• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kenya imethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya COVID-19 au Corona.

    (GMT+08:00) 2020-03-13 18:44:09

    Serikali ya Kenya imethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya COVID-19 au Corona. Waziri wa Afya Mutahi kagwe ijumaa alithibitisha kuwa mgonjwa huyo ni mkenya ,mwanamke wa miaka 27,aliyesafiri kutoka Chicago,Marekani kupitia London,Uingereza.

    Katika mkutano na wanahabari ijumaa mchana,Waziri wa Afya wa Kenya,Mutahi Kagwe alitangaza na kuthibitisha kupatikana kwa kisa cha virusi vya Korona nchini.

    "Wakenya wenzangu,nataka kuwafahamisha kwamba Wizara ya Afya imethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya korona nchini Kenya.Kisa hicho kilithibitishwa tarehe 12,jana usiku,kama kisa cha kwanza kuripotiwa nchini Kenya"

    Alisema kuwa japokuwa mgonjwa huyo anaendelea vizuri na anakula,hatatolewa hospitali hadi vipimo vithibitishe hana dalili zozote za ugonjwa huo.

    "Kisa hicho ni cha mwanamke raia wa Kenya,ambaye alisafiri kurudi Nairobi kutoka nchini Marekani,kwa kupitia London,Uingereza,tarehe 5 machi 2020.Alithibitishwa kuwa na virusi vya Corona na maabara ya Kitaifa ya Mafua,katika maabara za kitaifa za afya ya umma katika Wizara ya Afya.Ningependa kutoa msisitizo kuwa mgonjwa yuko salama,vipimo vya joto la mwilini vimeshuka,anakula,lakini hawezi kutolewa hospitali hadi vipimo viendelee na kuthibitishwa kuwa hana kabisa dalili zozote za virusi"

    Mwanamke huyo amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Kenyatta.

    Serikali pia imesema kuwa imewatambua watu wote ambao mwanamke huyo alitangamana nao tangu kuwasili nchini Kenya tarehe 5 Machi.

    Waziri wa Afya Mutahi kagwe aidha alitoa wito kwa wakenya wote kushirikiana na kudumisha usafi ili kupiga vita virusi vya corona.

    Alitoa wito kwa wafanyabiashara wote na wahudumu wa magari ya usafiri wa umma kuweka sabuni za kuosha mikono na vifaa vya kupima joto.

    Alisema kwa sasa hakuna haja yoyote ya kuwa na wasiwasi au hofu na kusisitiza watu wafuate kanuni na taratibu zilizowekwa kuhusu kujikinga na virusi vya korona.

    Alitoa wito kwa wakenya kuosha mikono yao vizuri kwa kutumia sabuni na kukaa umbali wa mita moja na mtu anayechemua au kukohoa.

    Pia mtu anayekohoa au kuchemua anahimizwa kukaa nyumbani na kutokwenda sehemu yenye watu wengi.

    Pia Waziri Kagwe alisema serikali imesitisha mikutano yote ya hadhara,michezo.Shule zitaendelea lakini michezo ya shule imefutwa.Pia ziara za kwenda kuwatembelea walio magerezani zimesitishwa kwa muda wa siku 30 zijazo.

    Waziri Kagwe pia alitoa onyo kwa wakenya dhidi ya kusambaza habari za uongo katika mitandao ya kijamii.Wakenya waliombwa kutotumia vibaya mitandao hiyo na kushiriki katika vitendo ambavyo vitaleta hofu na wasiwasi.

    Nchi zilizoathirika barani Afrika kufikia sasa ni Algeria,Burkina Faso,Cameroon,DRC,Misri,Morocco,Nigeria,Senegal,Afrika Kusini,Togo,Tunisia,na Kenya.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako