• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kongamano la viwanda na biashara la BRICS lafunguliwa China

    (GMT+08:00) 2017-09-03 17:46:20

    Kongamano la viwanda na biashara la nchi za BRICS limefunguliwa leo alasiri mjini Xiamen, China. Rais Xi Jinping wa China amehudhuria na kuhutubia ufunguzi wa kongamano hilo.

    Hili ni kongamano kubwa zaidi tangu mfumo wa BRICS uanzishwe miaka 10 iliyopita, na kuwashirikisha wajumbe zaidi ya 1,000 kutoka sekta za viwanda na biashara, wakiwemo wakuu wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa, na Benki mpya ya Uendelezaji ya Nchi za BRICS.

    Kwenye hotuba yake, rais Xi Jinping amekumbusha historia ya mfumo wa BRICS, na kujumuisha uzoefu wa ushirikiano kati ya nchi wanachama wake, na kutupia macho mustakabali wa mfumo huo. amesema, hivi leo baadhi ya watu wanaona uchumi wa nchi za BRICS hautaweza kuibuka tena duniani baada ya kupungua kwa kasi ya ongezeo la uchumi wa nchi hizo. Anakubali nchi za BRICS zinakabiliwa na changamoto kiuchumi kutokana na hali ya kutatanisha ya ndani na duniani, lakini ana imani kuwa mwelekeo na uwezo wao wa kujiendeleza siku hadi siku haujabadilika.

    Amezitaka nchi za BRICS kuenzi mawazo endelevu ya pamoja na ya jumla ambayo yanazingatia ushirikiano kuhusu hali ya usalama, kujiunga na kuchangia utatuzi wa masuala muhimu ya kikanda kwa msimamo wa kiujenzi. Ametoa ufafanuzi kwamba, nchi hizo ni walinzi wa amani ya dunia, na wajenzi wa utaratibu wa usalama wa kimataifa. Hivyo zinatakiwa kulinda kanuni za katiba ya Umoja wa Mataifa, sheria ya kimsingi kuhusu uhusiano wa kimataifa, na ushirikiano kati ya nchi nyingi katika utatuzi wa masuala ya kikanda na kimataifa, na kuhimiza uhusiano wa kimataifa uwe wa kidemokrasia, kupinga vitendo vya umwamba na siasa kali katika mambo ya kimataifa.

    Aidha amesema tunapaswa kupanua wigo wa ushirikiano wa BRICS ili nchi nyingi zaidi zinufaike, kwa kupitia kuanzisha mtandao wa kiwenzi, nchi nyingine zinazoendelea na zile zinazoibuka kiuchumi zinaweza kujiunga na shughuli zetu za kunufaishana zenye ushirikiano na mshikamano, ili kupata mafanikio ya pamoja.

    Mwisho rais Xi Jinping amesema ushirikiano kati ya nchi za BRICS utaingia mwongo wa pili ambao utakuwa na mafanikio makubwa zaidi, tutashirikiana na jumuiya ya kimataifa, ili mafanikio ya ushirikiano wetu uwanufaishe watu wa nchi tano wanachama wa BRICS, na hali ya amani na maendeleo ya dunia kuwanufaisha watu wa nchi zote duniani.

    Habari zinasema kongamano hilo litajadili hasa masuala manne ya biashara na uwekezaji, ushirikiano wa kifedha na maendeleo, kuunganisha miundo mbinu, na uchumi wa bahari.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako