• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Rais Putin wa Russia azungumzia uhusiano kati ya Russia na China

  (GMT+08:00) 2018-06-06 06:48:30

  Kabla ya kufunga safari ya kuja China kuhudhuria Mkutano wa kilele wa Baraza la viongozi wa nchi wanachama wa Shirika la ushirikiano wa Shanghai SCO na kufanya ziara ya kitaifa nchini China, rais Vladimir Putin wa Russia amefanyiwa mahojiano na mkuu wa Kituo Kikuu cha Radio na Televisheni cha Taifa cha China Bw. Shen Haixiong, na kuzungumzia uhusiano kati ya Russia na China, na mustakabali wa SCO baada ya kupanuliwa kwake.

  "Mheshimiwa Rais Putin, nakushukuru kukubali kufanyiwa mahojiano maalum na Kituo Kikuu cha Radio na Televisheni cha Taifa cha China…"

  Hii ni mara ya kwanza kwa rais Putin kukubali kufanyiwa mahojiano na vyombo vya habari vya nchi za nje tangu aapishwe kuwa rais wa Russia kwa muhula mwingine, pia ni mara ya kwanza kwake kufanyiwa mahojiano na vyombo vya habari vya China kwenye Ikulu ya Kremlin. Kabla ya kuanza kwa mahojiano hayo, rais Putin ametoa salamu kwa watu wa China, akiitakia kila familia ya wachina furaha na neema!

  Kwenye mahojiano hayo, Rais Putin amesema Russia inatilia maanani uhusiano wa kiwenzi na kirafiki kati yake na China, na nchi hizo mbili zimejenga uhusiano imara na wa kipekee kwenye msingi wa kunufaishana.

  Amesema Mkataba wa ushirikiano wa ujirani mwema uliosainiwa mwaka 2001 kati ya Russia na China umeweka msingi imara kwa maendeleo makubwa yaliyopatikana kwenye uhusiano kati ya nchi hizo mbili, na maoni mengi ya pamoja ya nchi hizo mbili kuhusu namna ya kuendeleza nchi na namna ya kuwatendea wananchi, yanaziunganisha nchi hizo mbili. Rais Putin anasema:

  "Tukinukuu hotuba aliyoitoa rais Xi Jinping kwenye Mkutano mkuu wa 19 wa Chama cha Kikomunisti cha China, ni mambo gani yana umuhimu mkubwa zaidi? Kama rais Xi alivyosema ni kuinua kiwango cha maisha ya watu. Kuna njia nyingi zinazoweza kutimiza lengo hilo, lakini lengo lenyewe ni la pamoja. Nchini Russia, hakuna lengo lingine licha ya kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wetu. ndiyo maana, tunafikiria kwa makini jinsi tutakavyojenga uhusiano kati yetu na China, namna ya kutimiza malengo hayo huku tukihakikisha usalama, na kuimarisha ujenzi wa uchumi wa aina mpya kupitia uvumbuzi, teknolojia za kisasa, masikilizano ya jamii na usimamizi wa kiuchumi. Naamini kuwa tukifanya juhudi kubwa hakika tutapata mafanikio mapya. "

  Huu ni mwaka wa tano tangu China itoe pendekezo la Ukanda mmoja Njia moja. Mwezi Mei mwaka 2015, viongozi wa China na Russia walisaini taarifa ya pamoja, na kuanzisha mchakato wa kuunganisha pendekezo la "Ukanda mmoja na Njia moja" la China na mpango wa Russia wa kuhimiza mafungamano ya kiuchumi kati ya Ulaya na Asia. Katika miaka mitatu iliyopita, ufanisi wa ushirikiano huo umeonekana, na matunda mengi yamepatikana kwenye sekta za nishati, uchukuzi na usafiri wa ndege.

  Kwenye mahojiano, rais Putin amesifu pendekezo la "Ukanda mmoja na Njia moja" lililotolewa na rais Xi Jinping, na kuona ni pendekezo muhimu lenye manufaa na mustakbali. Amesisitiza kuwa Russia siku zote inaunga mkono pendekezo hilo, na mchakato wa kuunganisha mikakati ya maendeleo ya Russia na China utapanua zaidi mustakbali wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Mwaka jana, thamani ya biashara kati ya China na Russia iliongezeka na kufikia dola za kimarekani bilioni 87, na rais Putin anaona ongezeko hilo ni la kuridhisha, na mwelekeo huu unapaswa kudumishwa katika siku zijazo.

  Mkutano wa kilele wa shirika la SCO utafanyika mjini Qingdao baada ya siku chache. Huu ni mkutano wa kwanza wa kamati ya viongozi utakaofanyika baada ya upanuzi wa shirika hilo. Rais Putin amesema, baada ya kupanuliwa, Shirika hilo limekuwa shirika la ulimwengu, ana imani kubwa kuhusu mustakabali wa maendeleo ya shirika hilo. Wakati huohuo, pia alisisitiza akisema:

  "Hatutaki kupambana na nchi nyingine, tunataka kuhakikisha ushirikiano wa pande zote kati ya nchi mbalimbali na kuweka mazingira ya lazima kwa ushirikiano huo bila kujali nchi hizo zipo katika sehemu gani au bara gani. Kuunganisha nguvu za nchi hizo bila shaka kutachangia maendeleo yetu, na pia kuwa na ushawishi kwenye jukwaa la kimataifa. Nina imani kuwa mambo hayo yatakuwa athari chanya."

  Kabla ya kuhudhuria mkutano wa shirika la ushirikiano la Shanghai utakaofanyika mjini Qingdao, rais wa Russia Bw. Vladimir Putin atafanya ziara rasmi nchini China kutokana na mwaliko wa Rais wa China Xi Jinping. Rais Putin amesema rais Xi ni mwenzi wa ushirikiano na rafiki wa kuaminika.

  "Baada ya kumaliza kazi, Rais Xi alinisherehekea siku yangu ya kuzaliwa, yeye ni mpole mwenye udhati na kuaminika, kama viongozi wa nchi nyingine, anajitahidi kuongeza ufanisi wa kazi na kutafuta maslahi ya wananchi wake. Yeye pia ni mchambuzi hodari wa masuala mbalimbali, na ninapenda sana kujadiliana naye masuala ya kimataifa na kiuchumi. "

  Kwenye mahojiano hayo yaliyofanyika kwa zaidi ya nusu saa, rais Putin pia amezungumzia uhusiano kati ya Russia na nchi za magharibi, na suala la peninsula ya Korea. Amesema vikwazo vyote haramu na sera zinazohujumu maendeleo ya uchumi wa dunia, vitatokomezwa hatua kwa hatua, na Russia inatarajia kurejesha uhusiano wa kawaida na nchi za magharibi kwa njia fulani. Kuhusu suala la peninsula ya Korea, Rais Putin amesema msimamo wa Russia na China juu ya suala hilo unafanana, na lengo la pamoja ni kuondoa silaha za nyuklia kwenye peninsula ya Korea na kumaliza hali ya mvutano kwenye kanda hiyo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako