• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Reli ya kisasa kuboresha uchumi wa Ethiopia na Djibouti

    (GMT+08:00) 2016-10-06 19:46:29

    Reli ya kisasa inayounganisha mji wa Addis Ababa nchini Ethiopia na ule wa Djibouti imezinduliwa.

    Reli hiyo mpya ina urefu wa kilomita 752.7 na treni itatumia umeme.

    Mradi huu umetekelezwa na kampuni mbili za China na kugharimu dola bilioni 4 za kimarekani.

    Ni afueni kwa Ethiopia ambayo ni nchi isiyokuwa na bandari ya baharini kwani sasa reli hii itarahisisha uchukuzi wa bidhaa kwa wingi kupitia bandari ya Djibouti.

    Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn wakati wa uzinduzi wa reli hiyo anasema.

    "Mpango tulio nao kupitia ujenzi wa miundo mbinu ni kuleta mageuzi ya kiuchumi katika nchi yetu. Kupitia kwa mpango huo tunafanyia mageuzi mfumo wetu wa miundo mbinu na hivyo kupunguza umaskini. Kabla ya kuanza mradi huu wa reli ya kisasa ilikuwa ni vigumu kupata maendelo ya kiuchumi kwa haraka na hatungesindana ipasavyo. Reli hii ya zaidi ya kilomita 750 itatumia asilimia 100 ya kawi ya umeme na ndio ya kwanza ya aina yake barani Afrika ambayo itaunganisha Djibouti na Afrika Mashariki"

    Imechukua miaka sita kukamilisha mradi huu na kasi ya treni itakuwa ni kilomita 120 kwa abiria nayo ile ya mizigo ikiwa na kasi ya kilomita 90 kwa saa.

    Reli ya zamani ya upana wa mita moja iliojengwa na Ufaransa zaidi ya karne moja iliyopita kwa sasa haitumiki.

    Ukosefu wa njia ya haraka ya kusafirisha bidhaa na watu umepelekea ukuaji dhaifu wa uchumi na pia vijana wengi wakisalia bila ajira.

    Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh anasema.

    "Ilikuwa inachukua wiki sita kusafiri kutoka bandari ya Djibouti kwenda Addis Ababa, lakini sasa kwa kutumia treni hii mpya ya umeme itachukua masaa 7 tu kusafirisha watu na bidhaa kati ya miji yetu mikuu. Kwa mara nyingine tena watu wetu wameungana kujenga upya reli hii na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo yetu"

    Asilimia 70% ya ufadhili wa reli hii imetolewa na benki ya Exim ya China huku serikali ya Ethiopia ikigharamia asilimia 30.

    Mwakilishi wa Rais Xi Jingping wakati wa uzinduzi wa reli hiyo mpya bwana Xu shaoshi anasema China itaendelea kufadhili miradi ya miundo mbinu barani Afrika, kama alivyotangaza Rais Xi kwenye mkutano wa FOCAC nchini Afrika Kusini mwaka jana.

    Pia anautaja mradi huu wa Ethiopia na Djibouti kama hatua mpya ya ushirikiano kati ya Afrika na China.

    "Kufunguliwa kwa reli ya Addis Ababa kwenda Djibouti sio tu hatua kubwa ya ushurikiano kati ya nchi zote tatu lakini pia ni mwanzo mpya wa ushirikiano wa siku za baadaye. Katika siku za usoni China inatafanya kazi kwa karibu na Ethiopia na Djibouti katika nyanja mbalimbali zenye kufaidi watu wa pande zote"

    Baada ya sherehe ya uzinduzi zaidi ya wakaazi 2,000 walipata fursa ya kuingia bila kulipa katika treni mpya na kusafiri kwa kilomita 10 hivi.

    Bwana Omar Soubagleh ambaye ni mfanyibiashara kutoka Djibouti anaona kwamba treni hii itasaidia kuendeleza biashara yake.

    "Namiliki mojawepo wa viwanda vikubwa vya nyama nchini Ethiopia, kwa hivyo reli hii itasaidia sana kukuza biashara yetu hasa kusafirisha mifugo kutoka vijijini hadi kwenye kiwanda chetu na pia kusafirisha nyama kutoka kiwandani hadi Djibouti na maeneo mengine ya Ethiopia"

    Mke wake Araksan Housein anajiangalilia mahadhari ya nje milima na watu wanaochunga mifugo huku akipiga picha.

    Hakuwahi kudhani siku moja atasafiri kwenye treni ya iana hii, anasema.

    "Nimefurahi sana kuwa kwenye hafla hii kwa sababu kwa maisha yangu sijawahi kupanda treni, najihisi kama niko nchi kama Marekani ama Canada ambako wanatumia treni kama hizi. Zamani nilikuwa napanda basi tu na ilichukua kama siku tatu hivi, na nauli ilikuwa kama dola 50. Naweza kusema sasa nitakuwa napanda hii treni kila baada ya siku tano hivi. Naweza kula kiamsha kinywa Addis Ababa na chakula cha mchana nakula Djibouti."

    Wakati wa ujenzi wa mradi huu zaidi ya wenyeji 15, 000 wamepokea mafunzo ya jinsi ya kuendesha, kukarabati na kutunza reli na treni.

    Mojawepo wa wale waliopokea mafunzo ni madereva wa treni hii ya umeme kama vile Nabiyu Melaku.

    "Kabla hatujaanza kuendesha treni yenyewe kwanza tulipata mafunzo ya kinadharia darasani kwa miezi miwili hivi tukifunzwa maswala kama vile ya kiusalama halafu mwalimu wa china akatuonyesha jinsi ya kuendesha treni. Jambo la kwanza kabla ya kuingia kwa treni ni kuangalia na kuhakikisha kila kitu kiko sawa. Hii treni ni tofuati kidogo unapoingia ndani hauna haja ya kuchunguza kila upande kwa sababu kuna komputa inayokuonyesha vitu kama vile breki, oparesheni na kamera ya ndani na nje."

    Kulingana na mkurungenzi wa kampuni ya ujenzi wa reli ya China CREC, kwa jumla zaidi ya wafanyikazi 20, 000 walihusika kwenye ujenzi wa reli hii asilimia 90 ikiwa ni wenyeji.

    Ding Ji Hua amekuwa akiongoza utoaji wa mafunzo ya ndani ya treni hii mpya.

    "Tumetoa mafunzo kwa zaidi ya wahudumu 40 wa hapa Ethiopia. Kila siku tunawafunza jinsi ya kuhudumia wasafiri na kuwapa mahitaji ya ndani ya treni. Lakini pia tumebadilisha kidogo mbinu ya utoaji huduma kutoka ile ya Kichina hadi ile inayoendana na desturi za hapa. Tunawafunza kuhusu vifaa ama sehemu ambazo hawafai kushika na pia jinsi ya kutumia vifaa kama vile kifaa cha kuzima moto. Pia tunawafunza kuwakataza abiria vitu ambavyo ni hatari ndani ya treni "

    Mafunzo yake yamezaa matunda, na wanafunzi wake wote 40 wakiwa na sare za zabarau wako tayari kutoa huduma.

    Worknesh Betru ndiye atakayeongoza wahudumu wa Ethiopia kwenye huduma za ndani ya treni.

    "Tunatoa huduma kwa abiria na pia kuhakikisha usalama wao na wa treni.Kwa mfano tunawaonyesha abiria nambari ya kiti na kuwaeleza kwamba hakuna kuvuta sigara. Pia tunawapea vinywaji kama chai na kahawa. Awali nilifanya kazi kama mtoa huduma kwa wateja kwa hivyo kazi hii ni rahisi kwangu"

    Ethiopia inawekeza fedha nyingi kwenye miradi ya reli na hadi sasa imejenga kilomita 2,400 ikiwa ni sehemu ya kufanikisha ruwaza yake ya kiuchumi ya kuwa na uchumi wa wastani ifikapo mwaka 2025.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako