• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wadau wa sekta mbalimbali wana matarajio ya kuchaguliwa kwa katibu mkuu mwanamke kwa kwanza wa Umoja wa Mataifa

    (GMT+08:00) 2016-04-19 06:33:16

    Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita lilianza mchujo wa siku tatu wa wagombea wanane wa nafasi ya katibu mkuu wa Umoja huo. Wakati vyombo vingi vya habari vinafuatilia jukwaa hili lililotolewa kwa mara ya kwanza katika historia ya Umoja huo kwa wagombea wa nafasi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kujieleza, wadau wa sekta mbalimbali wanajadili tena ni sifa gani ambazo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anapaswa kuwa nazo na anatakiwa kubeba wajibu gani. Mjumbe wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Bw. Matthew Rycroft anasema, katibu mkuu wa Umoja huo ana wajibu mkubwa.

    "Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa sio cheo cha kawaida. Tuna matumaini kuwa yeye atafanana na kiongozi wa kijeshi, wala sio katibu. Vilevile tuna matumaini kuwa mchakato wa kuteua katibu mkuu ajaye utakuwa wa uwazi, ili kurahisisha kumpata mgombea anayefaa."

    Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Bw. Mogens Lykketoft anaona kuwa, majadiliano kati ya katibu na mkurugenzi yalirahisishwa kupita kiasi, katibu mkuu ajaye wa Umoja huo anatakiwa kuwa na vigezo vya hao wote wawili.

    "Ili kumteua mgombea mzuri zaidi, tunatakiwa kuwafahamu zaidi, hii ndiyo sababu tunaandaa mazungumzo yasiyo rasmi. Mgombea huyo anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kimaadili kwa jumuiya ya kimataifa, ambaye ana uhodari wa diplomasia ya kisiasa, na pia anaweza kuongoza Umoja wa Mataifa kupata maendeleo kwa wakati."

    Swali waliloulizwa wagombea na Kundi la Marafiki wanaounga mkono Mwanamke kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa lilikuwa hilo, ukichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ni hatua gani ungependa kuchukua ili kuboresha usawa wa kijinsia ndani ya ngazi ya juu ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa? Akijibu swali hilo, mmoja wa wagombea Danilo Turk, rais wa zamani wa Slovenia, alisema anaamini kwamba jambo la msingi ni kuwa na uwakishi wa 50-50 wa idadi ya wanaume kwa wanawake.

    Maswali mengine juu ya suala hilo kama vile jinsi ya kushirikisha wanawake katika upatanishaji kama vile katika mazungumzo ya amani pia yamekuwa katika mijadala kwa siku mbili.

    Vesna Pusic, mgombea wa kike na waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Croatia, alisema ni muhimu sana kutafuta watu wenye "ubora wa juu" ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, na kama Umoja huo unatafuta wanawake wa "daraja la kwanza", "kutakuwa na zaidi ya asilimia 50. "

    Katika historia miaka 70 ya Umoja wa Mataifa, kumekuwa na makatibu wakuu wanane wa kiume, na hakuna mwanamke aliyewahi kushika wadhifa huo. Kuhusu kuwa na katibu mkuu mwanamke, Rais wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft na balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power walisema kwenye barua ya pamoja, kuwa "nchi wanachama zinahimizwa kuwasilisha wanawake, na wanaume, kama wagombea wa nafasi hiyo."

    Mgombea mwingine mwanamke Natalia Gherman, mwanasiasa kutoka Moldova, amesema wanawake wanapaswa kupewa fursa ya kutoa mchango wao kwenye Umoja wa Mataifa; na kama atachaguliwa kuwa mkuu wa Umoja huo, atatoa kipaumbele kuwapa nafasi muhimu wanawake ndani ya mfumo wa Umoaj huo.

    Bw. Lykketoft na Bw. Ban Ki-moon wote waliwahi kutoa wito kuwa, ni lazima kutoa kipaumbele kumteua katibu mkuu mwanamke, na wanatarajia katibu mkuu mwanamke ataweza kutekeleza wajibu wake kwa kutumia kikamilifu umaalum wa wakina mama. Mwangalizi wa masuala ya Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Mji wa New York na Chuo Kikuu cha Colombia Bibi Jean Krasno anakubaliana na wito huo.

    "Ukiangalia duniani utagundua kuwa, bila kujali ni migogoro inayotokea barani Afrika ama wimbi la wakimbizi huko Mashariki ya Kati, wanaoathirika zaidi ni wanawake. Ili sauti zao zisikike, hakuna njia bora zaidi kuliko kumfanya mwanamke mmoja kushika madaraka ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa."

    Kuboresha usawa wa kijinsia imekuwa moja ya mambo muhimu kuwahi kutahiniwa kati ya wagombea wa uongozi wa Umoja huo baada ya Katibu Mkuu wa sasa Ban Ki-moon atakapokamilisha muda wake wa kuhudumu mwishoni mwa mwaka huu.

    Irina Bokova, ambaye anachukuliwa kuwa mgombea mwenye nguvu zaidi wa kike alisisitiza kwamba ni vigumu kufikia amani au maendeleo endelevu bila ya usawa wa kijinsia. Alisema anadhani kwamba karne ya 21 inafaa kuwa karne ya ahadi ya kweli kwa usawa wa jinsia na kuwapa wanawake nafasi ya kujiendeleza bila kubaguliwa katika jamii.

    Miongoni mwa wagombea tisa waliotangaza kuwania nafasi hiyo hadi sasa, wanne kati yao ni wanawake. Mbali na watau waliotajwa awali, Msimamizi wa UNDP Helen Clark, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa New Zealand anasema, wakati wa mwanamke kuteuliwa kuwa katibu mkuu umefika, lakini anaongeza kuwa bila kufikiria sula la jinsia, jambop muhimu ni kuzingatia kama mgombea ana uwezo wa kutosha kushika wadhifa huo au la.

    "Anglia picha za waliokuwa makatibu wakuu kwenye jengo la Umoja wa Mataifa, hamna mwanamke hata mmoja. Hivyo tuseme sasa ni wakati mwafaka kwa mwanamke kushika madaraka hayo? Jibu ni ndiyo, lakini muhimu zaidi ni kwamba mgombea huyo anapaswa kuwa na uwezo wa kutosha."

    Tangu Umoja wa Mataifa uanze kutoa maombi kwa wagombea na kuweka mchakato wa kuchagua katibu mkuu ajaye wa Umoja huo, kumekuwa na wito kutoka vyama vya kiraia na baadhi ya nchi wanachama wa Umoja huo kuchagua mwanamke kuwa katibu.

    Wachambuzi wanaona, ingawa mazungumzo mapya mwaka huu yameletea mabadiliko kwa uchaguzi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, na wadau wa sekta mbalimbali wana matarajio ya kumteua katibu mkuu mwanamke, lakini mambo mawili hayatabadilika, yaani Baraza la Usalama litafanya uamuzi na mgombea mwenye uwezo mkubwa zaidi atashinda.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako