• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Kenyatta pamoja na viongozi wengine wasisitiza kuwa ushirikiano ni muhimu kwa bara la Afrika kupata maendeleo endelevu

    (GMT+08:00) 2018-11-28 08:40:19

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa ushirikiano baina ya nchi,miji na jamii ni ufunguo wa kuhakikisha maisha endelevu siku za baadaye.

    Akizungumza katika mkutano wa magavana na mameya,ambao uliandaliwa sambamba na kongamano linaloloendelea la Uchumi Endelevu wa Rasilimali za Baharini katika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi,Rais Kenyatta alisema dunia ina fursa moja ya kipekee ya kujenga mfano ambao ni rafiki kwa mazingira na ambao unaruhusu unyonyaji mkubwa wa rasilimali kwenye ardhi na kwenye bahari.

    Mwanahabari wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo.

    Rais Kenyatta amesema swali kuu linalokabili binadamu ni jinsi ya kuwalisha watu bilioni 9 ambao wanakadiriwa kuwa duniani ifikapo mwaka 2050.

    Alisema njia nzuri ya kukabiliana na changamoto hii ni kuongeza ujasiri wa jamii na pia kushiriki katika utunzaji wa mazingira.

    Rais Kenyatta alisema njia nyengine ya kukabiliana na changamoto ya idadi ya watu ni kukuza ushirikiano kati ya ngazi tofauti serikali na ushirikiano wa miji na miji.

    Alisema robo tatu ya idadi ya watu inaishi katika miji ya pwani na kuna haja ya kuzingatia uendelevu wao.

    "Maono yetu yasiwe tu kuhusu kujenga miji mikubwa,lakini pia yawe ni kuhusu kutengeneza nafasu za ajira na sehemu nzuri za jamii kuishi"

    Aidha Rais Kenyatta alisema hatua zinafaa kuchukuliwa ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi hasa kwenye miji ya pwani.

    Rais Kenyatta alisema kongamano la Uchumi endelevu wa rasilimali za majini limekuja wakati mzuri ambapo serikali na mashirika yasiyo ya serikali yanatambua umuhimu wa kufanya kazi pamoja.

    Wakati huo huo Rais Kenyatta alitoa mwito kwa wawekezaji kutumia fursa zilizopo na kuwekeza katika maji,usafi wa mazingira na usimamizi wa taka.

    "Kaunti zetu hapa nchini Kenya zina miradi ya uwekezaji.Nawaalika nyote kujadiliana na kaunti zetu kuhusu miradi hii na kuangalia ni jinsi gani mnaweza kushirikiana.Tunatarajia ushirikano ulioimarika zaidi kati ya miji,serikali,mashirika ya kimataifa,na sekta ya biashara ili kufanya miji yetu kuwa na maendeleo endelevu"

    Rais wa Ushelisheli Danny Faure alisema nchi za Afrika zinafaa kushirikiana katika kuleta maendeleo endelevu ya uchumi wa rasilimali za majini.

    "Kama nchi za Afrika sisi sote ni wanufaika wa uchumi wa majini.kwa hivyo ni muhimu Afrika ishirikiane katika kutafuta njia zote za uwekezaji endelevu katika sekta ya majini"

    Aidha alisema kuwa jukumu la Kenya kuandaa na kuwa mwenyeji wa kongamano hili la uchumi wa majini ni ishara kuwa bara la Afrika limeamka na kutambua utajiri ulioko katika bahari na maziwa yake.

    Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki alisema ipo haja ya kulinda mazingira kwani yasipolindwa husababisha athari hasi kwa kiasi kikubwa.

    "Athari za mabadiliko ya tabianchi husabisha viwango vya maji baharini kushuka,na kusababisha upungufu wa samaki,uchafuzi unatia sumu baharini .Ni kutokana na baadhi ya changamoto hizi ambapo vijana wengi badala ya kufaidika na rasilimali za uchumi wa majini hujitoa mhanga kuvuka bahari kwenda kutafuta maisha mazuri sehemu nyingine.Na wengi wao hupoteza maisha baharini wakiwa wanakwenda kutafuta maisha mazuri"

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako