• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mkutano wa kilele wa ushirikiano wa China na Afrika katika mapambano dhidi ya COVID-19 watoa taarifa ya pamoja

    (GMT+08:00) 2020-06-18 09:00:44

    Kutokana na pendekezo la pamoja la China, nchi mwenyekiti ya zamu ya Umoja wa Afrika, Afrika Kusini, na nchi mwenyekiti ya pamoja ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ya upande wa Afrika, Senegal, viongozi wa China na nchi za Afrika walifanya Mkutano maalumu wa kilele kuhusu ushirikiano kwenye mapambano dhidi ya virusi vya Corona kwa njia ya video, na kutoa taarifa ya pamoja.

    Kwenye taarifa hiyo, pande mbalimbali zimesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa dunia, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa iimarishe mshikamano na ushirikiano, ili kuzuia na kupunguza kwa pamoja maambukizi ya virusi, na kuzingatia mahitaji ya watu wenye matatizo.

    Taarifa imepongeza mchango wa ushirikiano kati ya China na Afrika katika kuhimiza maendeleo ya Afrika na kuboresha maisha ya wananchi, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa misaada mingi zaidi ya vifaa, teknolojia, fedha na ya kibinadamu, ili kuisaidia Afrika kupunguza athari za janga la virusi vya Corona na kutimiza maendeleo endelevu. Pia China itatekeleza pendekezo la kundi la nchi 20 la kusimamisha ulipaji wa madeni kwa nchi zilizo nyuma kimaendeleo, na kuongeza nguvu ya kutoa misaada kwa nchi za Afrika zilizoathirika zaidi katika mlipuko wa virusi vya Corona.

    Rais Xi Jinping wa China ametoa hotuba kwenye Mkutano wa Kilele wa Mshikamano na Ushirikiano katika kupambana na COVID-19, akisema,

    "Katika wakati huu muhimu dunia inapopambana na virusi vya Corona, tunapaswa kukusanyika pamoja katika Mkutano huu Maalum wa Kilele wa China na Afrika. Marafiki wa zamani na wapya wanaunganishwa kwa njia ya video kujadili majibu yetu ya pamoja juu ya virusi vya Corona na kuleta upya undugu kati ya China na Afrika. Ninawashukuru Rais Cyril Ramaphosa na Rais Macky Sall kwa kuungana nami katika kuandaa mkutano huu, na ninapongeza ushiriki wa wengine wote mliopo. Pia ninataka kutuma salamu zangu kwa viongozi wengine wa Afrika ambao hawakuweza kuwa nasi hii leo.

    Mlipuko wa ghafla wa COVID-19 umekuwa mzigo mkubwa kwa nchi mbalimbali duniani, huku malaki ya maisha ya thamani yakipotea. Hapa, ninapendekeza kuwa tuwe na muda wa kukaa kimya kuwakumbuka wale waliofariki kutokana na COVID-19, na kutoa rambirambi zetu kwa familia zao.

    Katika janga la COVID-19, China na Afrika zimevumilia majaribio ya changamoto kubwa. Watu wa China wamepambana vikali na kujitolea kwa kiasi kikubwa kudhibiti hali nchini China. Bado, tuko makini kutokana na hatari ya mlipuko huo kutokea tena. Katika moyo huohuo, serikali na watu wa Afrika wamesimama kwa pamoja, chini ya uratibu wa Umoja wa Afrika, wamechukua hatua kali kupunguza kasi ya uenezi wa virusi. Haya kweli ni matokeo ambayo hayakupatikana kwa urahisi.

    Katika janga ka COVID-19, China na Afrika zimeungana mkono na kupambana bega kwa bega kwa pamoja. Daima China itakumbuka uungaji mkono wa thamani uliotolewa na Afrika wakati wa mapambano dhidi ya virusi vya Corona. Kutokana na hilo, wakati Afrika iliposhambuliwa na virusi hivyo, China ilikuwa ya kwanza kuharakisha kwa kupeleka misaada, na tangu wakati huo, China imesimama kithabiti na watu wa Afrika.

    Katika janga la COVID-19, China na Afrika zimeboresha mshikamano na kuimarisha urafiki na kuaminiana. Ngoja nirejee tena ahadi thabiti ya China kwa urafiki wake wa muda mrefu na Afrika. Bila kujali mazingira ya kimataifa yanavyoweza kubadilika, China kamwe haitasita katika nia yake ya kutafuta mshikamano zaidi na ushirikiano na Afrika.

    COVID-19 bado inaendelea kuathiri sehemu nyingi duniani. China na Afrika zote zinakabiliwa na kazi ngumu ya kupambana na virusi wakati zikituliza uchumi na kulinda ajira za watu. Daima tunapaswa kutanguliza na kusimamia watu na maisha yao kwanza. Lazima tukusanye rasilimali muhimu, kuungana pamoja kufanya uratibu, na kufanya kila linaowezekana kulinda maisha ya watu na afya zao na kupunguza athari za COVID-19.

    Kwanza, lazima tudumu kwenye nia thabiti ya kupambana na COVID-19 kwa pamoja. China itaendelea kufanya linalowezekana kuunga mkono juhudi za Afrika kupambana na COVID-19. China haitapoteza muda kufuatilia hatua nilizozitangaza katika ufunguzi wa Mkutano wa Afya Duniani, na kuendelea kuzisaidia nchi za Afrika kwa kutoa vifaa, kupeleka timu za wataalam, na kuwezesha Afrika kununua vifaa vya matibabu kutoka China. Mwaka huu, China itaanza kabla ya wakati uliopangwa ujenzi wa makao makuu ya Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika. China itafanya kazi na Afrika kutimiza kikamilifu pendekezo la huduma ya afya lililotolewa katika Mkutano wa FOCAC uliofanyika Beijing, na kuongeza kasi ya ujenzi wa Hospitali za Urafiki kati ya China na Afrika na ushirikiano kati ya hospitali za China na Afrika. Pamoja, tutajenga jamii ya China na Afrika yenye afya bora kwa wote. Tunaahidi kuwa mara matengenezo na utoaji wa chanjo ya COVID-19 itakapomalizika nchini China, nchi za Afrika zitakuwa kati ya nchi za mwanzo kufaidika.

    Pili, lazima tudumishe ahadi ya kuimarisha ushirikiano wa China na Afrika. Ili kupunguza athari za COVID-19, ni muhimu kuongeza ushirikiano wa Ukanda Mmoja na Njia Moja, na kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa matokeo ya mkutano wa FOCAC wa Beijing. Kipaumbele kikubwa kinatakiwa kutolewa kwa ushirikiano katika afya ya umma, kufungua tena uchumi, na maisha ya watu.

    Ndani ya mfumo wa FOCAC, China itafuta madeni ya nchi husika za Afrika yaliyo katika aina ya mikopo isio na riba kwa serikali ambayo muda wake utatimia mwishoni mwa mwaka 2020. Kwa zile nchi za Afrika ambazo zimeathiriwa zaidi na virusi vya Corona na zina shinikizo kubwa la kifedha, China itashirikiana na jamii ya kimataifa kuziunga mkono zaidi, kwa njia kama kuongeza muda wa kulipa madeni, ili kuzisaidia kukabiliana na hali ngumu ya sasa. Tunazitaka taasisi za kifedha za China kutumia Pendekezo la G20 la Kusitisha Ulipaji wa Madeni (DSSI) na kufanya majadiliano ya kirafiki na nchi za Afrika ili kuweka mpango kuhusu madeni ya kibiashara na mamlaka husika za kifedha. China itafanya kazi na nchi nyingine wanachama wa G20 kutekeleza Pendekezo hilo, na kwa msingi huo, kuitaka G20 kuongeza muda wa ulipaji wa madeni mpaka baadaye kwa nchi husika, zikiwemo zile za Afrika.

    China inatarajia kuwa jamii ya kimataifa, hususan nchi zilizoendelea na taasisi mbalimbali za kifedha, zitachukua hatua zaidi za kupunguza na kusitisha madeni kwa nchi za Afrika. China itashirikiana na Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Duniani, na wenzi wengine kusaidia Afrika kupambana na COVID-19, na kufanya hivyo kwa njia inayoheshimu matakwa ya Afrika.

    Katika hayo yote, kinachojalisha zaidi ni kuisaidia Afrika kutimiza maendeleo endelevu. China inaunga mkono Afrika katika juhudi zake za kuanzisha Eneo la Biashara Huria la Afrika na kuboresha maingiliano na kuongeza nguvu ya mnyororo wa kiviwanda na ugavi. China itatafiti ushirikiano mpana zaidi na Afrika katika aina mpya za biashara kama uchumi wa kidijitali, miji ya kisasa, nishati safi, na teknolojia ya 5G ili kukuza na kuchochea upya maendeleo ya Afrika.

    Tatu, lazima tudumishe nia ya kusimamia mfumo wa pande nyingi. Katika janga hili la COVID-19, mshikamano na ushirikiano ni silaha yenye nguvu zaidi. China itashirikiana na Afrika kudumisha mfumo wa uongozi wa dunia ambao kiini chake ni Umoja wa Mataifa na kuunga mkono WHO katika kutoa mchango mkubwa zaidi katika mapambano ya dunia dhidi ya COVID-19. Tunapinga kuingiza siasa na ubaguzi kuhusu COVID-19, na tunapinga ubaguzi wa rangi na upendeleo wa kiitikadi. Tunasimama kithabiti kwa ajili ya usawa na haki duniani.

    Nne, lazima tudumu kwenye lengo la kuendeleza zaidi urafiki kati ya China na Afrika. Dunia inapitia mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kuonekana kwa mwongo mzima. Kutokana na fursa mpya na changamoto tunazokabiliana nzo, ushirikiano wa karibu kati ya China na Afrika unatakiwa, kuliko ilivyokuwa zamani. Kwa upande wangu, nitaendelea kuwasiliana kwa karibu na nyie wote, wenzangu, kuimarisha urafiki wetu na kuaminiana, kuungana mkono katika masuala yanayohusu maslahi yetu muhimu, na kuendelea maslahi ya kimsingi ya China na Afrika, na, kwa hilo, nchi zote zinazoendelea. Kwa njia hii, tutaweza kupeleka uhusiano wa ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Afrika katika ngazi ya juu zaidi.

    Katika mkutano wa kilele wa FOCAC uliofanyika Beijing, tulikubaliana kufanya kazi kwa pamoja kujenga jamii yenye nguvu zaidi ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja. Mkutano Maalum wa leo wa Mshikamano China na Afrika dhidi ya COVID-19 ni hatua yetu thabiti ya kutimiza ahadi tuliyotoa katika Mkutano wa Beijing na kuchukua nafasi yetu katika ushirikiano wa kimataifa dhidi ya COVID-19. Ninaamini kuwa ubinadamu hatimaye utashinda virusi, na kwamba watu wa China na Afrika wako tayari kukumbatia siku nzuri za baadaye. "

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako