• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • TRA 'kila mahali' kudai risiti kwa EFD

    (GMT+08:00) 2016-07-27 19:56:08
    MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha operesheni nchi nzima ya kudai risiti kutoka kwa wananchi wanafanya manunuzi mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara wanaotakiwa kuwa na mashine za kielektroniki (EFD).

    Akizungumza jana Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema operesheni hiyo iliyoanza mwanzoni mwa mwezi huu inatekeleza matakwa ya sheria.

    Hivi karibuni Bunge lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine inampa wajibu mwananchi kudai risiti za kielektroniki anapofanya manunuzi na kama atashindwa kufanya hivyo atapewa adhabu ya kulipa faini ya kuanzia Sh 30,000 hadi Sh milioni 1.5 kulingana na thamani ya bidhaa aliyonunua.

    "Ili kuhakikisha wananchi wanatekeleza sheria kwa kudai risiti wanaponunua bidhaa, tumeanza operesheni ambayo maofisa wa TRA watamtaka mwananchi kuonesha risiti ya bidhaa alizonunua. Wananchi wanatakiwa kujua kuwa jukumu la kudai risiti si la TRA pekee bali ni la kila mwananchi," alisema Kayombo.

    Alisema mwananchi anapofanya manunuzi yoyote anatakiwa kudai risiti na kuhakikisha anaangalia kama ni ya TRA, iwe na Namba ya Utambulisho ya Mlipa Kodi (TIN number), risiti ina kiasi sahihi kilicholipwa na tarehe husika ya manunuzi yaliyofanyika.

    "TRA imegundua udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, wanatoa risiti siku tatu zilizopita, ina maana watu wanakuwa na risiti na wanasubiri mtu akidai basi wanampa kumbe haina bidhaa sahihi, kiasi cha fedha zilizotolewa na tarehe ya manunuzi," alisema.

    Kayombo alitoa tahadhari hawa kwa wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo yao kwenda mikoani kuhakikisha wanakuwa na risiti sahihi za mizigo yao ili kukwepa usumbufu wa njiani sambamba na kutozwa faini.

    Aidha, Kayombo amewataka wananchi kuwa makini na kukataa kurubuniwa na wafanyabiashara ambao wanadai hawezi kutoa risiti kutokana na mtandao kutokana na kuwa utoaji wa risiti hautegemei mtandao bali mashine kuwa na chaji na kuwa mtandao unatumika kwa wafanyabiashara wanapotuma ripoti.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako