• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Busara za Confucious zatumika kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya waondokane na tabia hiyo

    (GMT+08:00) 2016-04-14 18:36:32

    Hivi karibuni mkoa wa Shandong ulioko mashariki mwa China, ulianzisha taasisi ya Confucious kwenye kituo cha kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya kuondokana na tabia hiyo cha Jidong huko Jinan, mji mkuu wa mkoa huo, hatua ambayo ilizusha mjadala mkubwa kwenye jamii kuhusu jinsi falsafa ya kale ya kichina inavyoweza kusaidia kutatua tatizo la sasa la matumizi ya dawa za kulevya.

    Falsafa ya Confucious inatetea mahusiano ya kifamilia, wajibu wa kuwatunza wazee na maadili ya kuheshimiana, ambavyo mamlaka mkoani Shandong zinaamini kwamba vitatoa ushawishi wa kimaadili kwa wale wanaopewa matibabu ya kuwasaidia kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya.

    Katibu mkuu wa Shirikisho la Confucious la China CCF Wang Daqian ambaye pia ni mmoja wa waanzilishi wa taasisi hiyo, amesema busara za Confucious zitaongeza imani ya watumiaji wa dawa za kulevya ya kuondokana na tabia hiyo, na pia zitawasaidia kurekebisha ulimwengu wao wa kiroho.

    Mamlaka mkoani Shandong zinatumai kuwa falsafa hiyo ya kale itabadilisha mawazo yasiyo sahihi na vitendo visivyofaa vya watumiaji wa dawa za kulevya, ili wawaze kuondokana kabisa na tabia hiyo na kurejea kwenye jamii.

    Hii ni njia mpya iliyovumbuliwa na mamlaka mkoani Shandong ili kuwasaidia watu walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Mkoa huo ambao ni chimbuko la Confucious, mpaka sasa umejenga taasisi nane za Confucious kwenye vituo vya kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya, na taasisi ya kwanza ilianzishwa mwaka jana mjini Jining.

    Kwenye maktaba ya taasisi hiyo mwandishi wetu wa habari aliwaona watumiaji wa dawa za kulevya wakisoma vitabu, na picha kubwa ya Confucious imebandikwa kwenye ukuta, kando ya picha hiyo kuna maandiko yanayotetea tabia nzuri, upendo, heshima, uangalifu na unyenyekevu.

    Mmoja wa watumiaji wa dawa za kulevya wanaopewa mafunzo kwenye taasisi hiyo alimwambia mwandishi wetu kwamba, mbali na kusoma vitabu, pia wanafundishwa sanaa ya maandishi ya kichina. Amesema, kama mtu akijifunza mambo mengi zaidi, ataelewa kwa kina zaidi hisia ya utulivu.

    Naibu mkurugenzi wa kituo hicho Bw. Cui Dongzheng amesema, Sanaa ya maandishi, inayohitaji umakini mkubwa, itasaidia kusafisha roho ya waathiriwa wa dawa za kulevya.

    Kwenye taasisi nyingine ya Confucious katika kituo cha kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya cha Jining, kuna madarasa, maktaba na kituo cha sanaa ya maandishi. Mbali na elimu ya kawaida, kituo hicho pia kinaingiza utamaduni wa Confucious kwenye mafunzo ili kugusa roho za waathirwa.

    Kijana Zhang mwenye umri wa miaka 24 ni mmoja wa waathirika wa dawa za kulevya wanaopewa msaada kwenye kituo hicho. Amesema, hajawahi kusoma kitabu hata kimoja baada ya kuhitimu kutoka shuleni. Alimwambia mwandishi wetu kwamba zamani aliona si jambo kubwa kutumia dawa za kulevya, lakini sasa amefahamu madhara yake na ana imani kuwa ataondokana na matumizi ya dawa hizo.

    Naye mkurugenzi wa kituo hicho Sui Shanjian amesema, ni rahisi kwa watumiaji wa dawa za kulevya kuondokana na tabia hiyo kivitendo, lakini ni vigumu kwao kuachana nayo kisaikolojia. Amesema, ni jambo la kawaida kuona watumiaji wa dawa za kulevya wakirejea tabia hiyo baada ya kuondoka kwenye kituo cha msaada.

    Sui amesisitiza kuwa, ingawa hilo linatokea, falsafa ya Confucious, inayotetea kujitafakari na kuwajibika, inasaidia kwa ufanisi kujenga utaratibu wa motisha ambao utawasaidia waathirika wa dawa za kulevya wajizuie na kuepuka kwa hiari kuzitumia tena dawa hizo.

    Shughuli mbalimbali zikiwemo mashindano ya sanaa ya maandishi na mihadhara ya utamaduni, zimefanyika kwenye kituo hicho, ambazo zimeimarisha imani ya waathirika wa dawa za kulevya ya kuondokana kabisa na dawa hizo.

    Kutokana na msaada wa elimu ya Confucious, waathirika wengi wa dawa za kulevya wamejiamini zaidi, wamekuwa wapole zaidi wanapozungumza na familia zao, na pia wamepunguza vitendo vya kimabavu.

    Ofisa mmoja wa mamlaka mkoani Shandong amesema, baadhi ya waathirika wa dawa za kulevya walikuwa na uzito wa kilogramu 45 tu walipopelekwa kwenye vituo hivyo, lakini baada ya kupewa elimu hiyo kwa miezi miwili au mitatu tu, wengi wao wameongeza uzito.

    Naye naibu mkuu wa Idara ya sheria ya mkoa wa Shandong Qi Yan'an amesema, China inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupamabana na matumizi ya dawa za kulevya, ambapo idadi ya watumiaji wa dawa hizo walioandikishwa imefikia milioni 3 kote nchini.

    Katibu mkuu wa Shirikisho la Confucious la China CCF Wang Daqian amesema, ukosefu wa upendo na moyo wa kuwajibika ni matatizo yaliyopo nyuma ya kila mtumiaji wa dawa za kulevya. Ameongeza kuwa, kuna usemo wa kichina usemao " ni rahisi kukamata wezi milimani, lakini ni vigumu kukamata wezi mioyoni." Anatumai kuwa waathirika wa dawa za kulevya wanaweza kujifunza kwa makini utamaduni wa jadi wa kichina, ili wawe na maadili bora na kuwa watu wema na wapole kwa familia zao, na pia kwa jamii katika siku za baadaye.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako