• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mary Keitany avunja rikodi kwenye Marathon ya London

    (GMT+08:00) 2017-04-24 09:01:39
    Bingwa mara tatu wa Marathon ya New York Mary Keitany sasa amekuwa bingwa mara tatu wa Marathon ya London na mshika rekodi mpya ya dunia na Afrika ya mbio za kilomita 42 ya wanawake. Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 35 atatia kibindoni Sh27, 556,916 za Kenya kwa kuipiku rekodi ya Muingereza Paula Radcliffe ya saa 2:17:42 na kuweka mpya ya 2:17:01.

    Keitany, ambaye amechukua uongozi wa mapema wa msimu wa 11 wa Marathon Kuu Duniani (WMM), aliongoza mbio hizo za kilomita 42 kutoka mwanzo hadi utepeni. Wapinzani wa karibu wa mshindi huyu wa msimu wa tisa wa Marathon Kuu Duniani ni Waethiopia Tirunesh Dibaba na Aselefech Mergia. Mkenya Vivian Cheruiyot alimaliza marathon yake ya kwanza kabisa katika nafasi ya nne. Zawadi za wakimbiaji wa nne wa kwanza ni Sh5,687,000, Sh3,102,000, Sh2,326,500 na Sh1,551,000, za Kenya. Keitany, ambaye alishinda Marathon ya London mwaka 2011 na 2012, na mshika rekodi mpya ya kitaifa ya marathon ya Ethiopia, Tirunesh pia walizawadiwa Sh10, 340, 000 kwa kukimbia chini ya saa 2:18:00.

    Naye Daniel Wanjiru aliendeleza utawala wa Kenya katika Marathon ya London kwa kushinda taji la wanaume kwa saa 2:05:48. Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 24 alifuata nyayo za bingwa wa mwaka 2014 Wilson Kipsang' na mshindi wa mbio za 2015 na 2016 Eliud Kipchoge.

    Kwa upande wa Tanzania Alphonce Simbu, Jumapili hii amemaliza kama mshindi wa tano katika mbio hizo za Marathon ya London.

    Alphonce ambaye ni Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano maarufu ya Marathon ya Mumbai, amewapa wakati mgumu manguli wa riadha ulimwenguni walioshiriki mbio hizo za London akiwemo Muethiopia Kenenisa Bekela pamoja wa wengine kutoka Ethiopia na Kenya.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako