• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ndoto ya vijana wa mji wa Chengdu ya kuanzisha jarida binafsi

    (GMT+08:00) 2016-05-12 15:18:50


    Bi. Zhang Jianlan ni msichana wa mji wa Chengdu, kutokana na upendo mkubwa kwa usanifu wa vitabu, miaka miwili iliyopita yeye na mwenzake Bi. Xue Rong walianzisha jarida lao binafsi liitwalo "Keyi". Ili kuwajulisha wasomaji wa sehemu mbalimbali kuhusu hadithi za Chengdu, wasichana hao wawili walijitahidi kutimiza ndoto zao kwenye sekta ya uchapishaji ambayo hawakuwa na uzoefu hata kidogo.

    Bi. Zhang Jianlan alisomea kozi ya usanii chuo kikuu, ingawa baada ya kuhitimu alitaka kuwa mjasiriamali, lakini kutokana na upungufu wa uzoefu, aliamua kufanya kazi kwanza katika kampuni moja ya matangazo mjini Beijing. Baada ya kuhimili pilikapilika za kazi kwa miaka mitatu, alianza kuangalia upya hali ya maisha yake. Wakati huo huo mazingira mazuri ya kiutamaduni pia yalimchochea afikirie tena ndoto yake ya awali. Anasema,

    "Ndani ya miaka mitatu nilipoishi mjini Beijing, nilitazama drama nyingi, pia nimefahamu majarida mengi ya nchi za nje, napenda sana vitu kama hivyo, pia napenda kufanya utafiti wa vitu hivyo. Wakati ule nilifikiri kuwa ninataka kushughulikia kazi zinazohusiana na vitabu, ili kutafuta hisia za awali nilizokuwa nazo mara baada ya kuhitimu chuo kikuu."

    Hivyo Bi. Zhang Jianlan alitumia fursa ya kurudi mjini Chengdu, kukutana na rafiki yake mkubwa Xue Rong, na kumwambia mpango wake wa kuanzisha jarida la "Keyi". Wasichana hao wawili mara moja walifikia maoni ya pamoja, na kuanza shughuli zao za ujasiriamali. Wanafanya kazi mbalimbali za maandalizi wenyewe, kwa mfano wa kufanya mahojiano, kusanifu kurasa za jarida, na kuchagua karatasi za kuchapishwa.

    Jarida la "Keyi" linaeleza hadithi zilizotokea mjini Chengdu, kupitia mahojiano na watu mbalimbali wa kawaida. Bi. Zhang Jianlan anasisitiza kuwa, yeye na Xue Rong wanataka kulifanya jarida hilo liwe na uhusiano wa karibu na wasomaji, na kuonesha hali halisi ya maisha mjini Chengdu.

    "Mwanzoni wakati tulipojadili walengwa wa jarida letu, tuliona majarida mengi ya sasa yanaeleza maisha ya watu wa sekta ya utamaduni na burudani, ambayo ni mbali na maisha ya watu wa kawaida. Tulitaka kuanzisha jarida linaloeleza hali halisi ya watu wa kawaida, ili wasomaji wetu waweze kuona kumbe kuna watu wengi wanaofanana nao karibu nao, ambao wanaishi kwa furaha. Licha yao kurudi nyumbani, kula chakula na kulala, unaweza kugundua mambo mengine yenye furaha. "

    Kama tunavyojua, hivi sasa vyombo vya habari vinavyotumia makaratasi vinakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka vyombo vya habari vya aina mpya. Hivyo ni kazi ngumu sana kwa wasichana hao wawili kuendesha jarida lao binafsi. Bi. Xue Rong amesema ili kupata pesa za kutosha za kudumisha uendeshaji wa jarida hilo, yeye na Zhang Jianlan wamelazimika kufanya kazi nyingine za usanifu. Kwa bahati nzuri, wao wana marafiki wengi ambao wanapenda kuwasaidia bila malipo. Bi. Xue Rong anasema,

    "Hivi sasa timu yetu inaundwa na sisi wawili na marafiki zetu. Mimi na Zhang Jianlan ni full-time, na wengine ni part-time, wakiwemo wapiga picha, na waandishi."

    Msichana Wang Jing ni mwandishi wa jarida la "Keyi", ambaye ameshiriki kwenye kazi nyingi za uandishi na kufanya mahojiano. Wang Jing alisema, mwanzoni alipoambiwa wazo la kuanzisha jarida hilo, alikubali mara moja, hivyo aliamua kujiunga na timu ya jarida hilo. Anasema,

    "Uzuri wa Jarida la Keyi ni kwamba hawajali gharama wanapopata stori za kuvutia zinazostahili kuandikwa. Kwa mfano wanaweza kwenda mlimani au sehemu nyingi ili kufanya mahojiano na mtu asiyejulikana, kama mtu mmoja anayefuga nyuki. Wazo hili linanivutia sana."

    Bi. Zhang Qi ni mpiga picha wa jarida la Keyi, alisema ana wasiwasi kwa mustakbali wa vyombo vya habari vinavyotumia makaratasi, lakini kutokana na upendo kwa ndoto yake, aliamua kuendelea pamoja na wenzake wa jarida hilo. Anasema,

    "Kimsingi hatuna malipo, kama hatuna wazo na ndoto ya pamoja, tusingeendelea kwa muda mrefu hadi sasa katika hali ya kutokuwa na malipo. Natumai nitakua pamoja na jarida hilo kwa muda mrefu zaidi. "

    Hivi saa matoleo matatu ya Jarida la Keyi yamechapishwa, na matoleo ya nne na ya tano yameingia kwenye kipindi cha usanifu wa kurasa na mahojiano. Wasichana hao awali walipanga kuchapisha matoleo manne kila mwaka, lakini kutokana na upungufu wa fedha na sababu nyingine, walilazimika kupunguza nusu ya matoleo kwa mwaka. Lakini mshikamano kati yao unawahimiza wakue bila kusita.

    Msichana Li Aiyou ni mwandishi na mpiga picha wa jarida la Keyi, alisema kujiunga na timu ya jarida hilo kunamfanya aelewe uzuri tofauti wa mji wa Chengdu, pia mchakato wa kuanzisha jarida hilo pia umetia nguvu ya uhai kwa maisha yake. Anasema,

    "Nilikumbuka wakati naandaa jarida la toleo la pili, niliandika makala moja, ambayo inaeleza jinsi nilivyojiunga na timu ya jarida hilo. Ukiona mchakato wa ukuaji wa jarida hilo, utajionea sana. Unaweza kuona jarida hilo kuwa ni zuri zaidi. Kwenye mwisho wa makala hiyo niliandika kuwa, natumai kulihudumia jarida hilo kwa muda mrefu zaidi."

    Mwezi Aprili mwaka huu, kutokana na mapendekezo ya mhariri wa jarida jingine binafsi, jarida la Keyi limeoneshwa kwenye maonesho ya vitabu na sanaa ya Singapore. Haya ni mafanikio ya vijana hao ambao walifanya juhudi za miaka miwili, na pia ni mwanzo mpya kwao.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako