• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Uchaguzi wa urais Kenya wafanyika huku kukiwa na maandamano ya upinzani

  (GMT+08:00) 2017-10-26 19:25:19

  Kenya leo imeandaa uchaguzi mpya wa urais ambao umesusiwa na upinzani.

  Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakifanya maandamano kupinga uchaguzi huo huku polisi wakiimarisha doria katika maeneo mengi nchini humo.

  Rais Uhuru Kenyatta amewataka wakenya kudumisha amani wakati na baada ya zoezi hilo.

  Mwandishi wetu Tom Wanjala anaripoti kutoka Nairobi.

  Hapa ni katika eneo la katikati ya mji wa Nairobi, siku ya kupiga kura nchini Kenya.

  Maduka mengi yamesalia kufungwa, na barabara nyingi hazina msongamano wa magari.

  Vituo vya kupigia kura nchini Kenya vilifunguliwa alfajiri saa kumi na mbili Alhamisi.

  Lakini sio kwenye vituo vyote ambako wapiga kura walijitokeza hasa kwenye maeneo kwenye wafuasi wengi wa muungano NASA.

  Muungano huo tayari ulikuwa umetangaza kwamba hautashiriki kwenye zoezi hilo la marudio ya kura ya urais wakilalamikia kutokuwepo na mageuzi kwenye tume huru ya uchaguzi IEBC.

  Wale waliojitokeza kupiga kura walikuwa na haya ya kusema.

  "Imekuwa mzuri sana leo. Hatujapoteza muda. Hii tunajua Uhuru ameshaingia na atukumbuke pia sisi maskiniā€¦..nimetoka Kiambu kaunti,sijaona vita yoyote nilikotoka. Nimeona tu amani."

  Na afisa wa tume ya uchaguzi kwenye mojawepo wa vituo anasema upigaji kura umeendelea kwa njia ya amani.

  "Turn up ya leo si mbaya. Watu ni wachache. Sio kama wakati huo mwingine."

  Kumekuwa na maandamano katika miji ya migori, eneo la kibera mjini Nairobi, Homabay na mjini Kisumu wafuasi wa upinzani wakipambana na polisi wa kutuliza ghasia.

  Wanaoandamana wamefunga barabara na hivyo kutatiza shughuli yoyote ile ya upigaji kura.

  Ijapokuwa wanasusia kura wafuasi wa upinzani wanashinikiza kuwepo kwa mageuzi.

  "Baba akisema tuandamane, tutaandamana. Baba akisema, lazima tufuate sheria. Hata hakuna mpango wa kupiga kura. Sijapiga kura kwa sababu hakuna demokrasia. Lazima IEBC isafishwe"

  Jumatano mahakama nchini Kenya ilitoa uamuzi kwamba uchaguzi unafaa kuendelea hata kama mgombea mmoja amejiondoa.

  Uamuzi ambao unakaribishwa na rais Uhuru Kenyatta anayeongoza chama cha Jubilee.

  Leo akipiga kura katika eneo bunge la Gatundu kusini, Kenyatta anawaomba wakenya kudumisha amani wakati na baada ya uchaguzi.

  "Hakikisho langu kwa wakenya ni kwamba tutalinda usalama. Nimesikia kwamba kuna baadhi ya maafisa wa tume ya uchaguzi ambao wametolewa vitisho, lakini nataka kusema asilimia 90 ya nchi iko tulivu. Nadhani uchaguzi ni fursa kwa watu kuchagua kiongozi wao, kama ilivyoagizwa na mahakama ya upeo. wanaotaka kupiga kura wafanye hivyo na wale wasiotaka ni haki yao ya kidemokrasia kutopiga kura. Ningependa kusema kwamba demokrasia yetu sasa imekomaa. Uchaguzi unawezwa kufutwa na tunafuata agizo la mahakama, taasisi zetu zimekomaa na naona hiyo ndio njia ya kufuatwa na bara la Afrika"

  Katika ukumbi wa Bomas, kituo kikuu cha kujumuisha kura, usalama umeimarishwa huu polisi wakikagua magari na watu wote wanaoingia.

  Ni hapa ambapo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati anatarajiwa kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi wa leo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako