• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa matende zafikishwa Kilifi

    (GMT+08:00) 2016-12-21 09:50:10

    Serikali ya Kenya imefikisha kampeini ya kukabiliana na ugonjwa wa matende kwenye kaunti ya Kilifi katika juhudi ya kuuangamiza ugonjwa huo.

    Hii ni baada ya utafiti wa kimataifa wa afya kuonya kwamba takriban watu milioni 3 nchini Kenya wanahofiwa kupata maradhi ya matende.

    Elephantiasis maarufu matende ni ugonjwa hatari unaosababiswa na mbu.

    Ukiwa zaidi huwavamia jamii zinazoishi katika mazingira duni yenye viwango vya chini vya usafi,matende husababisha miguu kufura na hata sehemu nyeti za kiume unapokua na makali zaidi.

    Ugonjwa huu huathiri miguu, mikono, figo, korodani na kusababisha korodani kuvimba na kuwa kubwa sana.

    Hali ya hofu imeanza kuendea katika sehemu kame nchini Kenya zilizojaa mbu na ripoti mpya ya mkurupuko wa ugonjwa huu umezidi kusababisha wasi wasi na jeke jeke miongoni mwa wakenya.

    Baada ya kampeini ya kukabiliana na ugonjwa huu kuanzishwa mwezi mmoja uliopita ,wizara ya afya imekita kambi Kilifi wiki hii ikiwa ni moja ya maeneo yanaripotiwa kuwa na visa kadhaa vya maambukizi ya matende.

    Madaktari,wataalamu, maafisa wa afya na usafi watatoa matibabu ya siku tatu kwa waathiriwa,aidha watapeana chanjo dhidi ya ugonjwa huu na kugawanya neti zilizotibiwa kwa wakaazi ili kupunguza maambukizi.

    "Walengwa wa kampeini hii ni wa kutokomeza matende ni watu wote wenye miaka 5 na kuendelea"

    Hizi ni harakati za sekta ya afya nchini kuhakikisha wanaumaliza ugonjwa huu kufikia mwaka 2020.

    Kampeini hii imeanzishwa Mombasa,Tana River,Taita Taveta ,Kilifi na itafikishwa hadi Lamu.

    Afisa mkuu wa kukabiliana na maradhi yaliotelekezwa katika sehemu za joto ama kiangazi Sultani Matendechero amesema ugonjwa huu ulianza kushuhudiwa tena baada ya kupotea kwa miaka mingi kwa sasa ni rahisi kuwapata watoto iwapo hawatapewa chanjo ama kulala kwenye neti zilizotibiwa.

    "Tumeanza na idadi ndogo ya maafisa wa afya katika kutoa elimu ya jamii kuhusu matende,tunajaribu sana lakini bado tuna tatizo kwa sababu watu wenyewe hawajui athari za ugonjwa huu,wanajificha wengine wakidhani ni uchawi ama wamerogwa.tuna hakika kwa ushirikiano imara tutakabiliana nao."

    Waathiriwa wengi wa matende ni wanaume ambao baadhi yao hulazimika kufanyiwa upasuaji wa sehemu nyeti kwa ajili ya matibabu.

    Usafi,kutumia dawa bila kukosa,kusafishwa vidonda ni miongoni tu mwa mambo ambayo yamesisitizwa kwenye kampeini hii.

    Waathiriwa wa matende hupata changamoto nyingi ikiwemo ulemavu wa mwili,msongo wa mawazo,unyanyapaa na kufikilisika kwa matibabu pamoja na kupata umaskini.

    Takriban watu elfu 80 hupata maradhi haya kila mwaka nchini Kenya.

    Serikali imeweka shilingi bilioni 1 kwa kukabiliana na ugonjwa huu huku asilimia 65 ikilengwa kutibiwa na kupewa chanjo.

    Tatizo lingine linalokwamisha juhudi za kukabiliana na matende ni msimamo wa jamii kwamba ugonjwa huu unasabaishwa na uchawi hivyo waathiriwa hutengwa na kufukuzwa wasipate matibabu.

    Kwa mujibu wa Matendechero ni kwamba kampeini hiyo itaendelzwa kwa miaka 4 ikiwa ni pamoja na tafiti tofauti kuanzishwa ili kubuni mbinu mpya za kumaliza matende.

    Kenya inalenga kufikisha chini ya asilimia 1 tu ya visa vya maambukizi ikiwa ni pamoja na kushirikiana na na shirika kuu la afya duniani.

    Serikali aidha imepata usaidizi wa madawa,fedha na mafunzo kutoka kwa GlaxoSmithKline and Eisai.

    Maafisa wa afya kutoka kwa wizara watafikishwa katika sehemu zote kuhamasisha wakenya .

    Juhudi za kumaliza ugonjwa huu aidha zimetiliwa mkazo nchini Tanzania huku Mkuu wa mkoa wa Daresalaam Paul Makonda akizindua kampeini za kutoa matibabu.

    "Tukishaugua magonjwa haya ndio tunafanya bidii kutafuta matibabu lakini tukipewa maelekezo ya kujikinga hua hatuna mda wa kusikiliza nawapongeza nyinyi mulioko hapa ,huduma hii itafanywa kwa siku tano,wanasema heri kinga kuliko tiba"

    Ugonjwa wa matende husababishwa na vimelea aina ya minyoo (parasitic worm) huenezwa na mbu jike aina ya culex. Mbu hawa hueneza ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine.

    Aina nyingine ya ugonjwa wa matende inayojulikana kama nonparasitic elephantiasis au podoconiosis ambayo haisababishwi na vimelea vyovyote hupatikana katika nchi za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi) Sudan, Egypt na Ethiopia.

    Kulingana na shirika la afya duniani WHO watu milioni 947 katika nchi 54 wanaishi kwenye sehemu ambazo zinaweza kupata ugonjwa huu wa matende.

    Kwa mara ya kwanza mamilioni ya pesa yatatumika ili wagonjwa watibiwe matende ugonjwa unaogopewa kutokana na mabadiliko ya kimwili kwa mwaathiriwa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako