• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rwanda nchi ya kwanza duniani kuanzisha marufuku ya mifuko ya plastiki.

    (GMT+08:00) 2016-11-24 10:03:28

    Mwaka 2008 ,serikali ya Rwanda ilikuwa nchi ya kwanza duniani kupiga marufuku matumizi ya aina yoyote ya mifuko ya plastiki katika nchi hiyo.

    Marufuku hiyo imechangia mafanikio makubwa nchini humo katika kuimarisha mazingira safi,kudumisha afya njema pamoja na kuchangia kwenye uchumi kwa kuvutia watalii.

    Ahmed Bahajj ametembea Kigali hivi karibuni na kutuandalia ripoti hii.

    Katika safari yangu jijini Kigali hivi majuzi,kwenye kituo cha ndege wakati wa ukaguzi ,baadhi ya bidhaa zangu zilizuiwa na maafisa wa zamu.

    Sio kutokana na kuwa labda nlihusika na uhalifu ,la hasha bali nlivunja moja ya sheria ya nchi hiyo bila kukusudia."Kubeba bidhaa kwa mifuko ya plastiki"

    Nchini Rwanda ,wizara ya mazingira mwaka 2008 iliweka sheria mpya ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

    Hii ni baada ya tafiti mbali mbali kudhihirisha kwamba mifuko ya plastiki ilisababisha uchafu katika miji,iliharibu mazingira na haikuwa na mchango wowote kwenye uchumi wa taifa hili badala ya hasara.

    Leo hii ikiwa ni miaka 8 tangu kuanzishwa kwa utekelezaji wa sheria hiyo,ni bayana kwamba Rwanda imefanikisha manufaa mengi na marufuku hiyo.

    Katika pita pita zangu kwenye jiji kuu la Kigali,nlijihisi nipo kwenye sehemu ya kuvutia,hewa safi mandhari ya haiba ya kupendeza ,dakika moja tu utagundua mji huu uko tofauti sana na miji mengi Afrika .

    Hata hivyo kufikia hatua hii ilihitaji juhudi kubwa ya kuhamasisha jamii kupitia kwa elimu ya uhifadhi wa mazingira .

    Nlimuuliza waziri wa elimu Papius Musafiri hatua ya kwanza ya utekelezaji wa sheria, je ilikuwa vigumu sana kwa raia kukubali?

    "Mwanzo ilikuwa ngumu sana ,kuweka sheria kuweka mikakati na adhabu kwa watakaovunja sheria.tulifanya utafiti na wanasayansi na tukaamua tutahakikisha tunatunza mazingira"

    Nchini Rwanda mtu anaweza kufungwa jela kwa kufanya biashara haramu ya mifuko ya plastiki na kuingiza nchini humo.

    Rwanda inajivunia kwamba imekuwa nchi ya kwanza katika historia kuanzisha sheria jambo ambalo waziri Musafiri anasema walilibuni wenyewe tu sio kuiga kokote

    "Inabidi waafrika tujifunze kuanzisha vitu vyetu sio kuiga ,huu ni ujuzi wetu hatukuchukua marekani wala ulaya ni hapa kwetu tu na sas ulimwengu utaiga kutoka kwetu."

    Kutaka kufahamu zaidi kuhusiana na jambo hili nakutana na Mkurugenzi wa halmashauri ya uhifadhi wa mazingira nchini Rwanda Dk Mukankomeje Rose.

    Akiongea katika lugha ya Kinyarwanda anasimulia changamoto walizokabiliana nazo katika utekelezaji wa amri hii.

    "Rwanda ni nchi ambayo inaendelea sasa ,haikuwa na viwanda vya kutosha vya kutengeneza aina nyingine ya mifuko ambayo ingekuwa salama kwa mazingira yetu,serikali ililazimika kuwekeza fedha nyingi katika jambo hili ,na hapo karatasi zilitumika kwa shuhuli za kubebea vyakula na bidhaa nyingine.Sasa tumepiga hatua viwanda vimebuni ajira na kupunguza umaskini pamoja na kuhifadhi mazingira"

    Pindi unapowasili katika uwanja wa ndege wa Kigali ,Maelezo ya marufuku ya plastiki na matangazo yanatolewa kwa wageni ama watalii kuhakikisha hawaingii nchini humo na mifuko ya plastiki.

    Waziri Musafiri anatufahamisha zaidi

    "Tuliweka sheria,tuliweka matangazo,tulieleza wananchi kuhusu hili na baada ya hapa tulihakikisha kwamba wageni hawaingii na mifuko,tunatoa karatasi kwa wageni kubebea bidhaa zao.Hata kwenye ndege tunatoa matangazo,tumefanikiwa"

    Wananchi wa Rwanda wamechangia pakubwa kwenye ufanisi wa sheria hii kwani

    "Hapa Rwanda, huwezi kuona hata mfuko mmoja wa plastiki ukitapakaa barabarani,ukipepea kwenye miti na hata ukifunga mitaro ya maji"

    "Tunafurahia sana usafi wa nchi yetu kwani mazingira safi ni maisha safi bila magonjwa.

    "Mifuko ya plastiki husababisha uchafu na kero,sisi hapa Rwanda tumeanzisha marufuku hii na iwapo nchi nyingine zitaiga zitaona manufaa yake'

    Mbali na sheria hii,Rwanda imeendeleza kudumisha mazingira kwa kutenga siku maalum kila mwezi kwa ajili ya usafi wa nchi.

    Siku hii inajulikana kama Umuganda ambapo raia wote wenye umri wa miaka 18 hadi 65 hujitolea kwa ushirikiano kufanya usafi wa mji.

    Harakati hizi za Rwanda zimetambuliwa kote duniani .Rwanda imepewa tuzo chungu mzima za usafi na moja ikiwa kuteuliwa kama nchi safi zaidi afrika na Kigali kutajwa kama jiji safi zaidi Arkia kwa mujibu wa Umoja wa Mtaifa.

    Utalii nchini humo umekuwa kwa kasi kwani watalii wengi hufika kutembelea turathi za kitaifa na wengine wakivutiwa mazingira safi ya nchi hiyo.

    Raia wa kawaida nchini humo husema Kigali ni gali kutokana na usafii.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako