• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  •  Kenya yalenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kibiashara na China

    (GMT+08:00) 2018-08-07 09:11:46

    Kenya itatafuta kukuza ushirikiano na China katika kuongeza thamani bidhaa za kilimo wakati wa mkutano wa kilele wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ,FOCAC , ili kuongeza mauzo ya bidhaa zake nchini China pamoja na kupunguza pengo la urari mbaya wa biashara.

    Waziri asiye na Wizara maalum ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama tawala cha Jubilee,Raphael Tuju amesema Kenya inalenga kufanya uwekezaji wa kuongeza thamani kwa majani chai pamoja na bidhaa nyingine za kilimo wakati wa Mkutano wa kilele wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliopangwa kufanyika mwezi Septemba jijini Beijing.

    Bidhaa zinazoagizwa Kenya kutoka China zimeongezeka zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hadi shilingi bilioni 390.

    Maafisa wa Kenya wamekuwa wakijadiliana na serikali ya China na viongozi wa kibiashara kuhusu kutafuta njia za kuongeza mauzo ya bidhaa nchini China ili kuleta usawa wa biashara.

    Kulingana na Waziri asiye na wizara maalum,ambaye pia ni katibu Mkuu wa chama tawala cha Jubilee,Raphael Tuju,nyongeza ya thamani na upakiaji mzuri wa bidhaa ndio njia ya haraka ya kuongeza mauzo ya bidhaa za Kenya nchini China.

    Akizungumza katika ofisi yake jijini Nairobi jana,aidha Tuju alisema juhudi zimefanywa katika kutafuta wawekezaji na makampuni ya China kuwekeza nchini Kenya.

    "Hivi majuzi Bw Yang kutoka uongozi wa chama tawala cha China alipokuja Kenya nilienda nae katika baadhi ya mashamba ya majani chai ,na tunaangalia ni jinsi gani tutavisaidia viwanda vya majani chai na upakiaji au ufungaji wa bidhaa hiyo haswa kulingana na soko la China"

    Tuju anaamini kuwa kushirikiana na serikali ya China na viongozi wa biashara kutasaidia kutoa fursa nyingi zaidi za biashara kwa Kenya kuliko ilivyo sasa.

    "Kwa sasa tunapata chini ya asilimia 10 ya kile ambacho tungepata kama tungeshirikiana nao katika upakiaji"

    Naye Naibu mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara na Viwanda nchini Kenya (KNCCI),Bw James NdungĀ“u Mureu anasema wanajitahidi kuongeza mauzo ya bidhaa za Kenya katika soko la China na pia kuwashawishi wachina kuwekeza nchini Kenya.

    "Yetu imefifia kidogo kwa sababu mauzo yetu ya nje ni kidogo,lakini tumekubaliana ya kwamba tutajaribu kusukuma majani chai,kahawa,vinyago,maua ili kupunguza lile pengo lisiwe kubwa vile lilivyo.Tunajaribu kuwahimiza waje nchini Kenya wafungue viwanda hapa na bidhaa zile tuzipeleke sehemu mbalimbali barani Afrika"

    Wakati huo huo Mureu amesema Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda nchini Kenya kitaendelea kujiweka karibu na kushirikiana na China kwa sababu China ni rafiki wa kweli.

    "Sisi tunaangalia China kwa sababu wana masharti machache na tutazidi kufanya kazi na wao kwa sababu ukiangalia nchi za magharibi na Marekani masharti yao ni mengi na shida zetu zinazidi.saa zingine ukipata barabara zimekatika hautaki kuambiwa masharti mengi unataka kupewa suluhisho.Kwa hivyo tunaona wachina wanatupatia suluhisho mara kwa mara"

    Aidha Mureu amezitaka kampuni za China ziendelee kuongeza uwekezaji kwa Kenya, na kutafuta miradi zaidi inayoweza kufanyiwa ushirikiano.

    Vilevile ameitaka serikali ya Kenya iweke sera nafuu zaidi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako