• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mkutano wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa wafunguliwa Nairobi

  (GMT+08:00) 2017-12-04 17:53:41

  Mkutano wa tatu wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEA umeanza leo mjini Nairobi. Katika mkutano wa mwaka huu utakaofanyika kwa siku tatu ukiwa na kauli mbiu ya "Kuelekea Dunia isiyo na Uchafuzi", suala la kupambana na uchafuzi wa mazingira litapewa kipaumbele katika majadiliano. Jana kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP lilizindua shughuli za kupanda baiskeli ya Mobike mjini Nairob, ili kuinua mwamko wa nafasi ya usafiri endelevu mjini katika kupunguza uchafuzi wa mazingira.

  Shughuli za kupanda baiskeli ya Mobike zenye kauli mbiu ya "kupanda baiskeli kushinda vita dhidi ya uchafuzi" zilifanyika jana mjini Nairobi, na kuhudhuriwa na watu zaidi ya mia mbili kutoka sekta mbalimbali, akiwemo naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP Bw. Erik Solheim, balozi wa China nchini Kenya na mjumbe wa China kwenye shirika la mpango wa mazingira UNEP Bw. Liu Xianfa na mwanzishi wa baiskeli ya Mobike Bibi Hu Weiwei.

  Baiskeli ya Mobike ni moja ya njia za usafiri zinazopendwa na watu wa China, na inapatikana katika kila sehemu nchini China. Tangu izinduliwe miezi 19 iliyopita, idadi ya watu wa China wanaotumia baiskeli kama njia ya usafiri imeongezeka mara mbili, na kupunguza utoaji wa carbon kwa tani milioni 4.4. Njia hiyo ya uvumbuzi ya usafiri usiosababisha uchafuzi wa mazingira imepongezwa na pande mbalimbali, na naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP Bw. Erik Solheim anasema,

  "Tunapenda kueneza zaidi matumizi ya baiskeli ya Mobike, ikiwa ni njia ya usafiri inayopunguza matumizi ya nishati, ili kupunguza uchafguzi mijini, na kujenga mazingira mazuri na ya kirafiki ya kuishi kwa watu ."

  Balozi wa China nchini Kenya na mjumbe wa China kwenye UNEP Bw. Liu Xianfa amesema kupanda baiskeli ya Mobike ni kitendo kinachofanywa na kampuni ya China kuunga mkono shughuli za UNEP. Anasema,

  "Kitendo hicho kinatoa fursa kwa makampuni na watu wengi zaidi wa China kushiriki kwenye shughuli za mazingira duniani, ili tuweze kuishi katika mazingira mazuri."

  Mbali na maofisa, wapenzi wengi wa kupanda baiskeli pia walishiriki kwenye shughuli za jana, na kusema wanapenda kuchangia juhudi zao katika kupunguza uchafuzi. Bibi Maria Mugure raia wa Kenya anasema,

  "Naona shughuli za leo ni nzuri sana, na zinaweza kuinua mwamko wa watu kuhusu kupunguza utoaji wa uchafuzi pamoja na kuonesha kuwa kupanda baiskeli ni njia nzuri katika juhudi hizo. Leo nimefurahi sana, ni rahisi kutumia baiskeli ya Mobike, na rangi yake ni nzuri."

  Baiskeli ya Mobike ni aina moja ya mfumo wa baiskeli ya kutumiwa kwa pamoja, ambao unatoa mchango mkubwa katika kupunguza uchafuzi na kutatua msongamano wa magari, lakini baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa haifai baiskeli kama hizo kuenezwa katika baadhi ya nchi na miji kutokana na hali ya barabara. Kuhusu wasiwasi huo, mwanzilishi wa baiskeli ya Mobike Bibi Hu Weiwei anaona hali zinatofautiana katika nchi mbalimbali, lakini baiskeli haina mipaka ya nchi, njia ya usafiri isiyochafua mazingira haina mipaka ya nchi, na kulinda mazingira kunahitaji juhudi za pamoja za makampuni, serikali na raia.

  "Mwanzoni watu walikuwa na mashaka kuwa mazingira ya hapa hayafai kupanda baiskeli, lakini wazo letu ni kuanza tu, halafu mazingira yatazidi kufaa kupanda baiskeli. Hii inahitaji ushirikiano wa serikali na watumia baiskeli. Baiskeli ya Mobike ni ya watu wote, sio ya kampuni yetu. Pia natarajia mkutano wa mwaka huu wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa utafanya serikali za nchi mbalimbali zitambue kuwa kutokana na njia hiyo, mazingira yatakuwa mazuri, na maisha ya watu yatakuwa mazuri."

  Mbali na kupendekeza kupanda baiskeli, wakati wa mkutano wa mwaka huu wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa, washiriki pia wamehamasishwa kubeba vikombe na vifaa vya kidijitali vya kuandika maelezo, ili kupunguza matumizi mabaya ya karatasi na uchafuzi wa mazingira, na kutekeleza kivitendo kauli mbiu ya "Kuelekea Dunia isiyo na Uchafuzi".

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako