Serikali za Tanzania na Uganda zimesaini mikataba miwili kati ya sita ya ushirikiano wa maendeleo katika sekta ya nishati pamoja usafiri wa anga.
Mikataba hiyo imesainiwa mjini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Bw Sam Kutesa.
Mojawapo kati ya mkataba hiyo ni uendelezwaji wa mradi wa umeme wa megawati 14 eneo la Kikagati na Morongo ambao kila nchi itapata megawati saba.
Mkataba wa pili ni sekta ya usafiri wa anga ambapo ulisainiwa na Profesa Makame Mbarawa ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda Bibi Irene Muloni.
Akizungumzia makubaliano hayo, Balozi Mahiga amesema Tanzania na Uganda ni nchi marafiki na ndio maana wamekubaliana kusaini makubaliano mawili kati ya sita yaliyokuwa awali.
Ameongeza kuwa makubaliano mengine ambayo ni usafiri wa maji, reli, ushirikiano wa Jeshi la Polisi Tanzania na Uganda katika masuala ya usalama, sekta ya utangazaji na mengineyo yatasainiwa kwenye kikao cha wakuu wa nchi kitakachofanyika baadaye jijini Dar es Salaam.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |