• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mradi wa Teens Watch unasaidia vijana kujikwamua kutoka kwa madawa Kenya

    (GMT+08:00) 2017-06-26 10:38:53

    Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya. Maudhui ya siku hii ni kuwasikiliza waathirika kama hatua ya kwanza kuwasaidia kuachana na matumizi ya mihadarati. Nchini Kenya mradi wa Teens Watch unawawezesha vijana waliokuwa wanatumia dawa hizo kupata ajira.

    Baada ya kila siku chache polisi wanakamata watu wakiwa kwenye biashara haramu ya mihadarati na pia waraibu wa madawa hatari ya kulevya kama vile cocaine, bangi na heroin.

    Hata hivyo wengi wa watumiaji ama wauzaji wa madawa haya mara nyingi wanaepuka mtego wa polisi na hivyo kuendelea na uraibu wao.

    Na athari zake zimejitokeza kwenye jamii.

    Lakini kitumbua hakijatumbukia nyongo kwa wote.

    Hapa ni katika eneo la Diani kaunti ya Kwale pwani ya Kenya na vijana 30 hivi wanajihusisha na usafi wa mazingira.

    Wanafanya kazi hii chini ya mradi wa Teens Watch ulioanzishwa ili kuwasaidia vijana walioathirika.

    Lakini hadithi yao ya kufanya usafi hapa ni ndefu.

    Walikuwa watumiaji wa madawa ya kulevya lakini sasa wanaishughulisha na kazi hii ili kujiepusha na utumiaji wa mihadarati.

    Mohammed Gonga ni mwenye tabasamu hasa akijua kama asingekuja hapa leo angekuwa mafichoni akitumia madawa, lakini angalau kazi hii inamsaidia kunusuru afya na maisha yake.

    "Nilianza mihadarati mwaka wa 2006 lakini sasa naona maisha imebadilika, hapo nyuma hatukuwa na ajira na watu walituchukia mitaani"

    Japeth Muema naye pia anasema licha ya kwamba hawalipwi pesa nyingi lakini manufaa ya kuwa hapa hayawezi kulinganishwa na chochote.

    Amekuwa kwenye lindi la madawa ya kulevya kwa zaidi ya miaka 10.

    "Huu mradi umetusaidia sana kama vijana, isipokuwa hauna pesa nyingi tunaomba serikali iongeze pesa kwenye mradi wetu ili tufaidike zaidi."

    Pamoja na juhudu izi za serikali ya Kaunti, bado vijana wengi wanasalia kukwama kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

    Chanzo kikuu kinatajwa kuwa ukosefu wa ajira na shinikizo kutoka kwa wale tayari wanatumia.

    Bwana Cosmos Maina ni mkurungezi wa mradi wa Teens Watch.

    "Sasa tuna vijana karibu 4,200 wanaotumia madawa na hao ni wengi sana. Lakini zaidi ya hapo tuna vijana zaidi ya 1,640 ambao wanatumia madawa ya kujidunga kwa sindano "

    Kwa jumla nchini Kenya eneo la pwani ndio lililoathirika sana na matumizi na biashara ya mihadarati.

    Hii ni kwa sababu Mombasa ambao ndio mji wa bandari pia unatumika kama mlango wa biashara hii haramu.

    Mohamed Gonga anasema, "Unga unapatikana kwa bei rahisi mtaani kwa sababu kuna maeneo kama matatu saa hii"

    Kila uchao wale wanaouza ama kutumia madawa wanatumia njia za siri kuepuka polisi.

    Pia kuna changamoto ya kuhusika kwa watu matajiri kwenye biashara hiyo ambao hutumia pesa zao kuhakikisha vijana wanaouza madawa hawakamatwi na polisi.

    Lakini Kamishena wa kaunti hii ya Kwale Kutswa Osaka anasema polisi nao wanakusanya taarifa kila siku ili kuwafuatiliwa wanaouza na kutumia madawa ili kukomesha kabisa biashara hiyo.

    "Kuna mbinu mpya ambayo sasa itatuelekeza kwa wale ambao wanauza hizo madawa "

    Mapema mwezi uliopita pia Naibu wa wa Rais William Ruto alitoa onyo kali kwa watu matajiri wanojihusisha na uuzaji wa madawa.

    "Hijalishi wako na uwezo gani wa kisiasa. Haiwezekani kwamba wewe ni kiongozi, mfanyabiashara wa kuuza madawa ya kulevya ili watoto wa wakenya wengine waharibike na watoto wako wanasoma"

    Na huku leo dunia ikiadhimisha siku ya kukabili matumizi ya madawa ya kulevya linasalia jukumu la kila mtu katika jamii kusaidia serikali kutatua tatizo hilo kama juhudu zinazofanywa na mradi wa Teens Watch.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako