• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kenya na Tanzania zakubaliana kuondoa vikwazo vya biashara

    (GMT+08:00) 2017-07-25 09:14:23

    Kenya na Tanzania zimekubaliana kuondoa vikwazo vya biashara katika bidhaa mbalimbali kutoka nchi hizo kufuatia mazungumzo kati ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

    Mawaziri wa masuala ya kigeni wa nchi hizo mbili Balozi Amina Mohammed kutoka Kenya na Augustine Mahiga wa Tanzania walitoa tangazo hilo jijini Nairobi siku ya jumapili.

    Katika taarifa ya pamoja iliyosomwa na Waziri wa masuala ya kigeni wa Tanzania Augustine Mahiga,ni kwamba Kenya imekubali kuondoa vikwazo kwa unga wa ngano na gesi ya kupikia kutoka Tanzania.

    "Kufuatia majadiliano kati ya Rais wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli,marais hao wawili wamekubaliana kwamba jamhuri ya Kenya itaondoa marufuku ya unga wa ngano na gesi ya kupikia kutoka Tanzania kuanzia sasa"

    Kwa upande mwengine,Tanzania imekubali kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa maziwa,bidhaa za maziwa na sigara kutoka Kenya.

    Nchi mbili hizi jirani pia zimekubaliana kuondoa vikwazo vingine vyovyote vya biashara ambavyo vinaathiri bidhaa na huduma zinazobadilishwa kati ya nchi hizi mbili.

    "Jamhuri ya muungano wa Tanzania itaondoa vikwazo vya kibiashara kwa maziwa,bidhaa za maziwa na sigara zinazotengenezwa Kenya kuanzia sasa.Nchi hizi mbili pia zitaondoa vikwazo vingine vyovyote ambavyo vinaathiri bidhaa na huduma zinazobadilishwa kati ya nchi hizi mbili.Marais hao wawili walitupatia jukumu sisi mawaziri wa masuala ya kigeni wan chi hizi mbili kutangaza uamuzi wao huu wa ngazi za juu"

    Hata hivyo wakenya bado watahitajika kupata visa wanaposafiri Tanzania kwa biashara,jambo ambalo Mahiga amesema linashughulikiwa.

    Mahiga alisema iwapo kutakuwa na matatizo yoyote,wako tayari kuyashughulikia ili raia wa nchi zote mbili waweze kusafiri kwa urahisi.

    Alisema nchi hizi mbili bado zitaendelea kulinda sehemu za mipaka kwa pamoja wakati utengenezaji wa cheti cha kusafiria cha Jumuiya ya Afrika (EAC) kitasaidia kurahisisha utembeaji katika nchi za Jumuiya Afrika Mashariki.

    Waziri wa masuala ya kigeni wa Kenya Balozi Amina Mohammed alisema nchi hizi mbili zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja ya kiufundi.

    "Tutaunda kamati ya pamoja ya kiufundi ambayo itaongozwa na wizara zetu mbili.Kamati hiyo itajumuisha wizara ya biashara,fedha,usalama,nishati,usafiri,jumuiya ya afrika mashariki,na utalii.Pia tutajumuisha mashirika mengine ya serikali iwapo itahitajika"

    Amina amesema sababu ya kuunda kamati hii ya pamoja ni kushughulikia masuala yoyote ambayo yataibuka baina ya nchi hizi mbili.

    "Lengo la kuunda kamati hii ya pamoja ya kiufundi ni kuweza kushughulikia masuala yoyote ambayo yataibuka kati ya nchi zetu mbili.Tumeelewana kwamba hatutakubali mtu yoyote au jambo lolote kuharibu uhusiano kati ya nchi zetu mbili"

    Mwezi Aprili mwaka huu Kenya ilipiga marufuku uagizaji wa gesi ya kupikia kutoka Tanzania,huku wizara ya nishati wakati huo,ikisema kuwa hatua hiyo ililenga kuzuia kuenea kwa viwanda vinavyojaza gesi kinyume cha sheria.

    Makampuni ya gesi kutoka Tanzania husafirisha Kenya takriban tani 40,000 za gesi ya kupikia kila mwaka.

    Tanzania ni nchi pekee katika ukanda huu ambayo imewekeza mitambo ya kupokea gesi na kuiweka kwenye mitungi.

    Aidha gesi inayotoka Tanzania huwa na gharama nafuu nchini Kenya kuliko gesi inayoagizwa kupitia bandari ya Mombasa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako