• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Watu 40 wafariki kutokana na mlipuko wa Malaria Kenya

  (GMT+08:00) 2017-10-09 08:33:52

  Takriban watu 40,miongoni mwao watoto wanne kutoka kaunti 5 nchini Kenya wamethibitishwa kufariki kutokana na Ugonjwa wa malaria.

  Kulingana na Wizara ya Afya nchini Kenya,visa 733 vya malaria vimeripotiwa katika kaunti za Marsabit,Lamu,Turkana,Baringo ,Pokot magharibi na katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma ambapo watu 438 wameripotiwa kuwa na ishara za ugonjwa wa malaria.

  Mwanahabari wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

  Watu wengine 295 wanaripotiwa kupata matibabu katika hospitali mbalimbali nchini,wakati ambapo serikali ikipiga hatua za kuidhibiti hali hiyo kwa kusambaza madawa na vifaa vya kupima malaria katika kaunti zilizoathirika.

  Kaunti iliyo na idadi kubwa ya watu walioathirika na malaria ni Marsabit ambayo imesajili vifo 26.

  Serikali kuu kwa ushirikiano na serikali za kaunti na mashirika yasiyo ya serikali wako mbioni kupambana na ugonjwa huo kwa kusambaza madawa na vifaa sehemu za mashinani.

  Huku idadi ya wanaoathirika ikiongezeka siku hadi siku,Wizara ya Afya jumamosi ilisambaza vifaa vya kupima malaria 4,000 na madawa ya kukinga malaria 24,000 kwa kaunti zilizoathirika.

  Munim Duba kutoka kaunti ya Marsabit ni mmoja wa waathiriwa wa malaria.Anasema yeye pamoja na watoto wake wameathirika na malaria.

  Kulingana na Mkurugenzi wa Mpango wa kukabiliana na malaria katika wizara ya afya kaunti ya Marsabit Daqo Gulacha kuna idadi kubwa ya watu wanaugua malaria katika kaunti hiyo.

  "Sehemu hizi malaria imeenea sana,hadi kufikia hatua kwamba kinga dhidi ya magonjwa ya wanajamii wa maeneo haya iko chini,na malaria inawaathiri pakubwa"

  Aidha Gulacha anasema idadi hiyo kubwa imechangiwa na mgomo wa wauguzi kwa sababu sio watu wengi wanapata huduma wanapokwenda katika zahanati.

  "Kuenea kwa visa vya ugonjwa wa malaria pia kumechangiwa na mgomo wa wauguzi:tuna zahanati mbili tu eneo hili ambazo zinafanya kazi"

  Wakati haya yakijiri ,timu ya wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa matibabu nchini Kenya (Kemri) alhamisi iliyopita ilitumwa kuchukua sampuli za damu za wagonjwa baada ya kugundulika kuwa baadhi ya wagonjwa waliotibiwa Marsabit walionyesha dalili sawa na za malaria ya ubongo.

  Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari,Mkurugenzi wa Kemri Yeri Kombe amesema timu inayojumuisha wanasayansi bingwa itasafiri katika shemu zilizoathirika na malaria wikiendi na kufikia leo jumatatu wataweza kusema haswa shida ni nini.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako