• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kenya kuimarisha ushirikiano wa biashara na kimkakati na Ushelisheli

    (GMT+08:00) 2017-04-04 08:48:51

    Kenya na Ushelisheli zimesaini makubaliano ambayo yataimarisha nchi hizo mbili na kupanua ushirikiano baina yao katika biashara na usalama.

    Makubalioano hayo yalifikiwa wakati Rais Uhuru Kenyatta alipofanya mazungumzo na mgeni wake Rais Danny Faure wa Ushelisheli katika ikulu ya Nairobi jana.

    Rais wa Ushelisheli Danny Faure jana asubuhi aliwasili nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku tatu.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    Mkutano baina ya viongozi hao wawili ambao ulifanyika katika ikulu ya Nairobi,uliafikia makubaliano ambayo yatafanikisha kwa wakenya waliohitimu kutafuta ajira nchini Ushelisheli kwa sababu taifa hilo linahitaji mtaji wa rasilimali watu walio na taaluma kwa ajili ya uajiri katika sekta mbalimbali za uchumi wake.

    Aidha taifa la Kenya litaweza kuuza bidhaa nyingi za kilimo nchini Ushelisheli.

    "Tumezungumza kuhusu jinsi gani Ushelisheli inaweza kuisaidia Kenya katika kuinua uchumi wetu wa samawati na usalama wa baharini.Tumejadiliana na kukubaliana kuhusu vipi tunaweza kuimarisha ushirikiano wetu kuhusu Kenya kusafirisha maua na bidhaa za kilimo Ushelisheli,nyama,kuku na bidhaa za maziwa"

    Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wao jana,Rais Kenyatta na Rais Faure walitangaza kuwa Ushelisheli itaisaidia Kenya kuifanya bandari ya Mombasa kuwa na uwezo wa kuwa bandari ya usafirishaji wa samaki.

    Rais Faure alisema Ushelisheli iko tayari kufanya kazi na Kenya na kuisaidia kupanua sekta ya uvuvi.

    "Ushelisheli iko tayari kufanya kazi na wewe Rais Kenyatta na serikali yako kuweka mfumo mpya ambao tutawasaidia kukuza sekta yenu ya uvuvi na sekta ulinzi.Tumekubaliana kwamba kufikia mwezi Juni hadi Julai tuwe na tume ya pamoja baina ya nchi hizi mbili ambayo itaweka makataa ya kufikiwa kwa hatua hizi"

    Aidha alisema ushirikiano baina ya nchi hizi mbili unaweza kuimarishwa kupitia mipango mengine kama vile ubadilishanaji wa taarifa za ujasusi na mipango ya kujenga uwezo.

    Rais Faure alisema utalii ni kitega uchumi kikuu cha fedha za kigeni kwa Kenya na Ushelisheli,na nchi hizo mbili zote zina bidhaa sawa-utalii wa fukwe za bahari.

    Aidha alisema ni vyema kwa nchi hizo kushirikiana ,na nchi zote mbili zitanufaika kwa sababu kuna fursa nyingi za ushirikiano katika sekta hiyo.

    "Sasa tutaangalia ukuzaji wa vituo viwili vya utalii.Nyinyi mna utalii wa safari katika mbuga za wanyama na sisi tuna utalii wa fukwe za bahari,kwa hivyo tumekubaliana kwamba mashirika yetu yote ya mauzo na mawaziri watashirikiana katika kubadilisha maono haya kuwa kweli"

    Fursa hizo zitajumuisha ugawanaji wa njia bora,mafunzo,ubadilishanaji wa mipango ,mikakati ya pamoja ya mauzo na ufungaji wa pamoja wa sehemu za kuzuru.

    "

    Rais Kenyatta alisema pia wamezungumza kuhusu uwezo wa Kenya wa kusafirisha walimu kufunza nchini Ushelisheli.

    Aidha Rais Kenyatta alitoa shukrani kwa Rais Faure na serikali yake kwa kuimarisha usalama dhidi ya maharamia na katika kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevya.

    "Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais Faure kwa ushirikiano na umoja ambao maafisa wetu wa usalama wamepata katika vita dhidi ya uharamia ,ugaidi,na hasa katika vita dhidi ya madawa ya kelvya.Ni kweli kwamba ushirikiano ambao tumepata kutoka taifa la Ushelisheli tumefanikiwa kupata ushindi ambao tumeupata katika siku za nyuma .Nachukua fursa hii kumshukuru Rais Faure na serikali kwa msaada huo"

    Ziara hii ya Rais Danny Faure wa Ushelisheli nchini Kenya ni ya kihistoria.Kenya ni nchi ya kwanza ambayo Rais Faure amezuru tangu awe rais miezi sita iliyopita.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako