• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mji wa Zhoushan wazingatia uhifadhi wa mazingira wakati unapoendeleza uvuvi

  (GMT+08:00) 2017-09-25 18:53:19

  Visiwa Zhoushan kwenye bahari ya Donghai viko kusini mashariki mwa China, ni eneo kubwa zaidi la uvuvi nchini China, na nguzo ya uchumi wa mji wa Zhoushan ni shughuli za uvuvi na utengenezaji wa samaki. Naibu mkurugenzi wa idara ya bahari na shughuli za uvuvi ya Zhoushan Bw. Liu Shunbin, amesema mji huo unatilia maanani sana maendeleo ya uvuvi, kwani kati ya wakazi wake milioni moja, laki nne wanafanya kazi zinazohusiana na uvuvi.

  Bw. Liu amesema maendeleo endelevu ya shughuli za uvuvi yanategemea juhudi za kuhifadhi mazingira, zamani watu wa Zhoushan walifanya makosa yaliyosababisha hasara kubwa. Anasema,

  "Watu walidhani raslimali baharini zinamilikiwa na kila mtu, hivyo watu wote walikwenda kuvua. Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana na uvuvi wa kupita kiasi, shughuli hizo zilididimia, na hata baadhi ya watu walisema samaki wamekwisha kabisa kwenye bahari ya Donghai."

  Ili kukabiliana na changamoto hii, baadhi ya wavuvi walipendekeza samaki wadogo wasivuliwe. Pendekezo ambalo lilizingatiwa na wizara ya kilimo ya China, na ikaamua kuanzisha utaratibu wa kupiga marufuku kuvua samaki wakati wa majira ya joto. Utaratibu huo ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 1995 katika bahari za Donghai na Huanghai, baadaye ulitekelezwa katika bahari zote nchini China.

  Hata hivyo kitendo cha kuvua samaki kupita kiasi bado ni changamoto inayoukabili mji wa Zhoushan, mji huo unatakiwa kutafuta uwiano wa mahitaji ya uvuvi na kufufuka kwa mazingira ya bahari. Bw. Liu amesema hali hii imeulazimisha mji huo kujenga mfumo wa huduma unaolingana na maendeleo ya shughuli za uvuvi zisizoleta uharibifu wa mazingira. Anasema,

  "Kuwapa wavuvi haki ya kumiliki raslimali baharini, na kuwafanya watumiaji hao wa raslimali pia wawe wasimamizi. Huu ni uvumbuzi wa njia ya usimamizi, baadaye gharama za kusimamia shughuli za uvuvi zitapungua huku juhudi za kuhifadhi rasilimali zikifanywa."

  Hivi sasa mji wa Zhoushan unaunda muundo wa shughuli za uvuvi zisizoleta uharibifu wa mazingira, haswa kwa njia za kuvua samaki. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kujenga maeneo ya uvuvi pamoja na ufugaji wa samaki, kupiga marufuku matumizi ya nyavu kuvua samaki wadogo. Takwimu zilizotolewa mwishoni mwa mwaka jana zinaonesha kuwa, raslimali za samaki mjini Zhoushan zinafufuka.

  Mwezi Septemba mwaka 2017, kituo cha kitaifa cha majaribio ya uvuvi usioleta uharibifu wa mazingira mjini Zhoushan kilizinduliwa, na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya shughuli za uvuvi mjini huo. Bw. Liu anasema,

  "Baadaye kwenye eneo la uvuvi la Zhoushan, wavuvi watazingatia uwiano wa viumbe, na kutumia raslimali baharini kwa mtazamo endelevu, aidha shughuli za ufugaji samaki zitastawi."

  Hivi sasa mbinu za teknolojia ya mtandao wa Internet pia zimetumiwa katika shughuli za uvuvi, kwa mfano mfumo wa udadisi wa sehemu zilizojaa bidhaa za uvuvi kwenye mtandao wa Internet, uendeshaji wa kielektroniki wa meli za uvuvi na uchukuzi wa samaki, na njia za kisasa za kuboresha mazingira ya bahari.

  Ili kuhifadhi raslimali za uvuvi, mwaka 2016 mji wa Zhoushan ulianza kutekeleza sheria ya kuhifadhi mazingira ya bahari ya kupiga marufuku kuvua samaki kwa ndoano bila ruhusa. Bw. Liu amesema hii ni sheria ya kwanza ya aina hiyo nchini China.

  Mbali na serikali, mjini Zhoushan kuna mashirikisho mengi yasiyo ya kiserikali yanayotangaza ustaarabu wa kuhifadhi uwiano wa viumbe baharini kwa hiari, na pia yametoa mchango muhimu katika juhudi za kuhifadhi mazingira baharini.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako