• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yatoa msaada wa chakula wa gharama ya Sh2.25 bilioni kukabiliana na njaa Kenya

    (GMT+08:00) 2017-03-28 08:59:43

    China imesaini makubaliano na Kenya ya kutoa msaada wa shilingi bilioni 2.25 za kupamba na ukame.

    Chini ya makubaliano hayo China itatoa tani 21,000 za mchele kwa Kenya ambazo zitawasaidia watu milioni 1.4 kwa mwezi.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    Makubaliano hayo yamesainiwa katika wizara ya fedha na waziri wa wizara hiyo Henry Rotich na Balozi wa China nchini Kenya Liu Xianfa.

    Akizungumza wakati wa hafla hiyo Balozi wa China nchini Kenya Liu Xianfa alisema China imeguswa sana na tatizo la ukame na njaa linaloathiri taifa la Kenya,na iko tayari kusaidia wakenya walioathirika na baa la njaa.

    "Kama marafiki wazuri na washirika ,China imeguswa sana na hali ya ukame nchini Kenya.Kwa miaka mitatu iliyopita nimejitahidi sana kupata msaada kutoka kwa serikali yangu na pia kuwahamasisha wachina wanaoishi Kenya kuwasaidia watu wa Kenya.Kutokana na ombi la serikali ya Kenya,serikali ya China ingependa kuwapatia watu wa Kenya msaada wa dharura wa chakula ili kukabiliana na baa la njaa.Tutatoa mchele tani 21,000 unaogharimu Sh2.25bn"

    Balozi Xianfa amesema chakula hicho kinaweza kulisha watu milioni 1.4 kwa mwezi kutoka sehemu mbalimbali zinazoathirika na ukame.

    Msaada huo wa chakula unatarajiwa kuwasili katika bandari ya Mombasa ndani ya mwezi mmoja.

    Aidha Xianfa amesema wiki ijayo atakuwa na hafla nyengine pamoja na jamii ya wachina wanaoishi Kenya kutangaza kiasi cha fedha ambazo jamii hiyo imechangisha.

    "Pia tutaihamasisha jamii ya wachina inayoishi hapa Kenya kutoa msaada wao wa chakula,maji na fedha.Wiki ijayo tutakuwa na shughuli katika ubalozi wa China na tutatangaza kiwango cha fedha ambacho jamii ya wachina imetoa"

    Waziri wa Fedha nchini Kenya Henry Rotich amesema China imekuwa mshirika mkuu wa Kenya katika masuala mbalimbali,na alielezea furaha yake ya kupata msada huo wa chakula kutoka kwa serikali ya China.

    Amesema msaada huo umekuja wakati muafaka.

    "Leo tumetia saini makubaliano ya msaada wa chakula kutoka China.Tumekumbwa na changamoto ya ukame hapa nchini.Rais Uhuru alitangaza changamoto hii kama janga la kitaifa.Ninaishukuru serikali ya China kwa kutupatia msaada huu,utasaidia pakubwa katika kupambana na janga la njaa"

    Kufuatia kiangazi cha muda mrefu,baa la njaa limeathiri watu kutoka sehemu mbalimbali.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako