• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Uamuzi wa kesi ya uchaguzi wa urais inayopinga ushindi wa Uhuru Kenyatta kutolewa Ijumaa

  (GMT+08:00) 2017-08-30 19:16:02

  Baada ya vikao vya siku nne vya kusikilizwa kwa kesi ya kukataa kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta kuwa rais mteule, majaji wa mahakama ya upeo wanatarajiwa kutoa uamuzi wao siku ya Ijumaa, wiki hii. Haya yanajiri baada ya kinara mkuu wa upinzani Raila Odinga kuelekea kwenye mahakama ya upeo juma lililopita kupinga uchaguzi wa Uhuru Kenyatta, na kusema kuwa uchaguzi ulikumbwa na hitilafu. Wakati huo huo, mawakili wa Uhuru Kenyatta wanasema kwamba mteja wao alishinda uchaguzi huo kwa njia ya wazi.

  " Jaji mkuu, swala linguine ambalo ningependa kugusia ni kuhusu sababu kuu ambayo inaweza ipa mahakama haya mamlaka ya kufutilia mbali uchaguzi mkuu. Ni kosa la nani au utepetevu upi unaweza kusababisha mahakama ya upeo kuamuru uchaguzi mkuu kurejelewa ? Mkuu wangu, jibu la maswali haya litawashangaza wengi. Nitakwambia hivi, kati ya kesi asilimia 99, unaweza kufutilia mbali uchaguzi wa urais endapo kulikuwa na dosari au haki za mpiga kura zilihujumiwa wakati wa kupiga kura pekee ! Kulingana na kipengele cha kwanza cha 38 cha katiba kuhusu uchaguzi, hujuma kwa mpiga kura au kudhulumiwa kwa haki za mpiga kura ndio sababu kuu ya kipekee inayoweza kusababisha uchaguzi wa urais kurudiwa upya….'

  Ni maneno yake wakili mkuu Ahmednasir Abdullahi, anayeongoza jopo la mawakili wanaomwakilisha Rais Uhur Kenyatta kwenye kesi inayopinga ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi uliopita. Kulingana na Ahmednasir, mteja wake ambaye ni Bw Kenyatta alishinda uchaguzi huu kwa njia ya wazi na huru, huku akiyataja madai ya mlalamishi mkuu Raila Odinga ya kuibiwa kura kuwa hayana uzito wowote. Juma lililopita, kinara mkuu wa upinzani Raila Odinga alipeleka kesi mahakamani ya kupinga uchaguzi wa Uhuru Kenyatta kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa urais.

  Mawakili wa Uhuru Kenyatta walisema kuwa mteja wao alipata kura zaidi ya milioni nane dhidi ya milioni 6.7 za Bwana Odinga na hivyo basi hakuna sababu yeyote ya kupinga uchaguzi huu kwa sababu ya tofauti ya kura milioni 1.4 kati yao.

  Na baada ya vikao vya siku nne, majaji wa mahakama ya upeo wako faraghani kuandaa uamuzi ambao utatolewa siku ya Ijumaa, wiki hii. Hata hivyo huenda majaji hawa wakawa na wakati mgumu kutathmini na kuamua jinsi ushahidi wa kompyuta kuu ya kuyapokea na kuyatangaza matokeao ya urais ya IEBC almaarufu server,utakavyotumika katika kuamua kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta Agosti nane. Siku ya mwisho ya vikao vya kusikilizwa kwa kesi hii, mawakili wa upinzani wakiongozwa na wakili James Orengo walisema kuwa IEBC haikuwapa ruhusa ya kuangalia mtambo wa kompyuta hiyo kuu kama ilivyoagiza mahakama. Swala hili lilipingwa vikali na mawakili wa tume huru ya uchaguzi ya IEBC Paul Muite na wa Uhuru Kenyatta Paul Ngatia. Huyu hapa ni James Orengo, wakili wake Raila Odinga.

  'Kile ambacho utaona kwenye ripoti yetu, kile ambacho tuliweza kupata ni kwamba, mkuu wangu , hata akaunti ya mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi IEBC, iltumika kufuta baadhi ya taarifa kwenye kompyuta. Hilo ndilo wataalamu wetu waliona walipopewa fursa ya kupitia taarifa za kompyuta kuu.

  Wakili Paul Ngatia anayemwakilisha Uhuru Kenyatta alikana madai hayo.

  'Kuna taarifa kwamba stakabadhi ambazo zilipeanwa hazikuwa zimeithibitishwa. Huo ni uongo bwana jaji mkuu kwa sababu vyeti vilitolewa.

  Kilichosalia sasa ni uamuzi wa majaji wa mahakama ya upeo wakiongozwa na jaji mkuu David Maraga siku ya Ijumaa, wiki hii.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako