• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Salamu za Mwaka Mpya Mwaka 2020

    (GMT+08:00) 2019-12-31 20:22:00

    Salamu za Mwaka Mpya Mwaka 2020

    (Desemba 31, 2019)

    Xi Jinping

     

    Makomredi, marafiki, mabibi na mabwana,

    Wakati mwaka 2020 unapokaribia, ningependa kuwapa salamu za mwaka mpya kutoka Beijing.

    Mwaka 2019, tumeendelea kupiga hatua mbele kwa jasho na bidii. Tumedumisha maendeleo yenye ubora wa hali ya juu, pato la ndani la taifa linakadiriwa kukaribia dola za kimarekani trilioni 14, huku wastani wa kila mtu ukifikia dola za kimarekani elfu kumi. Juhudi zetu za kuhimiza maendeleo kwenye nyanja tatu zimezaa matunda, ambapo maendeleo yenye uwiano kati ya miji ya Bejing na Tianjin na mkoa wa Hebei, maendeleo ya Ukanda wa Kiuchumi wa Mto Changjiang, ujenzi wa eneo kuu la kiuchumi la ghuba ya Guangdong-Hongkong-Macao, na maendeleo ya pamoja ya peninsula ya mto Changjiang, vyote vimepiga hatua kwa kasi, na uhifadhi wa mazingira asili ya maeneo ya mto Huanghe na maendeleo yenye ubora wa juu vimejumuishwa kwenye Mkakati wa Taifa. Kote nchini, wilaya karibu 340 zimeondolewa kutoka kwenye orodha ya maeneo yaliyoko nyuma kimaendeleo, na watu zaidi ya milioni 10 wameondokana na umaskini. Chombo cha anga ya juu cha Chang'E No. 4 kilitua kwenye sehemu ya nyuma ya Mwezi kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu, roketi ya Long March No. 5 ilirushwa kwa mafanikio, meli ya uchunguzi wa kisayansi ya Xuelong No. 2 ilifika Ncha ya Kusini kwenye safari yake ya kwanza, ujenzi wa mfumo wa setilaiti wa kuongoza mawasiliano wa Beidou umeingia kwenye hatua ya mwisho, mtandao wa kasi wa 5G umeanza kutoa huduma, na uwanja mpya wa ndege wa kimataifa wa Beijing ulioko wilayani Daxing umekamilika na kuanza huduma……mafaniko hayo yote yaliyopatikana kwa jasho na damu walizotoa wachapa kazi wetu wa zama mpya, yameonesha sura na nguvu ya kipekee ya China.

    Katika mwaka uliopita, sera ya mageuzi na kufungua mlango vimeendelea kutilia nguvu mpya maendeleo yetu. Mageuzi ya kitaasisi ya Chama na Serikali vimekamilika kwa mafanikio. Tumeongeza maeneo mapya ya majaribio ya biashara huria na kupanua yale ya mjini Shanghai. Soko la hisa la kuhimiza sayansi na uvumbuzi limeanzishwa na kuendelezwa. Thamani ya kodi na gharama mbalimbali zilizopunguzwa imefikia dola za kimarekani bilioni 280. Tumeinua kikomo cha chini cha kutoza Kodi ya Mapato Binafsi, tumepunguza bei ya dawa nyingi za kawaida, tumeongeza kasi ya mtandao huku tukishusha gharama yake, na zoezi la kuainisha takataka limeongoza mtindo mpya wa maisha unaosaidia kupunguza utoaji wa gesi ya ukaa. "Mwaka wa Kuwapunguzia Mizigo Madiwani" umewarahisishia kazi watumishi wa serikali ya mitaa. Mabadiliko mapya na hali mpya vimetokea katika kila pembe ya nchi yetu.

    Katika mwaka uliopita, mageuzi kwa jeshi na ulinzi wa taifa yamesonga mbele hatua kwa hatua, jeshi la umma limeonesha sura mpya ya zama mpya. Tumefanya Gwaride la Kijeshi la Siku ya Taifa, tumefanya sherehe za kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwa jeshi la majini na jeshi la anga, na tumeandaa Michezo ya Saba ya Majeshi Duniani. Manowari ya kwanza ya kubeba ndege iliyotengenezwa na China imekabidhiwa rasmi kwa jeshi. Jeshi la umma siku zote ni Ukuta Mkuu wa kulinda taifa letu, tutoe heshima kwa walinzi watiifu wa taifa letu!

    Mwaka 2019, kisichosahaulika ni maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Tumeshangilia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika miaka 70 ya Jamhuri yetu, na pia tumeguswa na nguvu thabiti ya Uzalendo. Vikosi vya gwaride vikiwa vimesimama kishujaa, washiriki wa matembezi wakiwa na msisimko, hali iliyofanya uwanja wa Tian'an Men ujae furaha na shangwe. Kila kona ya nchi yetu ikapambwa na rangi ya nyekundu, kila mtu akawa na tabasamu ya fahari usoni, na wimbo wa "Mimi na Taifa Letu" ukasikika katika kila mtaa. Hisia za uzalendo zimetugusa hadi kutokwa na machozi, na moyo wa uzalendo ndio uti wa mgongo wa taifa letu. Mambo hayo yote, yamekuwa mkondo wa kuisifu China Mpya na kupigania Zama Mpya, ambayo yametupa nguvu isiyoisha.

    Katika mwaka mmoja uliopita, nilitembelea sehemu nyingi. Mpango wa ujenzi wa Eneo Jipya la Xiong'an unatekelezwa hatua kwa hatua, bandari ya Tianjin inastawi siku hadi siku, Eneo kuu la pili la mji wa Beijing limeanza kung'ara, mbuga kubwa ya Mongolia ya Ndani yenye mandhari nzuri, Ushoroba wa Magharibi mwa Mto Huanghe ulioshuhudia historia ya miaka elfu moja na pia kuonesha uhai mpya……kila sehemu ya nchi yetu imeonesha hali ya ustawi. Niliguswa na kutiwa nguvu nilipotembelea maeneo ya chimbuko la mapinduzi ya China, kutoka kituo cha mwanzo cha Safari Ndefu ya Jeshi Jekundu huko Yudu mkoani Jiangxi hadi Jumba la Makumbusho ya Makao Makuu ya Mapinduzi ya mikoa ya Hubei-Henan-Anhui lililoko huko Xinxiang mkoani Henan, kutoka Mnara wa kumbukumbu ya Jeshi la Upande wa Magharibi huko Gaotai mkoani Gansu hadi eneo la kumbukumbu ya mapinduzi lililoko katika mlima wa Xiangshan mjini Beijing, kila sehemu kati ya hayo imenikumbusha kuwa, lengo la asili na jukumu ni nguvu isiyoisha ya kutusukuma mbele kwenye Safari Ndefu katika zama mpya.

    Kama kawaida, bila kujali nina pilikapilika kiasi gani, nilitafuta nafasi za kuwatembelea wananchi wa maeneo mbalimbali. Waliniambia mambo mengi ya moyoni, ambayo pia nimeyaweka moyoni mwangu. Ndugu wa kabila la Dulong katika eneo la Gongshan mkoani Yunan, wanavijiji katika tarafa ya Xiadang wilaya ya Shouning mkoani Fujian, askari wa Kikosi cha Wang Jie, wanafunzi wa darasa la mabingwa wanaosoma shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Michezo cha Beijing, watoto wa Macao na wazee wanaojitolea, waliniandikia barua. Nilipowajibu, nimepongeza mafanikio waliyoyapata, na pia kuwatumia salamu zangu.

    Katika mwaka mmoja uliopita, watu wengi na mambo mengi yalitugusa. Zhang Fuqiang ambaye ameshikilia nia yake ya asili bila kujali sifa na hadhi katika maisha yote, Huang Wenxiu aliyejitolea maisha yake kwenye mapambano dhidi ya umaskini, mashujaa 31 kutoka Muli mkoani Sichuan waliopoteza maisha yao kwa ajili ya kuzima moto mkubwa, Du Fuguo ambaye alimlinda askari mwenzake kwa mwili wake, na timu ya voliboli ya wanawake ya China iliyonyakua ubingwa wa Kombe le Dunia kwa ushindi 11 mfululizo……Mashujaa wengi wasiojulikana ambao wamechangia jasho, damu na hata maisha yao bila kusita wala kujuta, wakiwa watu wa kawaida, wameandika historia ya maisha yasiyo ya kawaida.

    Mwaka 2019, China iliendelea kufungua mikono yake na kukumbatia dunia. Tumeandaa Mkutano wa pili wa Baraza la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo cha Bustani ya Beijing, Mkutano wa Mazungumzo kati ya Staarabu za Asia, na Maonesho ya Pili ya Bidhaa zinazoagizwa na China kutoka Nje CIIE, ambavyo vimeonesha kwa dunia jinsi China iliyo na ustaarabu, uwazi na shirikishi. Nilikutana na wakuu na viongozi wa nchi mbalimbali, niliwaelezea mapendekezo ya China, ambapo tulizidisha urafiki na kufikia maoni ya pamoja. Baadhi ya nchi zimeanzisha uhusiano wa kibalozi na nchi yetu, na kuifanya idadi ya nchi zenye uhusiano wa kibalozi na China kufikia 180. Marafiki zetu wako kila mahali duniani!

    Mwaka 2020 utakuwa ni mwaka muhimu katika historia. Tutakamilisha kwa pande zote ujenzi wa jamii yenye maisha bora, na kutimiza lengo la maendeleo la "Miaka 100 ya Kwanza". Mwaka 2020 pia utakuwa ni mwaka wa kunyakua ushindi wa mwisho kwenye mapambano magumu ya kutokomeza umaskini. Baragumu limelia. Tunapaswa kushikamana na kufanya juhudi kwa pamoja, na kuthubutu kusonga mbele katika maeneo magumu, tunapaswa kuendelea kuongeza zaidi uwezo wetu katika nyanja zilizokuwa dhaifu, na kuimarisha zaidi msingi wetu, ili kuweza kushinda kithabiti na kikamilifu vita dhidi ya umaskini, na kutimiza lengo la kuwafanya watu wote maskini vijijini waondokane na umaskini, na kuzifanya wilaya zote maskini zijiondoe kwenye orodha ya maeneo maskini.

    Hivi karibuni, nilihudhuria shughuli za maadhimisho ya miaka 20 tangu Macao irudi China, nimefurahia kuona utulivu na ustawi mkoani Macao. Uzoefu wa mafanikio ya Macao umedhihirisha kuwa, sera ya "Nchi Moja, Mifumo Miwili" inaweza kutekelezwa, kufanikiwa na kuungwa mkono na watu. Katika miezi ya karibuni, hali ya mkoani Hongkong inafuatiliwa na kila mwananchi. Bila kuwa na mazingira ya utulivu na masikilizano, kamwe hakutakuwa na jamii ambayo watu wanafanya kazi na kuishi maisha yao kwa furaha. Nawatakia kwa dhati kila la heri Hongkong na watu wake. Utulivu na ustawi wa Hongkong ni matumaini ya ndugu wa Hongkong, na pia ni matarajio ya wananchi wa China.

    Historia huwa inapiga hatua bila kusita, kukiwa na utulivu na pia mawimbi makali. Hatuogopi mvua na upepo, na wala hatuogopi vikwazo na vizuizi. China itafuata kithabiti njia ya kujiendeleza kwa amani, na kulinda kithabiti amani ya dunia na kuhimiza maendeleo ya pamoja. Tungependa kushikana mikono na watu wa nchi mbalimbali duniani katika kujenga kwa pamoja "Ukanda Mmoja, Njia Moja", kusukuma mbele ujenzi wa Jumuiya ya Binadamu yenye Mustakabali wa Pamoja, na kufanya juhudi bila kusita kwa ajili ya mustakabali mzuri wa binadamu wote.

    Wakati huu, bado kuna watu wengi wanaoendelea na kazi zao, wengi wakiwa wanalinda usalama wetu, wengine wanafanya kazi kwa bidii. Poleni na kazi!

    Tufanye juhudi kwa nguvu zote bila kusita, na kuukaribisha kwa pamoja ujio wa mwaka 2020.

    Nawatakia heri ya mwaka mpya!

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako