• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Je, Kenya italeta manufaa gani kwa Afrika baada ya kujipatia kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa?

    (GMT+08:00) 2020-06-22 08:38:47

    Kenya imepata kiti muhimu cha uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuishinda Djibouti katika awamu ya pili ya kupiga kura Alhamisi. Hii inamaanisha kuwa kuanzia Januari 2021, Kenya itarejesha uwepo wake utakaodumu kwa miaka miwili katika asasi hiyo ya Umoja wa Mataifa baada ya miaka 23, ambapo itasaidia kufanya maamuzi muhimu kuhusu usalama na amani duniani. Mafanikio hayo ya Kenya kwenye kinyan'ganyiro hicho yanamaanisha kuwa sasa itakaa na nchi nyingine mbili za Afrika ambazo ni Tunisia na Niger, zote mbili zikiwa zimechaguliwa kuwa wanachama wasio wa kudumu kwa kipindi cha miaka miwili katika mwaka wa 2021. India, Mexico, Ireland na Norway zilichaguliwa hapo Jumatano.

    Sababu ya ushindi wa Kenya:

    Baraza la Usalama ni chombo cha kusimamia amani na usalama duniani. Na Kenya kwa muda mrefu imeshiriki kwenye diplomasia ya pande nyingi, mbali na kuimarisha mchakato wa demokrasia ya ndani ya nchi, pia imetoa michango muhimu kwa amani ya kikanda, haswa katika kuleta amani nchini Somalia. Kwa mujibu wa balozi wa Kenya nchini China Bibi. Sarah Serem, nchi hiyo imetoa makazi kwa wakimbizi zaidi ya laki 6 kutoka Somalia, Sudan Kusini na sehemu nyingine za Afrika, na pia kushiriki kwenye majukumu ya kulinda amani katika nchi 40. Kenya ina kambi kubwa zaidi za kulinda amani za kimataifa zenye historia ndefu barani Afrika; Kenya pia ni makao makuu ya mashirika mengi ya kikanda na kimataifa na ina uzoefu mkubwa katika kuandaa mikutano ya kimataifa. Safari hii Kenya imeungwa mkono sana na Umoja wa Afrika katika kuipigia debe kuwania kiti cha uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jambo ambalo linaonesha kuwa Umoja wa Afrika una imani kubwa na Kenya.

    Matokeo ya ushindi wa Kenya:

    Habari hizi njema zilipokelewa kwa furaha kubwa na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambaye amesema hii inaonesha kwamba Kenya sasa imepevuka na ina ushawishi mkubwa kwenye jamii ya kimataifa ikiwa kama nchi imara na mshirika wa maendeleo anayetegemewa.

    China ni nchi mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama, na siku zote inatetea maslahi ya nchi za Afrika katika chombo hicho cha Umoja wa Mataifa. Naamini kuwa katika kipindi hiki cha miaka miwili kuanzia Januari mwakani wakati Kenya ni mwanachama, nchi hizo mbili zitatoa michango yao kwa pamoja katika kulinda amani na usalama barani Afrika na hata dunia nzima.

    Kwa muda mrefu, kumekuwa na wito wa kulifanyia mageuzi baraza la usalama. Hivyo ikifanya kazi pamoja na nchi hizo tano wanachama wa kudumu zikiwemo Russia, Uingereza, Marekani, China na Ufaransa zenye uwezo wa kupiga kura ya turufu, Kenya pia itaungana na nchi nyingine tisa wanachama wasio wa kudumu na inaweza kupata hata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa muda wa baraza hilo, fursa ambayo ni muhimu katika kupenyeza ajenda muhimu za kiushawishi.

    Kenya imeahidi kutetea mageuzi ili kulifanya Baraza la Usalama liwe na uwakilishi zaidi na jumuishi, na kwa upande wa Afrika mageuzi hayo ni kuongeza viti vya kudumu na visivyo vya kudumu kwenye Baraza la Usalama kwa nchi za Afrika, lakini lengo hilo bado halijafanikiwa. Je, Kenya itaweza kuleta miujiza na kulishawishi baraza hilo kukubali kuongeza viti kwa Afrika? Hili ni swali ambalo itabidi tusubiri matokeo yake katika kipindi hiki ambacho Kenya inakalia kiti kwenye baraza hilo .

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako