• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Rais Xi Jinping kufanya ziara yake ya kwanza katika nchi za nje baada ya mkutano mkuu wa 19 wa CPC

  (GMT+08:00) 2017-11-03 17:28:29

  Wizara ya mambo ya nje ya China leo imetangaza kuwa, rais Xi Jinping wa China ambaye pia ni katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China CPC, atafanya ziara rasmi nchini Vietnam na Laos kuanzia tarehe 10 mwezi huu, na pia atahudhuria mkutano usio rasmi wa 25 wa wakuu wa Shirika la Ushirikiano wa Uchumi katika Asia na Pasifiki APEC utakaofanyika mjini Da Nang, Vietnam. Hii ni mara yake ya kwanza kufanya ziara katika nchi za nje baada ya mkutano mkuu wa 19 wa CPC, na pia ni ufunguzi wa kazi za diplomasia za China katika kipindi kipya.

  Mji wa Da Nang, Vietnam utakuwa kituo cha kwanza cha ziara ya rais Xi, ambapo atahudhuria mkutano usio rasmi wa 25 wa wakuu wa APEC. Hivi leo uchumi wa dunia kwa jumla unafufuka, lakini bado unakabiliwa na changamoto. Jumuiya ya kimataifa inatumai China ambayo imeingia katika kipindi kipya baada ya mkutano mkuu wa 19 wa CPC kutoa mchango zaidi kwa ajili ya kusukuma mbele muungano wa uchumi wa kikanda na kuhimiza maendeleo mfululizo ya uchumi wa dunia. Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Baodong ameeleza matumaini matatu ya China kuhusu mkutano huo,

  "Kwanza ni kulinda kwa pamoja mwelekeo wa ufunguaji mlango na maendeleo ya sehemu ya Asia na Pasifiki. China inatumai kuwa pande zinazohusika zitashirikiana katika kusukuma mbele ujenzi wa eneo la biashara huria la Asia na Pasifiki, kwa kurahisisha biashara na shughuli za uwekezaji, na kuzifanya ziwe huria zaidi. Pili ni kutafuta kwa pamoja uwezo na injini mpya za maendeleo ya sehemu hiyo. Tunatumai mkutano huo utatoa mpango na hatua mpya katika sekta za mtandao wa internet, uchumi wa kielektroniki, biashara za internet, shughuli za huduma na mashirika madogo na ya katikati, ili kuhimiza uchumi wa nchi wanachama wa APEC kupata maendeleo mfululizo kwa utulivu. Tatu ni kupanga mustakabali mpya wa ushirikiano katika siku zijazo. China itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wengine wa APEC, kusukuma mbele maendeleo ya ushirikiano wa uchumi, na kuhimiza maendeleo na ustawi wa sehemu ya Asia na Pasifiki na dunia nzima."

  Habari zinasema rais Xi atafanya shughuli nyingi katika ziara hiyo, zikiwemo kuhudhuria na kuhutubia mkutano wa kilele wa wakuu wa viwanda na biashara wa APEC, kuzungumza na wajumbe wa kamati ya ushauri wa mambo ya viwanda na biashara ya APEC, kuhudhuria duru mbili za mkutano wa APEC, kuhudhuria mkutano wa tafrija ya kikazi, na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Asia ya Kusini Mashariki. Kuhusu mikutano na viongozi wa Japan na Korea ya Kusini itafanyika au la, Bw. Li anasema,

  "Hadi sasa nchi nyingi zikiwemo Japan na Korea ya Kusini zimetoa ombi la kufanya mkutano kati ya viongozi wao na wa China. Bado tunafanya mawasiliano na majadiliano."

  Baada ya mkutano wa siku mbili wa APEC, rais Xi atafanya ziara rasmi nchini Vietnam na Laos, ambazo ni nchi jirani na wenzi muhimu wa China. Baada ya mkutano mkuu wa 19 wa CPC, ziara rasmi ya kwanza ya rais Xi itafanyika katika nchi hizo mbili, ambazo zote ni nchi za kijamaa zinazotawaliwa na Chama cha Kikomunisti kama China. Hali ambayo inaonesha kuwa China inatilia maanani sana uhusiano kati yake na nchi hizo mbili. Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Chen Xiaodong anasema,

  "Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa serikali na chama tawala cha China kufanya ziara katika nchi za nje baada ya mkutano mkuu wa 19 wa CPC, pia ni ufunguzi wa kazi za kidiplomasia zenye umaalumu wa China katika nchi jirani kwenye kipindi kipya."

  Habari zinasema rais Xi atakapofanya ziara nchini Vietnam, atabadilishana maoni na viongozi wa chama tawala na serikali ya nchi hiyo, kuhusu namna ya kukuza mawasiliano ya kimkakati, na kupanua ushirikiano halisi na mawasiliano ya utamaduni, na masuala ya kikanda na kimataifa yanayofuatiliwa na nchi hizo mbili, ili kupanga mwelekeo wa uhusiano kati yao katika kipindi kipya. Nchini Laos, viongozi wa nchi hizo mbili watazungumza kwa kina kuhusu kueneza urafiki wa jadi, kuimarisha uaminifu wa kisiasa, na kuongeza mawasiliano ya kimkakati na ushirikiano halisi, ili kupanga maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika kipindi kipya kwa pande zote.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako