• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maofisa, wachumi wa sehemu na nchi mbalimbali wakosoa mpango wa Marekani kuongeza ushuru dhidi ya bidhaa za China

    (GMT+08:00) 2018-03-25 19:16:51
    Ujumbe wa mabalozi, maofisa wa serikali na viongozi wa biashara wa Marekani na China wamekosoa uamuzi wa rais Donald Trump wa kuongeza ushuru dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka China kwenye shughuli ya ushirikiano wa biashara uliofanyika Ijumaa jimboni California.

    Mwenyekiti wa Baraza la Uuzaji Bidhaa Nje la Los Angeles Brian Peck amesema China ni mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa California na vita ya biashara inaweza kuharibu kila mtu. Ameongeza kuwa hatua za makini zinapaswa kuchukuliwa kabla ya kuanza kuitekeleza.

    Naibu mkurugenzi wa masuala ya kimataifa na maeneleo ya biashara katika ofisi ya gavana wa California Awinash Bawle amesema hii sio njia sahihi ya kutatua hali ya kukosekana uwiano katika biashara, na itasababisha matokeo mengi yasiyotarajiwa.

    Wakati huohuo maofisa na wataalamu wa Argentina na Ujerumani pia wameeleza kuwa hatua hiyo na vitendo vingine vya kujilinda kibiashara vinaweza kuongeza mvutano katika uhusiano wa kibiashara wa pande mbili, na kwenda kinyume na uchumi wa kimataifa katika zama za leo.

    Mchumi wa Argentina Jorge Marchini amesema mipango hiyo ni kinyume na mfumo wa pande nyingi na njia ambazo zimetawala uchumi wa kimataifa katika miongo saba iliyopita. Anaona kuwa hatua ya upande mmoja ya Marekani inaharibu uwiano wa kimataifa wenye utata kama vile uhusiano wa kibiashara, mabadilishano ya bidhaa na pia muunganiko (links) mpana wa mtiririko wa fedha kati ya nchi.

    Chansela wa Ujerumani Angela Merkel anayehudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya wa majira ya spring amesema nchi za Umoja huo zinaunga mkono kwa kauli moja biashara huria na kupinga sera ya kujilinda kibiashara.

    Gazeti maarufu la biashara la Ujerumani Handelsblatt ijumaa lilichapisha makala moja ya uchambuzi yenye kichwa cha "vita ya biashara ya Trump hakika itashindikana" imesema Trump anataka kufungua mlango wa soko la China kwa kupitia vita ya biashara, jambo ambalo litashindikana, na badala ya kuisaidia Marekani, itaharibu maslahi yake na nchi nyingine.

    Wakati huohuo, naibu mkuu wa shule ya usimamizi ya Rotterdam ya Chuo Kikuu cha Erasmus, Uholanzi Profesa Zhang Ying amesema kama Trump anashikilia kufanya vita hiyo ya biashara, italeta hasara kwa sekta ya biashara na uwekezaji, ushirikiano wa makampuni, wateja na walipa kodi nchini Marekani na Marekani itaumia yenyewe.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako