• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kampuni ya viatu ya China nchini Ethiopia

    (GMT+08:00) 2016-05-16 19:36:04


    Umbali wa kilomita 30 hivi kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuna eneo moja la viwanda la kisasa, na kiwanda cha viatu vya wanawake cha China cha Hua Jian ndio kiko katika eneo hilo. Ukiwauliza wakazi wa Addis Ababa, wote wanajua kiwanda cha viatu cha Hua Jian kilichopo katika eneo hilo la viwanda.

    Ethiopia ni moja kati ya nchi zenye historia ndefu barani Afrika, na pia ni makao makuu ya Umoja wa Afrika. Katika miaka 12 iliyopita, uchumi wa Ethiopia ulikua kwa kasi ya tarakimu mbili, lakini nchi hiyo bado inahesabiwa kuwa nchi iliyo nyuma kimaendeleo duniani. Katika nchi hiyo yenye watu karibu milioni 100, wastani wa kipato cha mtu mmoja haufikii dola za kimarekani 500, zaidi ya asilimia 80 ya watu ni wakulima, na asilimia 40 ya pato la taifa GDP linatokana na kilimo.

    Mwezi Agosti mwaka 2011, aliyekuwa waziri mkuu wa Ethiopia Hayati Meles Zenawi alifika Shenzhen kuhudhuria ufunguzi wa michezo ya wanafunzi wa vyuo vikuu duniani. Lakini lengo kuu la ziara yake hiyo nchini China ni kuiletea nchi yake sekta inayohitaji nguvukazi nyingi ya China, na kutumia ipasavyo nguvu bora ya Ethiopia ya bei nafuu ya rasilimali za watu, kuendeleza sekta ya viwanda ghafi ya nchi hiyo, na kutatua tatizo la ukosefu wa ajira unaokabili karibu nusu ya watu wote wa Ethiopia.

    Kutokana na pendekezo la mchumi wa China Lin Yifu, Hayati Zenawi alikwenda mji wa Dongguan, mkoani Guangdong kutembelea kampuni ya Hua Jian inayotengeneza bidhaa zinazohusiana na viatu kwa nchi zilizoendelea, na pia kuwaalika kutembelea na kufanya ukaguzi kuhusu uwekezaji nchini Ethiopia. Akikumbusha yaliyotokea katika ziara yake ya kwanza nchini Ethiopia, naibu meneja mkuu wa kampuni ya Hua Jian tawi la nchini Ethiopia Song Yiping anasema,

    "Mwezi Septemba mwaka 2011, mwenyekiti wa kampuni yetu Zhang aliongoza ujumbe wetu kuja nchini Ethiopia. Mwezi Januari tulitia saini mkataba, na baada ya miezi mitatu, tukaanza uzalishaji. Wakati ule, tulikodisha kiwanda kimoja, pia tulialika kampuni maarufu za biashara za Marekani na wateja wetu kuja Ethiopia kufanya ukaguzi. Niliona mwaliko wa Hayati Zenawi ulikuwa sahihi, mwelekeo pia ulikuwa sahihi, ndiyo maana tuliamua kufanya ushirikiano nao."

    Ushirikiano kati ya Ethiopia na kampuni ya Hua Jian unahesabiwa kuwa wa kunufaishana. Ikiwa kampuni ya sekta inayohitaji wafanyakazi wengi, Hua Jian inahitaji nguvu kazi nyingi na zenye bei nafuu pamoja na malighafi. Ethiopia ni nchi ya pili kwa idadi ya watu barani Afrika, kiwango cha ukosefu wa ajira kilifikia asilimia 50, lakini wakati huohuo ni nchi yenye utariji wa ngozi bora, na inahitaji sana ujio wa kampuni kama Hua Jian.

    Tokea mwaka 2012 uzalishaji ulipoanza hadi sasa, wafanyakazi wa Hua Jian nchini Ethiopia wamefikia elfu nne, kati yao 3,800 ni wenyeji. Katika kiwanda hicho, kazi zao zimegawanywa vizuri, na kila mmoja wao ana shughuli yake binafsi. Wafanyakazi hao wanaweza kufanya vizuri hatua mbalimbali za kutengeneza viatu, kama vile kukata, kubandika na kushona, na kila siku wanaweza kutengeneza viatu elfu 6.5 vya wanawake. Hivi sasa, kiwanda cha Hua Jian nchini Ethiopia kinauza nje viatu milioni 2 vya wanawake kila mwaka, faida ni asilimia 10.

    Akizungumzia kuhusu wafanyakazi wenzao wa kiafrika na kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi katika kiwanda hicho, Song Yiping anasema kwa kujivunia,

    "Tunawaongoza ndugu zetu wa kiafrika, kuwapa mafunzo ya kiufundi na kuwasaidia wajikimu kimaisha, na pia kusaidia nchi hiyo kuuza ngozi zake nje ya nchi, kuwafundisha wafanyakazi wake, kutoa nafasi za ajira na kustawisha soko la taifa hilo."

    Kabla ya hapo, kuna vyombo vya habari vya kimagharibi vilivyoripoti kuwa kiwanda cha Hua Jian kimeweka kanuni kali za kinidhamu kwa wafanyakazi wazawa wa Ethiopia. Bw. Song anasema nidhamu kali na yenye ufanisi ni sharti la lazima katika kuandaa wataalamu wa kutengeneza viatu. Mitazamo ya waafrika na wachina kuhusu kazi ni tofauti, hivyo kiwanda cha Hua Jian pia kilijifunza mengi katika kipindi chake cha mwanzo kilipoanza shughuli zake.

    Wakati ule, kutengeneza viatu lilikuwa ni jambo geni kwa waethiopia, japokuwa nguvukazi ilikuwa nafuu, lakini ufanisi wa wafanyakazi ulikuwa ni mdogo ukilinganishwa na ule wa wafanyakazi wa kichina, na kiwango cha viatu visivyokidhi vigezo kilikuwa cha juu sana. Ili kutatua suala hilo, Hua Jian ilifanya juhudi kubwa katika kuandaa wataalamu.

    Kuhusu utoaji mafunzo kwa wafanyakazi wapya, Hua Jian ilijenga darasa maalumu, na walimu wenye uzoefu wa China waliwafundisha wafanyakazi wenyeji jinsi ya kutengeneza kwa mikono au kutumia mashine. Kwa wale wanaofanya vizuri, Hua Jian iliwapa fursa ya kupewa mafunzo katika makao makuu ya Hua Jian au shule ya ustadi kazi hapa nchini China, ambapo walijifunza kutumia mashine, kusimamia kampuni na pia lugha ya kichina. Hivi sasa, wafanyakazi wengi waliopewa mafunzo China wamechukua nyadhifa muhimu na kushiriki kwenye usimamizi.

    "Wafanyakazi bora walipelekwa na kujifunza nchini China, katika mwaka wao mmoja hapa China, walijifunza lugha ya kichina, ufundi, usimamizi, na pia kufanya mazoezi ya kazi katika viwanda vyetu vya China. Mazingira ya hapa China ni mazuri kuliko yale ya Ethiopia, na mashine pia ni nzuri. Ndiyo maana asilimia 60 hadi 70 ya maofisa wa sasa waliwahi kupewa mafunzo hayo."

    Frazier ni kijani mwenye umri wa miaka 22, na amefanya kazi katika kiwanda cha Hua Jian nchini Ethiopia kwa miaka minne. Kutokana na kazi yake nzuri, aliwahi kupelekwa na kupewa mafunzo katika makao makuu ya Hua Jian yaliyopo mjini Dongguan nchini China. Baada ya mafunzo ya miaka miwili, alirudi kwenye kiwanda cha Hua Jian nchini Ethiopia. Hivi sasa anawasimamia wafanyakazi wenzake katika karakana ya kwanza ya kiwanda hicho. Akihojiwa na mwandishi wetu wa habari, anasema kwa kichina sanifu,

    "Jina langu la kichina ni Guang Zhou. Awali, sikufahamu chochote, sikufahamu jinsi ya kutengeneza viatu, wala lugha ya kichina. Lakini baada ya kwenda China, kulikuwa na walimu wengi, ambao walitufundisha jinsi ya kubandia, kushona, na hata kukata, ufundi wangu wote nilijifunza nilipokuwa China."

    Vyombo vya habari vya Ethiopia viliwahi kuuliza kuwa Hua Jian imefanya biashara yake nchini Ethiopia kwa miaka minne mitano, na lini itakuwa na afisa wa juu mwethiopia. Bw. Song anasema hii inahitaji uzoefu na ufundi, ambavyo vinapatikana kwa muda mrefu.

    "Tumekuwa tukijitahidi kuandaa viongozi wenyeji, lakini haiwezekani kuwa kiongozi asipokuwa na uzoefu wa kazi wa miaka kumi. Je, kila hatua katika kutengeneza viatu unafahamu? Jinsi ya kupanga vizuri hatua zote unafahamu? Mambo hayo yanahitaji mafunzo ya zaidi ya miaka kumi, halafu anaweza kuwa kiongozi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako