• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Kenyatta awahimiza wakenya kufanya kazi ili waendeleze taifa

    (GMT+08:00) 2017-08-15 08:57:30

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa wakenya kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza taifa.

    Rais Kenyatta ametoa tamko hilo baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwaambia wafuasi wake wasusie kazi jana,kama njia mojawapo ya kuonyesha kutoridhika na matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8 ambao Kenyatta alitangazwa mshindi.

    Mwanahabari wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    Rais Kenyatta alifanya vikao afisini mwake jana na idara mbalimbali za serikali,baada ya tume huru ya uchaguzi na mipaka,IEBC,kumtangaza mshindi katika uchaguzi wa Agosti 8.

    Rais Kenyatta alikutana na wakuu wa vyombo vya usalama katika afisi yake ya jumba la Harambee jijini Nairobi ili kutathmini hali ya usalama nchini.

    "Tumeripoti kazini,na leo tulikuwa tunatathmini hali ya usalama nchini.Tunashukuru sana kuona wakenya wengi ambao wamekubali matokeo,na wengi wamerudi kazini,tunahimiza hilo.Tunawashukuru wakenya kwa kudumisha amani wakati wa uchaguzi,na nazidi kutoa wito kwa wale ambao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi wasipigane,haifai kuharibu mali ya wengine,na haifai kutoa wengine uhai"

    Aidha Kenyatta aliwapongeza maafisa wa polisi kwa kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu,lakini aliwahimiza kutotumia nguvu wakati wanapokabiliana na waandamanaji.

    "Tunawashukuru maafisa wa polisi kwa kazi nzuri lakini tunazidi kuwahimiza kutotumia nguvu wakati wanapotekeleza majukumu yao"

    Katika kikao na wanahabari ,Rais Kenyatta aliwashukuru mamilioni ya wakenya ambao wamerejea kazini ,akisema kuwa kufanya kazi kunahitajika katika kuboresha uchumi wa nchi.

    Rais Kenyatta amewataka ambao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi kufuata kanuni za kisheria kwa kwenda mahakamani lakini sio kuwachochea wananchi.

    "Wale marafiki zetu ambao bado hawataki kukubali matokeo ya uchaguzi tunawaambia kwamba tumewanyooshea mkono wa amani na urafiki.Pia tunawaambia watumie njia za kisheria katika katiba yetu kueleza kutoridhishwa kwao,lakini naamini kuwa hakuna mkenya hata mmoja ambaye anataka kuendelea kuona ghasia,uporaji,na maandamano ambayo yanaharibu mali za wengine"

    Rais Kenyatta alisema wakenya hawafai kupigana kutokana na matokeo ya uchaguzi,na kuongeza kuwa maafisa wa polisi wako tayari kuwezesha maandamano ya amani kwa wale wasiokubaliana na matokeo ya uchaguzi wa urais.

    "Vyombo vya usalama viko tayari ,semeni tu mnataka kufanya maandamano sehemu Fulani na wakati Fulani,pangeni na polisi,hamhitaji ruhusa yangu au chama cha jubilee.Iko katika sharia,fanyeni maandamano ya amani.Msiingilie maisha ya wakenya wengine,hiyo inaruhusiwa.Lakini kama serikali hatutaruhusu watu kupoteza maisha,uharibifu wa mali na uporaji"

    Alisisitiza kwamba wakenya wote wana haki ya kikatiba kufanya maandamano ya amani lakini serikali haitaruhusu ujambazi na uharibifu wa mali.

    Rais Kenyatta ataapishwa tarehe 29 Agosti kwa muhula wake wa pili wa miaka mitano kama rais wa Kenya iwapo hakutakuwa na kesi yoyote mahakamani kupinga ushindi wake.

    Iwapo kutawasilishwa kesi mahakamani,basi Rais ataapishwa tarehe 12 Septemba.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako