• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Baraza la kijeshi la Sudan launga mkono waziri mkuu kuwa kiongozi wa nchi katika serikali ya kiraia

    (GMT+08:00) 2019-04-15 08:58:21

    Baraza la Mpito la Kijeshi nchini Sudan jana limetangaza kuunga mkono pendekezo la waziri mkuu kuwa kiongozi wa nchi katika serikali ya kiraia ambayo itaundwa ndani ya siku chache zijazo.

    Mapema siku hiyo, Kamati ya Kisiasa iliyo chini ya Baraza hilo ilikutana mjini Khartoum ikiwa na wawakilishi kutoka vyama vya siasa pamoja na jeshi. Mjumbe wa kamati hiyo Yassir Abdul-Rahman Al-Atta ameitaka kamati hiyo kukubaliana mapema kuhusu kiongozi asiye na upande wowote kuwa waziri mkuu, na kutaka Kamati hiyo kusaidia kufikia mwisho wa muda wa mpito. Ameeleza matumaini yake kuwa pande zote zitakubaliana kuhusu kuanzishwa kwa serikali ya kiraia ili kutimiza utulivu na amani.

    Wizara ya mambo ya nje ya Sudan nayo imeitaka jamii ya kimataifa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baraza hilo ili kutimiza mageuzi ya kidemokrasia na maendeleo ya usawa nchini humo. Wizara hiyo imesema, hatua zilizochukuliwa na jeshi zinatokana na haja ya mapinduzi ya watu wa Sudan kwa ajili ya uhuru, haki na Amani, baada ya wananchi kutoa wito kwa jeshi kuingilia kati ili kumaliza mgogoro wa kisiasa, kiusalama, na kijamii nchini Sudan.

    Wizara hiyo imerejea tena ahadi ya Sudan kwa mikataba ya ndani ya nchi, ya kikanda na ya kimataifa, maafikiano na makubaliano, na pia nia yake ya dhati ya ujirani mwema na uhusiano wa kimataifa wenye usawa. Pia imeeleza haja yake ya ushirikiano wenye manufaa wa kiuchumi na jamii ya kimataifa ambao utairuhusu Sudan kutumia kikamilifu rasilimali zake za asili na kiuchumi.

    Wakati huohuo, msemaji wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan Shams-Eddin Kabash amesema, kamati maalum imeundwa kusimamia makao makuu na mali za kilichokuwa chama tawala nchini humo, NCP, ambayo haitawashirikisha wanachama wa chama hicho. Amesema, Baraza hilo litaendelea na kampeni yake ya kuwakamata watu wanaohusika na kesi za ufisadi.

    Bw. Kabash pia amesema, Baraza hilo limeamua kuangalia upya balozi za nchi hiyo nje ya nchi, na kumrudisha nyumbani balozi wa nchi hiyo nchini Marekani Bw. Mohamed Atta-Moula, na pia mjumbe wa kudumu wa nchi hiyo kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Bw. Mustafa Ismail.

    Msemaji huo amesema nguvu ya kijeshi haitatumika kuwaondoa maelfu ya watu wanaoandamana mbele ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, na kuwataka wananchi kulisaidia Baraza la Kijeshi kurejesha maisha ya kawaida nchini humo.

    Nayo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (AL) imeeleza kuunga mkono hatua muhimu zilizotangazwa na Baraza hilo ili kufikia mpito wa kisiasa nchini Sudan. Jumuiya hiyo imeeleza kuunga mkono juhudi zilizofanywa na Baraza hilo pamoja na vyama vya siasa na wananchi ili kufikia mwafaka wa kitaifa ambao utatimiza mapenzi na matumaini ya watu wa Sudan.

    April 11, Jeshi la Sudan lilimwondoa na kumshikilia aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir, ikiwa ni kujibu maandamano yaliyodumu kwa miezi minne nchini humo kupinga utawala wake wa miongo mitatu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako