• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • SOKA: Real Madrid yasajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Getafe

    (GMT+08:00) 2020-07-03 18:05:08

    Penalti iliyopigwa na beki Sergio Ramos katika dakika ya 79 iliwawezesha Real Madrid kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Getafe Julai 2, 2020 na kufungua pengo la alama nne kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Hadi beki Mathias Olivera wa Getafe alipomchezea Dani Carvajal visivyo ndani ya msambamba na kuchangia penalti, dalili zote ziliashiria kwamba Real wangelazimishiwa sare tasa katika mechi hiyo iliyochezwa uwanjani Alfredo di Stefano. Penalti hiyo ilikuwa ya 21 kwa nahodha Ramos kupiga akivalia jezi za Real. Getafe ambao wanapigania nafasi ya kunogesha kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao walianza mechi dhidi ya Real kwa hamasa kubwa huku kipa Thibaut Courtois akilazimika kupangua makombora matano aliyoelekezewa na wavamizi wa Getafe chini ya dakika 15 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza. Gozi hilo lilitawaliwa na hisia na makabiliano makali huku jumla ya wachezaji 10 wakionyeshwa kadi za manjano. Real walionekana kulemewa kabisa na wageni wao huku majaribio yao mawili pekee langoni pa Getafe kabla ya penalti iliyofungwa na Ramos yakitokana na juhudi za kiungo Luka Modric na mshambuliaji Karim Benzema. Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real kwa sasa wanahitaji kusajili ushindi katika mechi nne kati ya tano zilizosalia katika kampeni za La Liga msimu huu ili kuwapiga kumbo mabingwa watetezi Barcelona na kutia kapuni taji lao la kwanza la soka ya Uhispania tangu 2012. Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa msimamo wa ligi kwa alama 74, nne zaidi kuliko Barcelona waliolazimishwa sare ya 2-2 kutoka kwa Atletico Madrid katika mchuano wao wa mwisho.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako