• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tanzania:Magufuli aagiza kuvunjwa kwa jengo la Umeme

    (GMT+08:00) 2017-11-16 19:10:29

    Rais John Magufuli ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuvunja sehemu ya Jengo la Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na la Wizara ya Maji na Umwagiliaji yaliyopo katika hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja la ghorofa tatu la Ubungo (Ubungo Interchange) jijini Dar es Salaam.

    Rais Magufuli ametoa agizo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la juu la Tazara (Tazara Fly-Over) na Ubungo Interchange .

    Rais Magufuli amemuagiza Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Ndyamukama Julius kuvunja sehemu ya jengo la Tanesco na la Wizara ya Maji na Umwagiliaji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.

    Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Tanroads kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 16 kutoka eneo linapoishia daraja la ghorofa tatu katika eneo la Ubungo kwenda Chalinze ili itanuliwe kwa lengo la kurahisisha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.

    Rais Magufuli amewataka makandarasi wanaojenga daraja la Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi wa madaraja hayo usiku na mchana ili yamalizike kwa wakati ama kabla ya muda huo katika kurahisisha maendeleo ya kibiashara katika Jiji la Dar es Salaam.

    Mhandisi wa Masuala ya Usalama wa Ujenzi, Richard Baruani alimueleza Rais Magufuli kuwa ujenzi wa Daraja la Tazara umefikia asilimia 64, na linatarajiwa kukamilika Oktoba mwakani. Kwa upande wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo, Mhandisi Mshauri Reginald Kayanga alisema ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako