• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kilimo cha GMO Tanzania kuanza na mazao manne

    (GMT+08:00) 2017-08-25 19:09:45

    Serikali ya Tanzania imependekeza teknolojia ya uhandisi jeni nchini humo ianze kwenye mazao manne ambapo zao la kwanza ni mahindi yanayostahimili ukame ambayo yanaendelea kufanyiwa utafiti katika kituo cha utafiti mkoani Dodoma. Akizungumza na waandishi wa habari, mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia nchini humo (OFAB) kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Bw. Nicholus Nyange amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi duniani kote, watafiti mbalimbali wa kilimo wamekuwa wakitafuta njia ambazo zitawezesha kupata mavuno kwa wingi kwa maana ya kuwa na uwezo wa kustahimili magonjwa na wadudu waharibifu.

    Amesema njia hizo pia zitawezesha kupata virutubisho kwa wingi kama kwenye mchele, muhogo na mtama wenye vitamin A pamoja na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuvumilia ukame, tindikali na hali ya chumvi.

    Mabadiliko hayo ya tabianchi yamefanya wataalamu kuanza michakato ya kuendeleza mazao yaliyofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki (GMO), ambayo yameleta mafanikio katika baadhi ya nchi ikiwemo Afrika Kusini kwenye kilimo cha mahindi na Burkina Faso kwenye zao la pamba.

    Jaribio la kupanda mahindi hayo nchini Tanzania lilifanyika Oktoba 5, mwaka jana.

    Ukaguzi wa jaribio hilo ulifanyika Novemba 22 mwaka jana, na uvunaji ulikuwa Februari 14 mwaka huu. Kwa sasa kinachosubiriwa ni kibali kutoka serikalini ili hatua nyingine ya utafiti huo iendelee.

    Zao la pili litakalofanyiwa teknolojia ya uhandisi jeni ni muhogo ambalo limekuwa likishambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia. Hivi sasa kuna aina mbalimbali ya mbegu za muhogo zinaboreshwa kwa njia ya uhandisi jeni katika maabara ya Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni (MARI) kilichopo Dar es Salaam.

    Wachanganuzi wa mambo ya kilimo wanaona hatua kama hizi zitafanikisha juhudi za kuhakikisha kuna usalama wa chakula na vile vile kupiga jeki biashara kati ya nchi za Afrika hususan jumuiya ya Afrika mashariki.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako