• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Marais wa nchi wanachama wa IGAD wakutana Nairobi kujadili wakimbizi wa Somalia

    (GMT+08:00) 2017-03-27 08:54:23

     

    Mkutano wa kilele wa Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki IGAD kuhusu hali ya wakimbizi nchini Somalia umependekeza kuanzisha mfuko wa udhamini ili kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

    Aidha nchi wanachama wa IGAD ziliafikiana kuhusu kuwasaidia wakimbizi wanaorejea Somalia kwa hiyari.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    Marais wa nchi wanachama wa Shirika la Maendeleo la Kiserikali la nchi za Afrika Mashariki,IGAD walikutana jijini Nairobi jumamosi kujadili hatma ya wakimbizi milioni 1 walioko katika kambi mbalimbali ndani ya mataifa wanachama.

    Kenya imekuwa na wakimbizi takriban 300,000 ambapo kati ya hao wakimbizi 60,000 walirudi Somalia kwa hiari kwa msaada wa serikali ya Kenya na Jumuiya ya Kimataifa.

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo amesema uhamasishaji wa rasilimali za kifedha ni sehemu muhimu katika ujenzi mpya wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi nchini Somalia.

    "Huu ukiwa ni mkutano maalum kuhusu ufumbuzi wa tatizo la wakimbizi wa Somalia,inakubalika kimataifa kwamba suluhisho jema ni wakimbizi kurudi kwa hiari.Kufikia sasa wakimbizi 60,000 wamerudi Somalia kwa hiari na wanachangia katika kujenga upya nchi yao.Wakimbizi wengi wa Somalia wanataka kurudi nyumbani.Wanashukuru sana uwepo wa majeshi ya AMISOM katika nchi hiyo kwa sababu matumaini na ndoto zao zinaweza kuwa kweli"

    Aidha Rais Kenyatta alisema mwka jana Kenya ilitoa U$Milioni 100 ,fedha ambazo zilitumika kutayarisha na kuwezesha urejeshwaji wa hiari wa wakimbizi nchini Somalia.

    Wakati huo huo Rais Kenyatta alisema serikali ya Kenya imeahidi kuzijengea uwezo taasisi za serikali ya Somalia ikiwa ni pamoja na ufunzaji wa walimu,manesi na wasimamizi,pamoja na ujenzi wa kituo cha mafunzo kwa vijana.

    "Kenya imeahidi kutoa Shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha mafunzo ya kiufundi katika eneo la Dadaab ambacho kitasajili vijana wa Somalia ili kupata mafunzo mbalimbali.Hata hivyo rasilimali nyingi bado zinahitajika kutoka kwetu sote kwa ajili ya shughuli ya wakimbizi kurudi iwe endelevu.Natoa mwito kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia kujenga miundombinu muhimu ambayo itawezesha wakimbizi kurudi,na huku sisi tukiendelea kuimarisha usalama katika sehemu ambazo hazina usalama nchini humo"

    Rais wa Somalia Mohammed Abdullahi Mohammed amesema kwa sasa itakuwa vigumu kwa wakimbizi wa Somalia kurudi nyumbani kutokana na njaa na ukame ulioathiri nchi hiyo.

    "Miaka michache iliyopita wakimbizi wengi wa Somalia walirudi nyumbani kwa hiyari,lakini hivi sasa njaa na ukame uliokithiri sehemu nyingi Somalia ni changamoto kubwa kwa wakimbizi kurudi nyumbani"

    Aidha Rais Mohammed ametoa wito kwa mashirika ya kimataifa ya ubinadamu kurudi Somalia na kushiriki katika ujenzi mpya wa nchi hiyo.

    "Nachukua fursa hii kutoa wito kwa mashirika ubinadamu na maendeleo kuhamia nchini Somalia na kufanya shughuli zao kutoka ndani ya nchi.Tunaelewa kuwa kuna matatizo ya kiusalama katika baadhi ya maeneo lakini sehemu kubwa ya nchi yetu kuna amani.Uzoefu unatuonyesha kuwa mashirika yakifanya kazi kutoka ndani ya Somalia athari yake inakuwa kubwa nay a kuonekana kuliko yakifanyia kazi kutoka nje ya nchi.Naahidi kuwapatia chochote mnachotaka kutoka kwetu kitakachowawezesha kufanya kazi kutoka ndani ya Somalia"

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako