• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yatoa waraka wake wa kwanza kuhusu Ncha ya Kaskazini

    (GMT+08:00) 2018-01-26 17:00:01

    Waraka wa "sera ya China kuhusu Ncha ya Kaskazini" umetolewa leo hapa Beijing. Hii ni mara ya kwanza ya China kutoa waraka kuhusu Ncha ya Kaskazini. Waraka huo umefafanua msimamo wa kimsingi wa China katika suala la Ncha ya Kaskazini, na kusisitiza kuwa China inapenda kushirikiana na pande husika kutumia fursa ya maendeleo ya sehemu hiyo, na kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

    Takwimu zinaonesha kuwa katika miaka 10 iliyopita, kasi ya ongezeko la joto katika sehemu ya Ncha ya Kaskazini ni mara mbili kuliko sehemu nyingine duniani, huku katika miaka 30 iliyopita, maeneo yanayofunikwa na barafu katika bahari ya Arctic katika majira ya joto yakipungua kwa nusu. Wakati huo huo, kutokana na kuzidi kwa mafungamano ya kiuchumi duniani, na umoja wa kikanda, thamani za Ncha ya Kaskazini katika nyanja za mikakati, uchumi, utafiti wa sayansi na uhifadhi wa mazingira imeongezeka kwa kiasi kikubwa, na kufuatiliwa na pande mbalimbali.

    China si nchi iliyoko karibu na Ncha ya Kaskazini, hata hivyo, waraka huo umeeleza kuwa China ina maslahi muhimu katika mambo ya sehemu hiyo. Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Kong Xuanyou leo amewaambia waandishi wa habari kuwa, badala ya 'vitendo vya kuotea', China itafanya 'kazi zipaswazo' katika mambo ya Ncha ya Kaskazini. Anasema,

    "Kutofanya 'vitendo vya kuotea', maana yake ni kwamba China haitaingilia mambo ya ndani ya nchi za Ncha ya Kaskazini. Tutashughulikia masuala ya sehemu hiyo kwa mujibu wa sheria za kimataifa. 'kazi zipaswazo' maana yake ni kuwa, ikiwa nchi yenye maslahi muhimu katika sehemu ya Ncha ya Kaskazini, China itafanya kazi ya kiujenzi katika masuala ya kimataifa yanayohusiana na sehemu hiyo."

    Waraka huo umeonesha kuwa malengo ya sera ya China kuhusu Ncha ya Kaskazini ni kutambua, kuhifahdi, kutumia na kushughulikia Ncha ya Kaskazini pamoja na pande nyingine, ili kuhifadhi maslahi ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa, na kuhimiza maendeleo endelevu ya sehemu hiyo. Hata hivyo baadhi ya nchi zina wasiwasi kuwa China ina madhumuni ya kimkakati na kijeshi katika Ncha ya Kaskazini. Bw. Kong anasema,

    "Nataka kusisitiza kuwa China kushiriki kwenye shughuli za kuendeleza Ncha ya Kaskazini kutatoa mchango kwa sehemu hiyo, na kuleta fursa ya maendeleo, ambayo itawanufaisha watu wake. Baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa tuna hila ya kunyakua maliasili, na kuleta uchafuzi wa mazingira. Naona wasiwasi huo hauna msingi wowote. Nchi za Ncha ya Kaskazini zina sheria kamili, na zimeweka vigezo vya juu katika nyanja za uhifadhi wa mazingira, ajira na shughuli za kibiashara. Tunaamini kuwa tutafuata sheria na vigezo hivyo, na kuchangia maendeleo ya jamii na uchumi wa Ncha ya Kaskazini na maisha bora ya watu wa huko."

    Naibu mkuu wa taasisi ya utafiti wa masuala ya kimataifa ya Shanghai Bw. Yang Jian amesema, waraka huo si kama tu umefafanua kanuni na msimamo wa China katika masuala ya Ncha ya Kaskazini, bali pia umeonesha ujasiri wa China wa kuwajibika katika kukabiliana na changamoto za kimataifa. Anasema,

    "Mwaka jana rais Xi Jinping wa China alitoa hotuba kuhusu uendeshaji wa mambo ya kimataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva. Viongozi wa nchi nyingi za Ncha ya Kaskazini walisikiliza hotuba hiyo na kuinukuu kwenye hotuba zao. Hivi karibuni kutokana na baadhi ya nchi haswa nchi zilizoendelea kurudi nyuma katika majukumu ya kimataifa, na vitendo vya China vinafuatiliwa zaidi na jumuiya ya kimataifa. Mawazo ya amani, mamlaka, manufaa ya pamoja na uendeshaji wa shughuli za kimataifa kwa pamoja yaliyotolewa na rais Xi kwenye hotuba yake yameonekana vya kutosha katika waraka huo."

    Waraka wa "sera ya China kuhusu Ncha ya Kaskazini" utachapishwa kwa lugha nane za Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirussia, Kijerumani, Kihispania, Kiarabu na Kijapan.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako