• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Makampuni madogo ya China yatafuta njia za kutatua tatizo la kukusanya fedha ili kuendesha shughuli zao

    (GMT+08:00) 2016-04-27 10:16:04


    Takwimu zinaonesha kuwa nchini China, makampuni madogo yamechukua asilimia zaidi ya 70 ya makampuni yote, na yametoa mchango muhimu katika kuhimiza ubunifu wa teknolojia na kutoa nafasi za ajira. Hata hivyo, katika mfumo wa uchumi wa China, makampuni madogo bado ni kundi dhaifu, na ugumu wa kukusanya fedha ni sababu moja muhimu ya kukwamisha maendeleo yake. Jinsi ya kutatua tatizo hilo ni suala lililoanza kufuatiliwa katika miaka ya hivi karibuni.

    "NXL" ni program inayotoa huduma za ushauri wa kisaikolojia katika simu. Mwanzilishi wake Jin Di ni mshauri wa saikolojia, ana kituo chake binafsi cha ushauri wa kisaikolojia. Hata hivyo, baada ya kujihusisha kwenye sekta ya ushauri wa kisaikolojia kwa miaka mingi, Jin Di amegundua mapungufu ya mtindo huo wa kijadi. Anasema,

    "Kutokana na maendeleo ya uchumi wa China, shinikizo la watu wengi kazini ni kubwa, na mahitaji ya ushauri wa kisikolojia ni makubwa. Lakini tumegundua kuwa watu wanaokuja kupata huduma hiyo katika kituo chetu sio wengi. Sababu kadhaa zinawazuia kuja, moja ambayo ni muhimu ni siri zao, pili ni gharama kubwa ya huduma ya ushauri wa kisaikolojia inayotolewa uso kwa uso. Tatu ni umbali, kwani nchi yetu ni kubwa, na maeneo mengi hayana taaluma za saikolojia."

    Kutokana na sababu hizo, Jin Di mwenye uzoefu wa kazi katika sekta ya teknolojia ya habari aliibua wazo la kuunganisha ushauri wa kisaikolojia na mtandao wa internet na kuwatafuta washauri wa saikolojia wenye sifa na watumiaji wenye mahitaji, ili kupunguza bei na kizingiti cha ushauri wa kisaikolojia.

    Program ya "NXL" iliwekwa rasmi katika mtandao wa internet mwezi Mei mwaka jana. Katika kipindi cha mwanzo, hawakuna na fedha nyingi, na fedha zilizotumika kujitangaza ni kidogo sana, lakini idadi ya watu waliotumia programu hii ilifikia zaidi ya laki 4 ndani ya miezi kumi ya mwanzo, hii inaonesha wazi kuwa kuna soko kubwa la ushauri wa kisaikolojia nchini China. Lakini kama makampuni mengine yaliyoanzisha biashara hivi karibuni lakini yenye mustakbali mzuri wa soko na mtindo wa kisasa wa biashara, kampuni ya Ji Di pia ilikumbwa na matatizo mbalimbali katika kukusanya fedha.

    "Tulipokusanya fedha nje, tuliwakuta watu wengi wasiokuwa na uhakika au kusitasita. Wengi wao wanafahamu kuwa ushauri wa kisaikolojia una soko kubwa, lakini hili bado ni jambo jipya, wao wanapendelea kusubiri."

    Kampuni iliyotoa huduma za kuitangaza programu hiyo sokoni pia ni kampuni mpya iliyoanzishwa mwaka jana, na wazo lake la biashara ni kusaidia kampuni mpya kukua vizuri na kutoa huduma za mpango wa chapa na mtindo wa kibiashara.

    Mwenyekiti wake Cao Jun ana uzoefu mkubwa katika usanifu, matangazo na uhusiano wa umma. Akizungumzia hali ya sasa ya makampuni yaliyoanzisha biashara hivi karibuni, Cao Jun amesema kiwango cha makampuni mengi ya aina hiyo kushindwa kuendelea ni cha juu, njia chache na utaratibu wenye utata wa kukusanya pesa vimefanya makampuni mengi mapya kufa ndani ya miezi kadhaa. Cao Jun amesema katika mazingira ya "ujasiriamali na uvumbuzi wa umma", serikali kweli imetangaza sera za kuunga mkono makampuni mapya, lakini jinsi ya kufikisha msaada wa kifedha mikononi mwa makampuni hayo bado haijafahamika.

    "Ni vigumu. Kila wilaya mjini Beijing ina mfuko wa kuunga mkono ujasiriamali, lakini tangu utoe ombi hadi fedha zitolewe, hii inachukua muda mrefu ambao huwa ni nusu mwaka, pia unahitaji kuwasilisha nyaraka mbalimbali, ambapo kama kweli unataka kufanya jambo fulani, tayari umechelewa."

    Mbunge wa China Xu Aihua amefuatilia maisha na maendeleo ya makampuni mdogo kwa miaka mingi. Akiwa mjasiriamali kutoka sehemu ya vijijini, Bibi Xu anafahamu sana ugumu wa kuanzisha biashara. Akizungumzia jinsi ya kutatua tatizo hilo, amesema makampuni mapya yanakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo ukosefu wa uhakika na uvumilivu kwenye jamii, kwa hiyo ametoa wito wa kuanzishwa kwa utaratibu wa kugawa hatari wa ujasiriamli na uvumbuzi.

    "Moja ni kuwapa mazingira mazuri ya biashara, pili ni kujenga mtandao wa kikanda wa uvumbuzi, haswa utaratibu wa kugawa hatari za jamii kwa makampuni hayo yanayoendeleza uvumbuzi, ikiwa ni pamoja na unafuu wa kodi, na kuanzisha mfuko wa sera ili kuwaunga mkono na kuwasaidia. Pia naona tunaweza kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha mfuko wa uvumbuzi, halafu mfuko unaoshirikisha serikali na sekta binafsi unaweza kuwasaidia kupata njia nyingi zaidi za kukusanya fedha."

    Mbunge mwengine wa China ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya Mi Bw. Lei Jun anaona kuwa kuhamasisha mitaji ya sekta binafsi kushiriki kwenye ujasiriamli na uvumbuzi ni njia muhimu ya kutatua tatizo la ukusanyaji fedha linaloyakabili makampuni mdogo. Anasema,.

    "Ukusanyaji fedha wa makampuni madogo ni suala kubwa lenye utata. Naona cha muhimu zaidi ni kushirikisha nguvu za kijamii, kuhamasisha mitaji mingi zaidi ya jamii kushiriki kwenye mkondo wa ujasiriamali. Naona huu ni ufumbuzi muhimu."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako