 2011 kwa bahati bibi Zhang Rong aligundua kuwa, kiwango cha upokeaji na ujuzi wa watu wa mji wa Qingdao kuhusu kahawa ni sawa na wale wa miji mikubwa ya Beijing na Shanghai, kwa hiyo akaamua kubaki Qingdao kuanzisha shughuli zake, na kufungua mgahawa wa Fisher Coffee.

    Tofauti na mbegu za kahawa zinazoweza kununuliwa supamaketi, Fisher Coffee ilipoanzishwa ilifanya juhudi kutoa kahawa bora inayoweza kukidhi mahitaji mbalimbali ya wateja. Hata hivyo ingawa ana uzoefu mkubwa na raslimali nyingi, mwanzoni alipofungua mgahawa wake, bibi Zhang Rong anakabiliwa na changamoto mbalimbali. Kwa hiyo anataka kuleta mabadiliko kwenye sekta ya kahawa, Bibi Zhang anasema,

    "Katika miaka miwili iliyoopita, sekta ya kahawa yameendelezwa kwa haraka hapa China, lakini kabla ya hapo mazingira yetu ya kuanzisha shughuli zetu hayakuwa mazuri. Tunaweza kuona katika sekta ya kahawa, bado kuna sehemu nyingi ambazo hazijapevuka kuliko sekta nyingine, hivyo tunajaribu kubadili hali hiyo, kufanya uvumbuzi na kujitahidi kutoa mchango kwa sekta hiyo ya kahawa."

    Tangu mgahawa wa Fisher Coffee uanzishwe hadi sasa, umepiga hatua kubwa kwa haraka kwa kutumia jukwaa la uuzaji lenye ufanisi kupitia mtandao wa internet na bidhaa bora za kahawa zilizochaguliwa kwa makini. Mwaka 2015 mgahawa wa Fisher Coffee uliuza tani 60 za kahawa, na kuwapatia wateja aina zaidi ya 100 za mbegu za kahawa; wakati huohuo, kundi la ujasiriamali la bibi Zhang Rong pia linaimarishwa, na idadi ya wafanyakazi wake imeongezeka kutoka saba hadi 21. Bibi Zhang anasema,

    "Hivi sasa tuna maendeleo ya kasi, na hii inatokana na mazingira mazuri ya nchi yetu, na maendeleo ya biashara kwenye mtandao wa internet, sababu nyingine ni kwamba tunachagua bidhaa nzuri yaani kahawa bora, tunafanya jambo sahihi kwa wakati sahihi."

    Bibi Zhang Rong bado anakumbuka alipokunywa Yirgacheffe, mbegu za kahawa zinazozalishwa barani Afrika. Wakati ule alifikiri kuwa, siku moja ni lazima aende sehemu wanakolima kahawa barani Afrika, na kuchukua mwenyewe mbegu mpya za kahawa zenye rangi ya kijani nyeusi kutoka banda la kukausha kahawa, kukaanga na kuonja. Mwaka huu kutokana na mwaliko wa shirikisho la kahawa la Afrika, bibi Zhang Rong alikwenda Nairobi na Addis Ababa kuwa jaji wa kimataifa wa shindano la kuonja kahawa. Katika kipindi hicho, alitumia siku 15 kutembelea sehemu nyingi zinazozalisha kahawa, na kuhisi kwa karibu namna ya watu wa huko wanavyoonja kahawa.

    Wakati alipoanzisha biashara yake, bibi Zhang Rong alikuwa na matarajio makubwa juu ya sehemu zinazozalisha kahawa nchini China, lakini tatizo ni kuwa kama ikipimwa kwa vigezo makini, bado kuna pengo kati ya kahawa ya China na ya nchi za nje. Mwaka 2012 bibi Zhang Rong na kundi lake waliamua kwenda sehemu zinazozalisha mbegu za kahawa mkoani Yunnan, na kushirikiana na mkulima wa kahawa wa huko katika hatua mbalimbali za upandaji, uchaguzi na utengenezaji wa mwanzo. Bibi Zhang anasema,

    "Kabla ya hapo kila mwaka au kila baada ya miaka miwili tulikuwa tunakwenda mkoani Yunnan, lakini mbegu za kahawa tulizopata hazikuwa nzuri kama tulivyotarajia, au hazikufikia matarajio yetu kuhusu kahawa bora. Tukiwa wataalam wa sekta hiyo, tulijua kuwa hakika kuna dosari katika teknolojia, kwa hiyo tulianza kutoka jambo dogo, kwa mfano tunatafuta wakulima wenye ujuzi zaidi kuhusu kahawa bora, na kuwaelekeza kupanda na kutengeneza kahawa nzuri kila mwaka, tuliwahimiza hatua kwa hatua. Mwaka huu kikundi cha kwanza cha mbegu za kahawa kimefika, na kiwango chake ni kizuri sana."

    Huu ni mwaka wa 10 tangu bibi Zhang Rong aifahamu kahawa. Katika kipindi hicho ametimiza ndoto ya kila mtengenezaji kahawa, yaani kuzindua mgahawa wa kahawa, mgahawa wa kahawa mwenye hadithi. Anaona kuwa, huu ni mwanzo mwingine wa ujasiriamali. Miaka 10 ya kwanza itamalizika, lakini bado kuna miaka 10 mingine ijayo. Bibi Zhang Rong anasema anataka kuanzisha chapa maarufu ya kahawa bora ya China, ili wote wanaopenda kahawa waweze kunywa kahawa nzuri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako