• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Rais Xi Jinping wa China atoa salamu za mwaka mpya wa 2018

  (GMT+08:00) 2017-12-31 19:29:19


  Makomredi, marafiki, mabibi na mabwana,

  Hamjambo! Wakati unakimbia haraka, ni hivi punde tu tutaukaribisha mwaka 2018. Napenda kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wa makabila mbalimbali, ndugu wa mkoa wa utawala malumu wa HongKong, ndugu wa mkoa wa utawala maalumu wa Macao, ndugu wa Taiwan na Wachina wanaoishi katika nchi za nje! Pia nawatakia kila la heri marafiki walioko nchi na sehemu mbalimbali duniani!

  Bidii huzaa matunda, na kuleta mabadiliko mapya kila wakati. Mwaka 2017, tulifanya Mkutano mkuu wa 19 wa Chama cha Kikomunisti cha China, na kufungua njia mpya ya kuijenga China kwa pande zote kuwa nchi ya ujamaa ya kisasa. Pato la taifa la China limefikia Yuan trilioni 80, nafasi za ajira mijini na vijijini zimeongezeka kwa zaidi ya milioni 13, bima ya uzeeni inawanufaisha zaidi ya watu milioni 900, bima ya matibabu ya kimsingi inawanufaisha zaidi ya watu bilioni 1.35, na watu maskini zaidi ya milioni 10 vijijini wameondolewa kutoka kwenye umaskini. Shairi moja la kale la kichina linasema "Ni vipi nitaweza kupata maelfu ya nyumba za kuwahifadhi watu wote maskini, na kuwafanya wawe na furaha!"Watu maskini milioni 3.4 wamehamishiwa kwenye maeneo mengine na kujengewa nyumba mpya, na mradi wa kukarabati maeneo ya makazi duni umetimiza lengo la kujenga nyumba milioni 6 kabla ya wakati uliopangwa. Shughuli mbalimbali za kuboresha maisha ya watu zimeharakishwa, mazingira ya kiikolojia yanaboreshwa hatua kwa hatua, na wananchi wamejionea mafanikio, furaha na salama. Tumepiga hatua nyingine kubwa kuelekea lengo la kukamilisha ujenzi wa jamii yenye maisha bora.

  Mafankio mengi yamepatikana kwenye uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia, na miradi mikubwa ya ujenzi. Satelaiti ya "Insight" ilirushwa kwa mafanikio, ndege kubwa ya abiria aina ya C919 iliyotengenezwa na China imeruka, kompyuta ya kisasa inayotumia teknolojia ya Quantum imetengenezwa kwa mafanikio, majaribio ya mpunga unaoweza kuhimili maji ya bahari yamefanyika, manowari ya kwanza ya China inayobeba ndege imetepelekwa majini, nyambizi ya kisasa ya "Seawing" imekamilisha operesheni ya uchunguzi kwenye bahari yenye kina kirefu, jaribio la kwanza la kukusanya gesi yabisi baharini limefanikiwa, bandari ya kisasa inayojiendesha ya Yangshan imeanza kutoa huduma rasmi, ujenzi wa daraja la kuvuka bahari linalounganisha HongKong, Zhuhai na Macao umekamilika, na treni za mwendo kasi za Fuxing zimeanza safari na kutoa huduma kote nchiniā€¦ Nawapongeza wanachi wetu wa China kwa nguvu yao kubwa ya uvumbuzi!

  Tulifanya gwaride kubwa kwenye kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Zhurihe, ili kuadhimisha miaka 90 tangu Jeshi la ukombozi wa watu wa China lianzishwe. Wakati wa kuadhimisha miaka 20 tangu HongKong irudi China, nilienda HongKong na kujionea mwenyewe kwamba, ikiwa na uungaji mkono mkubwa na imara kutoka kwa nchi yake, HongKong imedumisha ustawi na utulivu, na hakika itakuwa na mustakbali mzuri zaidi katika siku zijazo. Pia tulifanya maadhimisho ya miaka 80 ya mapambano ya watu wa China dhidi ya uvamizi wa Japan, pamoja na maadhimisho ya kitaifa ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji makubwa ya Nanjing, ili kuwakumbusha wananchi kuhusu historia na kuomba amani.

  Tuliandaa shughuli kadhaa za kidiplomasia za pande nyingi hapa nchini, ikiwemo Baraza la ushirikiano wa kimataifa la "Ukanda mmoja, Njia moja", Mkutano wa viongozi wa nchi za BRICS wa Xiamen, na Mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Chama cha kikomunisti cha China na vyama mbalimbali vya kisiasa duniani. Pia nilihudhuria mikutano muhimu ya pande nyingi duniani. Mwanzoni mwa mwaka huu, nilihudhuria mkutano wa mwaka wa Baraza la uchumi duniani Davos, na kutoa hotuba kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini Geneva, baadaye nilihudhuria Mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20, G20, na mkutano usio rasmi wa viongozi wa Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya Asia na Pasifiki APEC. Kwenye mikutano hiyo, nilibadilishana maoni kwa kina na pande mbalimbali, ambazo zote zimekubali kusukuma mbele ujenzi wa Jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja, ili kuwanufaisha watu wa nchi mbalimbali duniani.

  Mwaka 2017, nilipokea barua nyingi kutoka kwa wananchi, wakiwa ni pamoja na wanavijiji wa tarafa ya Yumai ya wilaya ya Longzi ya mkoa wa Tibet, na wafugaji wa Wulan kwenye eneo la Sunite mkoani Mongolia ya ndani, pia kuna maprofesa wazee wa chuo kikuu cha mawasiliano cha Xi'an, na wanafunzi wa chuo kikuu cha Nankai waliojiunga na jeshi, nimeguswa sana na maelezo kuhusu maisha yao. Jinsi wananchi wanavyoshikilia moyo wa uzalendo na kujitoa muhanga kwa ajili ya taifa bila kujuta, imenifanya nione kwamba mamilioni ya watu wa kawaida wanaochangia jasho na damu, ndio ni wakubwa, na kwamba furaha zinapatikana tu kwa juhudi na bidii.

  Makomredi, marafiki, mabibi na mabwana,

  Mwaka 2018 ni mwaka wa mwanzo wa kutekeleza kikamilifu moyo wa Mkutano mkuu wa 19 wa Chama cha kikomunisti cha China, ambao umechora ramani kwa ajili ya maendeleo ya China kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 ijayo. Mnara mkubwa hujengwa kwa kuanza na msingi imara. Ili tuweze kuibadilisha ramani hiyo iwe hali halisi, lazima tuachane na mawazo matupu, kuweka nyayo hatua kwa hatua na kufanya kazi kwa bidii na kwa makini.

  Katika mwaka 2018, tutakaribisha miaka 40 tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango. Mageuzi na ufunguaji mlango ni njia ya lazima kwa China kujiendeleza na kupiga hatua, na pia ni njia ya lazima katika kutimiza ndoto ya China. Tunapaswa kutumia fursa ya kuadhimisha miaka 40 ya mageuzi na ufunguaji mlango, kukabiliana kwa ushupavu na kwa busara, na matatizo na changamoto zote zinazotukabili, ili kutekeleza mageuzi kikamilifu.

  Ni ahadi yetu ya makini kwamba tutawaondoa watu wote maskini vijijini kutoka kwenye umaskini kutokana na vigezo vya sasa, ifikapo mwaka 2020. Ahadi ni deni. Bado imebaki miaka mitatu tu kuelekea mwaka 2020, jamii nzima inapaswa kuchangia busara na kuchukua hatua madhubuti kwa pamoja, ili kuweza kuendelea kupata ushindi kwenye kampeni hiyo. Tukishinda kwenye vita hiyo ngumu dhidi ya umaskini ndani ya miaka mitatu kama ilivyopangwa, itakuwa ni mara ya kwanza kwa taifa la China kutokomeza umaskini kikamilifu katika historia yake ya miaka elfu kadhaa, Tuungane mikono kwa pamoja katika kukamilisha shughuli hii kubwa na yenye maana muhimu kwa taifa la China, na kwa binadamu wote.

  Hivi sasa pande mbalimbali zina matarajio na pia wasiwasi juu ya mustakbali wa amani na maendeleo ya binadamu, na kuitarajia China ioneshe msimamo. Binadamu wote ni familia moja. China ikiwa ni nchi yenye kuwajibika, pia inapaswa kutoa maoni yake. China inalinda kithabiti mamlaka na hadhi ya Umoja wa mataifa, kutekeleza kwa makini wajibu na majukumu yake kimataifa, kufuata ahadi yake ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, na kusukuma mbele kwa hatua madhubuti ujenzi wa "Ukanda mmoja, Njia moja"; Siku zote China inakuwa mjenzi wa amani ya dunia, mchangiaji wa maendeleo ya dunia, na mlinzi wa utaratibu wa kimataifa. Watu wa China wangependa kushirikiana na watu wa nchi mbalimbali duniani, kufungua kwa pamoja mustakabali mwema wa binadamu wenye ustawi na amani zaidi.

  Makomredi, marafiki, mabibi na mabwana,

  Mafanikio yetu makubwa kwenye maendeleo yamevumbuliwa na wananchi wetu, na yanapaswa kuwanufaisha wananchi kwa pamoja. Kama ninavyofahamu, mambo wanayofuatilia zaidi wananchi ni yale yanayohusiana na elimu, ajira, mapato, bima ya jamii, matibabu, huduma za matunzo ya uzeeni, makazi na mazingira, tumekuwa na mafanikio mengi, lakini pia tunakabiliwa na wasiwasi na usumbufu. Bado kuna dosari nyingi kwenye kazi zinazohusiana na maisha ya watu, hali inayotuhitaji tuongeze moyo wa kubeba majukumu na wajibu, na kufanya vizuri na kihalisi kazi zinazonufaisha maisha ya wananchi. Kamati za chama, serikali na maofisa kwenye ngazi zote wanatakiwa kuyaweka moyoni kila wakati mambo yanayohusiana na usalama na neema ya wananchi, kuzichukulia kazi za kuboresha maisha ya watu kama mafanikio makubwa zaidi ya kisiasa, na kujali mambo yanayofuatiliwa na wananchi, ili kuwafanya waishi kwa furaha na kwa neema zaidi.

  Asanteni.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako