Marekani imelitambua Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislam cha Iran (IRGC) kuwa kundi la kigaidi, hatua isiyotarajiwa ambayo itaongeza zaidi mvutano kati ya nchi hiyo na Iran, na kufanya hali ya Mashariki ya Kati kuwa mbaya zaidi.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema katika taarifa yake iliyotolewa jana na Ikulu ya nchi hiyo kuwa, hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Marekani kutaja sehemu ya serikali ya nchi nyingine kuwa kundi la kigaidi. Amesema hatua hiyo ambayo haikutarajiwa, inayoongozwa na wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, inatambua ukweli kuwa Iran sio tu ni nchi inayofadhili ugaidi, lakini pia kundi la IRGC, kama kifaa cha serikali, linashiriki, kufadhili, na kutetea ugaidi.
Katika hatua nyingine, Baraza la Juu la Usalama la Iran limetangaza kuwa, kituo kikuu cha jeshi la Marekani katika Asia Magharibi kuwa ni kundi la kigaidi.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana, Baraza hilo limelaani vikali hatua isiyo ya kisheria na ya hatari iliyochukuliwa na Marekani kwa kulitambua kundi la IRGC kama kundi la kigaidi, na kusema hatua hiyo isiyo na msingi, inahatarisha amani na usalama katika kanda hiyo na dunia kwa ujumla.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |