Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri, alipokutana na waandishi wa habari kuwaonyesha shehena ya tumbaku iliyokamatwa ikisafirishwa kuelekea nchi jirani.
Mwanri ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na bodi ya tumbaku nchini kuwakamata wote watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo haramu ambayo inahujumu uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Alisema watu wawili waliokuwa wakitumia gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 290 DGV, walikamatwa juzi usiku wilayani Kaliua wakisafirisha tumbaku kinyume cha sheria.
Alisema thamani halisi ya tumbaku hiyo iliyokamatwa bado haijafahamika na kwamba gari hilo lipo kituo kikuu cha polisi mjini Tabora.
Licha ya kukamatwa kwa gari hilo ameliagiza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kulisaka gari jingine ambalo pia lilikuwa na shehena ya tumbaku inayodaiwa kutoroshwa baada ya kubaini wanafuatiliwa.
Mwanri alisema mkoa kupitia vikao vyake ulijiwekea utaratibu wa kusafirisha mazao kuwa ni mchana tu na si vinginevyo ili kuwadhibiti walanguzi na wana ushirika wachache wasiofuata taratibu za vyama vya msingi.
Alitoa wito kwa wananchi wote kushiriki katika vita hiyo na kuwaonya watumishi wa Serikali kutojihusisha na vitendo hivyo vya kuhujumu uchumi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |