Kocha Mkuu wa timu ya Gor Mahia ya Kenya, Steven Polack amesema wachezaji wa timu hiyo hawafai kumlaumu kwa kutowapigania walipwe malimbikizo ya mishahara yao wakati huu wa janga la virusi vya corona. Polack amesikitishwa na ripoti kwamba wanasoka wake wanamlaumu kwa kuwa kimya huku wakiendelea kuteseka kwa kutolipwa fedha zao kwa miezi kadhaa. Aidha ripoti hizo zilidai wachezaji hao wamekuwa wakipigania walipwe fedha zao kivyao huku kocha huyo akionekana kutoshughulishwa na suala hilo. Hata hivyo, Polack amejitetea akisema kwamba amekuwa akiusukuma uongozi wa Gor uwalipe wachezaji wake mishahara, akifichua kwamba hata yeye pia hajalipwa fedha zake. Kocha huyo raia wa Uingereza aliwashutumu baadhi ya watu wasiofurahia uwepo wake klabuni humo kama wanaochochea wachezaji dhidi yake ilhali yeye huwa halipi mishahara. Aidha alitishia kuwafichua watu ambao wamekuwa wakiwahangaisha wachezaji hao wanapojaribu kufikia uongozi wa klabu kudai hela zao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |