• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Rais wa Kenya na mfanyabiashara mashuhuri wa China Jack Ma wajadili uwezeshaji kwa vijana

  (GMT+08:00) 2017-07-21 10:02:10

  Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amekutana na mfanyabiashara mashuhuri wa China Jack Ma jijini Nairobi, Kenya, ambapo wamejadiliana njia za kuwawezesha vijana kupitia ujasiriamali. Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Kenya imesema, mazungumzo kati ya rais Kenyatta na Jack Ma yalijikita zaidi kwenue njia za kuwawezesha vijana kupitia biashara na uvumbuzi.

  Ma amealikwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara UNCTAD na anatoa pia ushauri kwa vijana kuhusu njia za kufanikisha biashara zao. Hii ni ziara yake ya kwanza barani Afrika Jack Ma mfanya biashara tajiri zaidi barani Asia.Biashara yake ni kuwezesha watu kuuza bidhaa zao kupitia kwa mtandao wa Alibaba aliouanzisha miaka 18 iliopita.

  Kwanza akiwa mjini Nairobi anakutana na kundi la vijana wajasiriamali kutoa ushauri kwao kuhusu jinsi ya kustawisha biashara na kukabili changamoto.
  "Sijakuja hapa leo kuuza bidhaa za china kwa sababu mko nazo za kutosha, lakini nimekuja kuwashauri kuhusu njia za China za kufanya biashara. Kama mjasiriamali unaanza kwa kuwa na ndoto na kuamini ndoto yako pia unahitaji kuanza na watu wanaoamini ndoto yako . Kitu muhimu zaidi ni kuhakikisha ndoto zako zinafanikiwa kila wiki, kila mwezi na kuhakikisha waajiriwa wako pamoja na wateja wanafurahia. Wote hao wakifurahi pia nao wenye hisa watafurahia"

  Kwenye ziara hii amealikwa na shirika la Umoja wa Mataifa la biashara UNCTAD akiwa sasa pia ameteuliwa kuwa balozi wa heri njema na shirika hilo kupigia debe ujasiriamali miongoni mwa vijana.
  Dkt. Mukhisa Kituyi ni katibu mkuu wa Shirika la UNCTAD.
  "Hatma ya biashara kote ulimwenguni ni kutumia njia za mtandao na kwa hivyo lazima Afrika ijihusishe kama mataifa yake mengine, Na sio Afrika peke yake, lakini  usipoonekana kwa mtandao basi huwezi kuonekana kwa soko. Nimemleta Jack Ma kumuonyesha vile mazingira ya biashara ya mtandao yalivyo katika mataifa ya Afrika na pia kumhusisha na mjadala na vijana"

  Jack Ma anaandamana na mabilionea 38 kutoka China ambao pia wamekuja kutafuta nafasi za ushirikiano Barani Afrika. Anasema barani Afrika kuna fursa nyingi za kujiendeleza kibiashara hasa ikizingatiwa kwamba sasa kuna mtandao wa kasi ikilinganishwa na miaka 18 alipoanzisha kampuni yake.

  Aidha Jack Ma anatafuta ushirikiano zaidi kupitia kwa huduma zake za mtandaoni kama vile Taobao ambayo ni maarufu nchini China, na njia ya kulipia bidhaa ya Alipay.
  "Tumekuja kutafuta washirika na sidhani Alipay itakuwa biashara inayosimama kivyake hapa. Tunatafuta washirika ambao tutawawezesha kukua lakini sio kuja kuleta ushindani kwa biashara nyingine. Pia tungependa Taobao ije Afrika, lakini kwa maoni yangu naona kwamba ni vyema tuwe na Taobao ya Afrika ya kuuza bidhaa za Afrika nchini China na pia barani Asia"
  Jack Ma pia alikutana na wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi, ambapo aliahidi kwamba vijana mia tano wajasiramali watapata fursa ya kwenda katika makao makuu ya Alibaba mjini Hangzhou ili kujifunza vile biashara ya mtandaoni inavyofanyika.
  Na wanafunzi hapa wamependezwa na ushauri wake.
  Baadaye leo Jack Ma atahudhuria mkutano wa Youth Connekt Africa mjini Kigali Rwanda.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako