• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wanawake 831,000 nchini Kenya kupata chanjo ya pepopunda

    (GMT+08:00) 2016-05-23 10:19:37
    Wasichana na wanawake 831,000 walio na umri wa kati ya miaka 15 na 49 wamelengwa kwa ajili ya dozi ya tatu ya chanjo ya pepopunda katika kampeni ya iliyoanzishwa mwishoni mwa wiki jana nchini Kenya.

    Walengwa wanapatikana katika kaunti 11 nchini Kenya,ikiwa ni pamja na kaunti za Kilifi,Mombasa,Meru,Mandera,Wajir,Garissa,Baringo,West Pokot,Turkana,Samburu na Narok ambazo zimetajwa kama maeneo yaliyo katika hatari kubwa,ambapo kuna uwezekano wa wanawake kuambukizwa pepopunda na kuisambaza kwa watoto ambao hawajazaliwa.

    Kampeni hii itaendelea hadi tarehe 26 Mei.

    Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya nchini Kenya Dkt Nicholas Muraguri amesema lengo la kutokomeza pepopunda miongoni mwa akina mama wajawazito ni kupunguza visa vya watoto wanaozaliwa na pepopunda hadi chini ya kisa kimoja katika watoto 1,000 waliozaliwa hai katika kila kaunti ndogo.

    Wakati akizindua kampeni hiyo jijini Nairobi alhamisi iliyopita,Dkt Muraguri alisisitiza kuwa chanjo hiyo iko salama na kuongeza kuwa ndio chanjo inayotumiwa kote duniani.

    Aidha Dkt Muraguri amesema wizara ya afya inalenga kuwapatia chanjo watoto milioni 19 walio kati ya umri wa miezi 9 na miaka 14 na wanawake zaidi ya 800,000.

    Kanisa katoliki nchini Kenya tangu mwanzo ilipinga chanjo hiyo ,likisema kwamba chanjo hiyo imechanganywa na dawa ambazo huenda zikafanya wanawake kutoshika uja uzito na pia kanisa hilo lilitishia kuwaambia wanachama wake kutochukua chanjo hiyo.

    Kufikia sasa msimamo wa kanisa hilo kuhusiana na chanjo hiyo bado haujaeleweka.

    Hata hivyo wizara ya afya ,shirika la afya duniani (WHO) na Unicef walipuuzilia mbali madai ya kanisa hilo na kusema kwamba chanjo hiyo iko salama.

    Dozi ya pili ya chanjo hiyo ilitolewa mwaka jana huku kukiwa na utata.

    Serikali iliwasilisha vipimo vilivyofanywa katika maabara ya kitaifa ya udhibiti wa ubora na kusema kwamba matokeo yamaeonesha chanjo hiyo iko salama.

    Shughuli hii ya upeanaji chanjo inaendeshwa nchini kote katika vituo vya afya vya serikali na baadhi ya makanisa na shule.

    Kutakuwa na vituo 20,000 vya upeanaji chanjo huku kukiwa wafanyakazi wa afya 42,000 na watu 24,000 wa kujitolea.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako