• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Historia ya mifuko ya plastiki

    (GMT+08:00) 2018-06-05 09:40:58

    Katika miaka ya 70 ya karne ya 20, mifuko ya plastiki ilikuwa ni kitu kipya na adimu, lakini sasa imekuwa ni bidhaa inayopatikana na kutumika kila mahali duniani, na uzalishaji wake umefikia mifuko trilioni moja kwa mwaka. Lakini mifuko hiyo ambayo kwa sasa imesambaa kila mahali duniani ikiwemo chini ya bahari na hata juu ya kilele cha Mlima Everest, imeleta changamoto kubwa kwa mazingira ya dunia. Je, mifuko hiyo ilivumbuliwa kivipi na itapigwa marufuku vipi?

    Mwaka 1933, kiwanda kimoja cha kemikali mjini Norwich nchini Uingereza kilivumbua bila kukusudia plastiki inayotumika sana sasa inayojulikana kama polyethylene PE. Ingawa kabla ya hapo plastiki ya aina hiyo iliwahi kuzalishwa kidogo kiwandani, hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa malighafi ya kikemikali inayotumika sana viwandani kuvumbuliwa duniani, na plastiki hiyo ilitumiwa kisiri na jeshi la Uingereza wakati wa Vita kuu ya pili ya dunia.

    Mwaka 1965, Kampuni ya Celloplast ya Sweden ilipata hakimiliki ya mifuko ya plastiki ya PE. Mifuko hiyo iliyosanifiwa na mhandisi Sten Gustaf Thulin ilisambaa haraka barani Ulaya na kuchukua nafasi ya mifuko ya kitambaa na ya karatasi.

     

    Mwaka 1979, mifuko ya plastiki iliyochukua asilimia 80 ya soko la mifuko ilianza kuingia kwenye soko la kimataifa, na kufikia Marekani. Makampuni ya kutengeneza mifuko ya plastiki yalianza kujitahidi kutangaza bidhaa zao, na kudai kuwa mifuko hiyo ni bora kuliko ile ya karatasi, na kutangaza manufaa ya mifuko ya plastiki inayoweza kutumiwa mara nyingi.

    Mwaka 1982, supamaketi mbili kubwa za Marekani Safeway na Kroger zilianza kutumia mifuko ya plastiki, na maduka mengi zaidi yakaanza kuzifuata. Katika miaka 10 iliyofuata, mifuko ya plastiki ikachukua kabisa nafasi ya mifuko ya karatasi kote duniani.

    Mwaka 1997, baharia na mtafiti Charles Moore aligundua ukanda wa takataka za plastiki kwenye bahari ya Pasifiki. Mzunguko wa maji baharini huchangia kulimbikiza takataka za plastiki, na ukanda huo wa takataka ni moja lenye eneo kubwa zaidi kati ya maeneo matano yenye malimbikizo ya takataka baharini, ambayo yametoa tishio kubwa kwa maisha ya viumbe wa baharini. Mifuko ya plastiki imepata sifa mbaya kutokana na kusababisha vifo vya kobe wengi, ambao walikabwa baada ya kuimeza mifuko hiyo kwa kushani ni viwavi.

    Mwaka 2002, Bangladesh ilikuwa nchi ya kwanza duniani kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, kwa kuwa mifuko hiyo ilikuwa chanzo kikuu kinachosababisha kuziba kwa mabomba yanayopitisha maji haswa wakati wa maafa ya mafuriko. Nchi nyingi zikafuata na kupiga marufuku mifuko ya plastiki.

    Mwaka 2011, mifuko ya plastiki milioni moja ilikuwa inatumika kila dakika duniani.

    Mwaka 2017, Kenya ilitekeleza marufuku ya mifuko ya plastiki, na kuifanya idadi ya nchi zilizoweka sheria ya kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki ifikie zaidi ya 20.

    Mwaka 2018, "Kupambana na kutokomeza mifuko ya plastiki" imechaguliwa kuwa kauli mbiu ya Siku ya mazingira duniani kwa mwaka huu, na maadhimisho ya Siku hiyo kwa mwaka huu yatafanyika India. Serikali na mashirika ya nchi mbalimbali duniani yameeleza kuunga mkono kampeni hiyo, na kusisitiza ahadi na dhamira yao ya kutatua suala la uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na mifuko hiyo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako