• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • IMF yatahadharisha kuwa huenda uchumi wa dunia hautakua kwa muda mrefu

    (GMT+08:00) 2016-04-20 14:48:50


    Hivi karibuni, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF limetoa ripoti kuhusu mustakbali wa uchumi wa dunia, likishusha makadirio yake ya ukuaji wa uchumi wa dunia yaliyotolewa mwezi Januari hadi asilimia 3.2 kwa mwaka huu na asilimia 3.5 kwa mwaka kesho, na kutahadharisha kuwa uchumi wa dunia unakabiliwa na hatari ya kutoongezeka.

    Wakati huohuo, IMF imepandisha makadirio kuhusu ukuaji wa uchumi wa China kwa mwaka huu na mwaka kesho hadi asilimia 6.5 na asilimia 6.2. Baada ya mashirika maarufu ya Marekani ya kutathmini uwezo wa nchi kuhimili madeni ya Moody's na Standard & Poor's kushusha ngazi ya China kwenye tathmini zao, ripoti hiyo mpya iliyotolewa na IMF itaongeza imani ya watu na mustakbali wa ukuaji wa uchumi wa China. Mchumi mkuu wa IMF Maurice Obstfeld anasema,

    "Uchumi wa dunia unaendelea kufufuka, lakini kasi yake ya polepole inasikitisha watu na pia kusababisha ukuaji wa uchumi wa dunia kukabiliwa na hatari nyingi zaidi. Ukuaji taratibu wa uchumi wa dunia umedumu kwa muda mrefu sana. Kwa mujibu wa makadirio mapya kuhusu mustakbali wa uchumi wa dunia, ikilinganishwa na hali ya mwaka 2015, ongezeko la uchumi wa dunia kwa mwaka huu litakuwa ni asilimia 3.2 tu, na mwakani litafikia asilimia 3.5."

    Obstfeld amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne iliyopita huko Washington, ambapo ripoti kuhusu mustakbali wa uchumi wa dunia ilitolewa. Kwenye hotuba yake, Obstfel alitoa tahadhari kuhusu ufufuaji taratibu na udhaifu wa uchumi wa dunia na kusema kupungua kwa ongezeko la uchumi wa dunia kunaweza kupunguza thamani ya sarafu duniani, kuchochea utaifa na kusababisha migogoro ya siasa za kijiografia.

    IMF huwa inafanya mkutano na waandishi wa habari mara mbili katika nusu ya kwanza na ya pili ya mwaka, kando ya mkutano wa majira ya kuchipua na ule wa majira ya kupukutika ili kutangaza ripoti kuhusu mustakbali wa uchumi wa dunia, na pia kurekebisha ripoti hiyo katikati ya mwaka huo na mwanzoni mwa mwaka unaofuata.

    Ripoti hiyo inayoitwa "polepole na muda mrefu", imeonesha wazi kuwa uchumi wa dunia umeongezeka taratibu kwa muda mrefu. Ukuaji wa aina hiyo una athari mbaya, kupunguza uwezo wa uzalishaji, hivyo kuathiri matumizi na uwekezaji. Kutokana na hilo, IMF imetoa wito kwa nchi mbalimbali kuchukua hatua kuchochea uchumi kama vile kuhimiza mageuzi ya kimuundo, kutoa sera za uchochezi wa kifedha na kuongeza utoaji wa sarafu sokoni.

    Wakati huohuo, ripoti hiyo kuhusu mustakbali wa uchumi wa dunia imepandisha makadirio kuhusu ongezeko la uchumi wa China hadi asilimia 6.5 kwa mwaka huu na asilimia 6.2 mwakani. Lakini kabla ya hapo, mashirika ya kutathmini uwezo wa nchi kuhimili madini ya Moody's na Standard & Poor's ya Marekani yalishusha ngazi ya China kwenye tathmini zao kutoka tulivu hadi hasi. Obstfel anasema,

    "Kupandisha makadirio kuhusu ukuaji wa uchumi wa China kunaonesha imani kwa hatua na sera nyumbufu zilizotangazwa na serikali ya China zinazolenga kukuza uchumi wake, na inaaminika kuwa uchumi wa China kwa mwaka huu unaweza kuongezeka kwa asilimia 6.5."

    Ripoti hiyo inaona kuwa, China inashuhudia mchakato wa mageuzi ulio muhimu lakini wenye utata, na inatarajia kutafuta maendeleo endelevu ya uchumi yanayopatikana kwa matumizi na huduma. Mwishoni, mchakato huo utainufaisha China pamoja na dunia nzima.

    IMF pia imesema uchumi wa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara unakadiriwa kukua kwa asilima 3 kwa mwaka huu, kiasi ambacho kinapungua kutoka asilimia 3.4 ya mwaka jana na asilimia 5.1 ya mwaka juzi. Nchi mbili za Nigeria na Afrika Kusini zinazoongoza kiuchumi katika kanda ya Afrika kusini mwa Sahara ambazo zimechangia nusu ya pato la kanda hiyo, zilionekana kuathiri ongezeko la kikanda mwaka jana.

    Kwa mujibu wa data za IMF, ukuaji wa Nigeria, nchi inayouza nje mafuta kwa wingi zaidi katika kanda hiyo, ulipungua hadi asilimia 2.7 mwaka jana kutoka asilimia 6.3 ya mwaka 2014, huku Afrika Kusini, nchi inayouza nje madini kwa wingi zaidi katika kanda hiyo ikishuhudia ongezeko la asilimia 1.3 mwaka jana kutoka asilimia 1.5 ya mwaka juzi.

    Ripoti hiyo imeongeza kuwa msukosuko wa wakimbizi wa Syria, wasiwasi na ugaidi, upigaji kura za maoni utakaofanyika mwezi Juni ili kuamua kama Uingereza itajitoa kwenye Umoja wa Ulaya, vizuizi vya ukuaji vya masoko mapya yaliyoibuka, kupungua kwa nguvu za ongezeko la makundi ya kiuchumi yaliyoendelea, kuyumbayumba kwa bei za bidhaa zinazoagizwa kwa wingi, na mvua kali za El Nino, vyote vitaongeza hali ya kutokuwa na utulivu kwa ufufukaji wa uchumi wa dunia. Kama matokeo ya kura za maoni yataifanya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya, hili litakuwa ni piga kubwa kwa uchumi wa dunia ambao tayari umekuwa dhaifu. Shirika la habari la Uingereza Reuters linaona kuwa hili ni onyo kali zaidi lililotolewa na shirika la kimataifa kuhusu hatari ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.

    Bw. Obstfel amesisitiza kuwa hivi sasa ufufukaji wa uchumi wa dunia ni dhaifu na kuna uwezekano wa kupungua, hivyo ni lazima kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto hizo.

    "Narudia kwa mara nyingine tena kuwa ufufukaji wa polepole wa uchumi umewafanya watunga sera wasiwe na nafasi nyingi za kufanya makosa, na kama watunga sera wa nchi mbalimbali wakitambua ipasavyo hatari zinazowakabili kwa pamoja na kuchukua hatua zenye uratibu, itaweza kuongeza imani ya watu, kuhimiza ukuaji na kulinda vizuri mchakato wa kufufuka kwa uchumi wa dunia."

    Naam, msikilizaji na kufikia hapo ndipo tunapokamilisha kipindi hiki cha uchumi na maendeleo kwa leo hii. Kumbuka tu kipindi hiki kinakujia kila Jumatano wakati kama huo katika Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Katika kipindi cha leo, tumezungumzia ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kuhusu makadirio ya uchumi wa dunia, ambayo inatahadharisha kuwa uchumi wa dunia unakabiliwa na hatari ya kutoongezeka kwa muda mrefu. Aliyekuletea kipindi hiki ni Zhou You, asante na kwa heri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako